Kama Hujui Ni Kitu Gani Unapaswa Kufanya Maishani, Anzia Hapa


Inatokea kwamba watu wengine kwenye maisha wapo kwenye hali ambayo hawaelewi wanapaswa kufanya nini wala ni wapi wanapaswa kuelekea. Sasa kwenye makala ya leo naenda kuongea na watu wa aina hii na kuona ni kwa jinsi gani ambavyo wanaweza kutumia fursa zilizopo kwenye maisha kuhakikisha kwamba wanasonga mbele.

Hivyo, kama wewe haupo kwenye hali hii hapa basi unaweza ukaachana na makala hii ili usome nyingine ambazo zinakuhusu, ila endapo utaamua kuisoma makala hii kuna vitu viwili ambavyo nina uhakika kwamba utaondoka navyo.

Kwanza kuna kitu ambacho unaweza kujifunza kutoka kwenye andiko hili.

Pili unaweza kupata ushauri ambao siku nyingine unaweza kuutumia  kumsaidi amtu mwingine.

Upo tayari niendelee?

KAMA UPO KWENYE HALI AMBAYO HUELEWI NINI CHA KUFANYA

Ebu chukulia kwamba ndio umemaliza chuo na ulikuwa na matarajio makubwa kwamba baada ya chuo unaenda kuajiriwa sehemu na utapata mshahara mkubwa kutokana na kazi ambayo utakuwa unafanya. Ila sasa upo mtaani na huelewi ni kitu gani ambacho unaweza kufanya. Yafuatayo ni mambo muhimu ya kuzingatia.

Kwanza unapaswa kujua kwamba kukosa ajira siyo kwamba unakuwa umekosa kazi kabisa. Kazi zipo, badala yake unaweza kuanza kutumia kile ulichonacho

Anza kutumia elimu yako

Kama umesoma na una kiwango fulani cha elimu, usikae tu hovyo ukabweteka. Hiyo elimu yako kuna watu ambao inaweza kuwasaidia kwenye hali zao walizonazo. Hivyo, unaweza kuitumia elimu hiyo kuwasaidia watu wengine na watu wengine wanaweza kuwa tayari kukulipa.

Anza kutumia kipaji chako

Kwanza kipaji chako unakijua wewe? Kipaji chako ni sehemu nzuri ya kuanzia, unaweza kutumia kipaji chako kama sehemu ya kuanzia kutengeneza kipato, lakini pia kutengeneza mali zinazoshikika na zisizoshikika. Unaweza kutumia kipaji chako kuandaa video au igizo, mafunzo ya sauti, makala, vitabu, muziki, tovuti n.k na hivi vyote vikawa chanzo cha wewe kuanza kuingiza kipato.

Anza kutumia ujuzi wako

Kama umewahi kuajiriwa sehemu au umewahi kufanya kazi sehemu nyingine yoyote, jua kwamba una ujuzi tayari ambao unaweza kuanza kuutumia mtaani. Tatizo kuna watu wana ujuzi ila wanaudharau au wanajiona kwamba sio watu wa viwango hivyo vya chini, wao wanachotaka ni kazi ambazo watakuwa wanafanya huku kipupwe kikipita kwa mbaali.

Sikia nikwambie; kila mtu anapenda kazi za aina hiyo, ila unapokuwa katika hali ambayo huelewi, usichague kazi. kwa sasa kitu kikubwa tunchoshughulika nacho ni wewe kupata kitu ambacho unaweza kuanza nacho maishani mwako na hatimaye ukaweza kusonga mbele na kufikia viwango ambavyo umekuwa unavitamani kwa siku nyingi. Ndoto zako hizo kubwa zinawezekana ila kwa sasa fanyia kazi haya.

Anza kutumia konekisheni zako

Kuna watu ambao umekuwa unafahamiana nao kwa siku nyingi, watu hawa wanaweza kuwa msaada kwako kwenye maisha yako, watumie hawa. Konekisheni zako zinaweza kukusaidia kwenye kupata mtaji, kukuunganisha na mteja, kupata kazi n.k. angalia kwenye hao watu wako wote unaofahamiana nao, ni mtu gani ambaye anaweza kuwa msaada kwako.

Tumia muda wako

Si huna kitu cha kufanya. Uwekeze muda wako vizuri maana utakuja kukusaidia sana siku zijazo. Hivyo basi, hakikisha kwamba unautuia vizuri muda wako katika kujifunza. Usichoke kujifunza. utumie pia muda wako.

Tumia nguvu zako

Nguvu zako kwa sasa ndiyo mtaji mkubwa ambao unapaswa kuuutumia. Anza kuutumia kwa kufanya kazi za nguvu ili upate kipato.

Nimekwambia haya yote ili uweze kupata sehemu ya kuanzia kabisa. na pale utakapokuwa umepata sasa sehemu ya kuanzia ndipo tunaweza kuendelea mbele.

Hakikisha kwamba baada ya kupata sehemu ya kunzia huishii tu kwenye hiyo kazi.

Endelea mbele. Yaani, fanya hiyo kazi huku ukiwa na ndoto kubwa kwenye maisha yako.

Weka akiba kwa ajili ya ndoto yako kubwa.

Wekeza fedha zako kwenye maeneo kama hisa, hatifungani na vipande, nyumba za kupanga, mashamba n.k

Kuza kipato chako kwa kuanzisha biashara n.k.

Rafiki yangu naomba ufahamu kuwa haya yote niliyoyoasema hayatachukua muda mfupi, yatachukua muda kwelikweli. Ila ukweli ni kwamba, kama kweli utakuwa tayari kuweka kazi na kuachana na njia za mkato, kuna siku utafika.

Najua umekuwa unatumia njia za mkato kwa siku nyingi sasa, ila hazijaweza kukufikisha popote, sasa ni muda wako wewe kuweka kazi na kuachana na njia za mkato.

Kila la kheri


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X