Maisha hayana fomula ila yanakuhitaji uwe na fomula


Siku moja dereva mmoja wa bodaboda alikuwa anaendesha bodaboda yake kutoka eneo moja kwenda  jingine. Akiwa njiani, alipata ajali akawa ameanguka chini. watu walikimbia haraka kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanamsaidia. Kitu cha kwanza watu walichoona ni shingo kupinda. Hivyo, walianza harakati za kumpa huduma ya kwanza na hapa waliamua kurudsha shingo kwenye eneo lake.

Dereva akawa amejitahidi kuwaambia kwamba shingo yake ilikuwa haijapinda kugeuikia nyuma, badala yake alikuwa amevaa koti vifungo amefungia nyuma.

Kwa vile alikuwa amepata ajali, watu walidhani hicho ni kiwewe tu cha ajali, hivyo dereva anaongea chochote tu kinachokuja kichwani mwake. Wakageuza shingo ii iangalie vifungo vilipo maana huko ndiko walijua kwa hakika ndipo shingo ilipaswa kuwa imeangalia, mwisho wa siku dereva akawa ameaga dunia.

Tunachopata hapa ni kwamba maisha hayana fomula, ila wewe kama mtu binafsi unapaswa kuwa na fomula kwenye mambo yako. Kinachowakwamisha watu wengi kwenye maisha ni kwa sababu wanaishi maisha yasiyokuwa na fomula. Wanaishi tu ilimradi wameishi.  Unapaswa kuyaendea  maisha kwa fomula na haya hapa ni mambo yatakayokusaidia wewe kuwa na fomula

Kwanza ni kuwa na malengo.

Malengo ni fomula ambayo mtu binafsi unajiwekeaa. Hii ni fomula muhimu sana kwa sababu unapoweka malengo, maana yake unakuwa unajichagulia wapi unataka kwenda na wapi unataka kufika kwenye maisha. Unapoweka malengo maana yake, unakuwa unaamua ni kitu gani ambacho unataka kufikia kwenye maisha na kitu gani hutaki. Unatengeneza fomula ya maisha yako kwa sababu, bila ya hii fomula utajikuta kwamba unafanya kitu chochote kile kinachokuja mbele yako.

Ila unapokuwa na malengo, maana yake unaachana na baadhi ya vitu na kuweka nguvu yako kwenye vitu vichache vyenye nguvu.

Pili kwa kuipangilia kila siku yako na kila wiki yako.

Hivi huwa unaweka to do list na kuorodhesha majukumu ambayo unapaswa kufanya ndani ya siku husika. Kama ulikuwa huweki hii orodha ya mjukumu yako ya kufanya ndani ya siku husika basi unapaswa kuanza kufanya hivyo kuanzia siku ya leo. Unajua kwa nini? Kwa sababu unapoweka to do list maana yake, unakuwa unachagua majukumu machache ambayo utafanya ndani ya siku husika na hivyo kuachana na majukumu yaliyo mengi.

Tatu ni kwa kufanya tathimini. Tathimini ni pale ambapo unaangalia yale uliyoyafanya na namna yalivyokwenda. Ni pale unapoangalia na kuona kama uliyoyafanya yameleta tija na yanapaswa kuendelea kufanywa zaidi au la unapaswa kuishia hapo. maisha yako yanapaswa kuwa na tathimini ya siku, wiki, mwezi mpaka mwaka. Usiishi maisha bila ya tathmini. Hakikisha kwambna kila wiki na kila mwezi unakuwa na tathmini. Fanya tathimini yako na kila unapopata jambo la kuboresha, basi liboreshe na lifanyie kazi katika kuhakikisha kwamba  unazidi kuwa bora zaidi. lakini kikubwa zaidi unazidi kufanya maisha yako yawe na fomula.

Kila la kheri

Ni mimi rafiki yako wa ukweli

Godius Rweyongeza

0755848391

Morogoro-Tz


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X