Dhana Ya Riba Mkusanyiko Kwenye Kipaji


Hakikisha unasoma: Kipaji Ni Nini?

Mwanasayansi Albert Einstein aliwahi kunukuliwa akisema “riba mkusanyiko (compound interest) ni moja kati ya maajabu saba ya dunia”.

Dhana ya riba mkusanyiko imejengwa kwenye msingi kwamba vitu vidogo vidogo vidogo vinapokusanywa kwa pamoja kwa kipindi kirefu, basi inafikia hatua ambapo vitu hivyo vinatengeneza kitu kikubwa.

Ukitaka kunielewa vizuri zaidi nikupe tu mfano wa mtu aliyekuwa na mpango wa kuingia kwenye biashara ya nyumba za kupangisha ila hakuwa na mtaji.

Mtu huyu alikuwa ana uwezo wa kuingiza fedha kidogo kila mwezi. Hivyo, kwenye hiyo fedha kidogo alikuwa anawatafuta watoto waliokuwa wanaenda kuokota matofali yaliyopasuka kidogo kwa ajili yake, kisha anawalipa.

Watu walikuwa wanamwona kama mtu asiyekuwa na akili, ila yeye ndani kabisa alikuwa anajua wazi ni kitu gani ambacho alikuwa anataka kufanya.

Walipokuwa wanafikisha kiasi kikubwa cha matofali alikuwa anajenga jengo lake kwa kutumia hayo matofali ila sasa akiwa ameyaweka vizuri.

Alianza kujenga vyumba vidogodogo, kisha baada ya muda akawa ameanza kujenga nyumba kubwa na akawa ameanzisha kiwanda chake cha kufyatua matofali.

Dhana ya riba mkusanyiko inafanya kazi hivi pia, kwenye kipaji. Unaweza kuona kama kufanya mazoezi leo hakutakuwa na maana.

Ila ukweli ni kwamba, kipaji chako hakijengwi kwa siku moja kama ambavyo huwezi kujenga misuli yako ndani ya siku moja. Badala yake ule mkusanyiko wa vitu na mazoezi ambayo unakuwa unafanya kwa ajili ya kipaji chako ndio kwa pamoja unaleta matokeo makubwa.

Kwa hiyo, jitoe kila siku kuhakikisha unakifanyia kazi kipaji chako. Kama itatokea kuwa unaenda kulala, ila ukakumbuka kuwa siku hiyo hukufanya kitu ili kukuza kipaji chako, hairisha kulala kwa dakika hata kumi, ili kwanza ufanye kitu kinachoendana na kipaji chako.

Njia nzuri ya kufanyia kazi kipaji chako ni kuhakikisha kuwa unaweka muda kwenye ratiba yako ambao utautumia kufanyia kazi kipaji chako. Na muda huo ukifika acha kila kitu. Weka nguvu kwenye kipaji chako kwanza.

Naipenda sana hadithi ya hekalu kubwa hapa duniani.

Taj Mahal, lilijengwa kwa miaka 22. Na kila siku kuna kitu cha kipekee ambacho kilikuwa kinaongezwa, siku nyingine tofali. Siku nyingine jiwe, siku nyingine nondo n.k .

Baada ya miaka 22 ya kulifanyia kazi lile jengo kila siku, ndio likatokea kuwa ni jengo bora.

Na wewe kipaji chako kinaweza kuchukua muda kuanza kukulipa au kutambulika, usiogope.

Endelea kukifanyia, siku nguvu ya riba mkusanyiko ikikaa pamoja, utafurahi sana.

Kupata Vitabu Vyangu BONYEZA HAPA au piga 0755848391

soma zaidi: Kipaji Ni Nini?

Mambo Matatu Usiyoyafahamu Kuhusu Kipaji

KUZA KIPAJI CHAKO

Muda sahihi Unaopaswa Kuendeleza Kipji chako


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X