Usiweke bajeti kwenye AKILI yako.


Kama umeanza kufanya hivyo, basi kuanzia leo iondoe bajeti hiyo maana ni kikwazo kikubwa sana. Akili yako itumie kubuni vitu vipya, itumie kufikiria mbinu mpya za kutatua matatizo, itumie kuongeza MAUZO kwenye biashara.

Tafiti nyingi zimefanyika na tafiti hizi mara zote zimekuja na jibu moja kuwa watu wengi wanatumia chini asilimia kumi ya uwezo wao. Kwa hiyo, ukikutana na mtu ambaye ameweza kufanya vitu ambavyo unaviona kwamba ni vikubwa, jua kwamba hajatumia hata asilimia 15 ya uwezo wake, bado anachezea chini ya asilimia kumi. Sasa ebu fikiria na wewe ukiweza kutumia hata asilimia 10 tu ya uwezo au akili yako. Unadhani utafika wapi?

Kama hawa wanasayansi wote ambao wamefanya makubwa au hawa wana wagunduzi, wote wametumia chini ya asilimia kumi, na wewe ukiongeza uwezo wako kidogo si unaweza hata kuwafikia?

James William aliwahi kunukuliwa akisema kwamba, kulinganisha na vile tunavyopaswa kuwa, watu bado wamelala.

Yaani, bado uko usingizini, hujaweza kutumia uwezo wako kadiri inavyotakiwa.

Ubora wa vitu hivi ni kwamba hakuna hata kimoja ambacho unaweza kusema kwamba nimekitumia mpaka kimeisha. Kipaji hakitumiki mpaka kikaisha, ujuzi wako hautumiki mpaka ukaisha, kadiri unavyotumia kipaji chako, ndivyo ambavyo kinazidi kuwa bora zaidi, kadiri unavyotumia akili yako, ndivyo ambavyo akili yako inazidi kuimarika zaidi. Anza leo hii kuvitumia.

Sasa unawezaje kutumia uwezo wako, akili au kipaji chako kwa viwango vikubwa?

Baada ya kusoma hapa nina hakika utaanza kusema kwamba ninataka nifike mbali, na ninataka nifanye makubwa. na ni kweli kabisa.

HATA HIVYO, unaweza kujikuta kwamba unatumia maarifa haya vibaya na mwisho wa siku unaishia kuangukia pua. Hapa nataka nikupe mwongozo sahihi ili usije ukaangukia pua.

Mara nyingi mwanzoni mwa mwaka watu huwa wanaweka malengo makubwa ya kufanya vitu vikubwa. Unakuta mtu kaweka malengo ya kukimbia, pengine baada ya kusikia habari kuwa kukimbia ni kitu muhimu kwa afya. Lakini siku ya kwanza tu mtu anakimbia kilomita tano, kesho yake anaamka akiwa hana hamu tena ya kukimbia, amechoka.

Sasa unachotakiwa kwenye kufanyia kazi kipaji na uwezo wako wa kiakili ni wewe kuhakikisha kwamba, unajiwekea lengo la kukua walau kwa asilimia moja kila kukicha. Yaani, kwamba leo hii uweze kuutumia uwezo wako kwa viwango vikubwa kidogo kulinganisha na vile ulivyoutumia jana. Kesho uutumie uwezo wako kwa asilimia moja zaidi ya vile ulivyoutumia leo. Kila siku walau utumie uwezo wako kwa asilimia moja juu zaidi ya vile ilivyokuwa jana.

Wajapani hiki kitu wanakiita kaizen au constant improvement. Yaani, kwamba kila mara na kila siku unahakikisha kwamba unajiongeza na kukua zaidi ya ilivyokuwa hapo jana.

Mfano, tuseme kwamba una lengo la kunoa kipaji chako cha uandishi. Unaanza kidogo kidgo na hakuna kurudi nyuma kila siku.

Leo unaamua kuanza kuandika maneno 10 tu ya ujumbe mfupi. Kesho unaongeza, maneno unaandika maneno kumi na tano.

Kesho kutwa maneno kumi na saba. Ila unakuwa haurudi nyuma. Unaendelea kukifanyia kazi kipaji chako bila ya kuchoka na bila ya kurudi nyuma.

Mimi nakuamini sana, nategemea kwamba baada ya hapa unaenda kutumia uwezo wako bila ya kurudi nyuma.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X