Dibaji ya kutoka sifuri mpaka kileleni Kama Ilivyoandikwa Na Albert Nyaluke Sanga


 

Habari ya siku ya leo rafiki yangu. Siku ya leo nimeona nikusogee walau kurasa chache kutoka kwenye kitabu cha kutoka sifuri mpaka kileleni ili uweze kuzisoma. Na kwa leo nimekuletea kwako Dibaji ya kitabu cha KUTOKA SIFURI MPAKA KILELENI  ambayo imeandikwa na Albert Nyaluke Sanga.

Kama hujawahi kusoma kitu chochote kile kwenye kitabu hiki, basi walau unaweza kusoma Dibaji hii hapa, nina uhakika itakupa mwanga wa kitu ambacho kimeandikwa ndani ya kitabu. Karibu sasa uisome

 

Nimepata wasaa wa kusoma vitabu vingi sana katika maeneo ya maendeleo binafsi na ukuaji wa kifikra hata hivyo nikiri kwamba nilipokishika kitabu hiki nikasema wawooo! Nimejikuta nakisoma tena na tena, sio ili nipate cha kukisemea bali nimejikuta ninavutiwa na kuguswa mno na mpangilio, muundo na maarifa ya kina ambayo mwandishi ameyawasilisha.

 

Mwandishi, ameingia katika orodha ya waandishi wachache na adhimu sana katika lugha ya Kiswahili, wanaoandika aina hii ya maarifa. Jambo kubwa la kujivunia katika kitabu hiki ni kwamba mwandishi amefanya utafiti wa kina na kuwasilisha maarifa kwa namna yake. Naweza kusema hiki ni kitabu kilichojipambanua mno kwa maana kwamba hakikufanyiwa tafsiri ya waliyoandika wengine bali kimeleta mawazo halisi na uvumbuzi wa mwandishi. Kongole kwa mwandishi!

 

Ni hakika kwamba muda huwa haubadilishi chochote, bali unachokifanya ndani ya muda ndicho huamua mabadiliko utakayoyapata. Mwandishi katika kitabu hiki ameeleza kwa namna ya kipekee namna bora ya kutumia muda.

 

Katika maisha kuna namna mbili za kufanikiwa. Ya kwanza ni kujifunza kwa kukosea na ya pili ni kujifunza kutoka kwa waliotangulia. Njia ya kwanza ni ndefu mno, maana utalazimika kugundua kila kitu wewe mwenyewe na itakuchukua muda mrefu. Njia ya pili ni fupi na itakuchukua muda mfupi sana kufanikiwa.

 

Hata katika Biblia, mathalani, Mungu anasisitiza kwamba ni vema kuchukua muda na kuyatazama maisha ya waliotangulia ili kujipatia raha nafsini mwetu, yaani furaha na mafanikio ya maisha. Mwandishi katika kitabu hiki ameturahisishia mno, maana pamoja na uvumbuzi wake mwingi pia anatuletea hekima zilizounganishwa kutoka kwa rundo la waliofanikiwa katika maeneo mbalimbali.

 

Mimi nimeandika vitabu takribani 11 hadi sasa katika maeneo ya uchumi na familia. Kwa uzoefu wangu katika uandishi wa vitabu ninakiri kwamba kitabu hiki kina upekee mkubwa sana tena wa namna yake. Ndio maana kitabu hiki nathubutu kukiita kuwa ni hekima nyingi ndani ya kapu moja. Utakapokisoma mwanzo hadi mwisho utathibitisha hilo.

 

Mwandishi amefanya kazi nzuri mno kushughulika na vile mtu unavyoweza kuboresha hatma yako. Wale ambao huwa wanadhani mafanikio ni jambo la bahati nasibu, mwandishi anawanoa huo uvimbe wa fikra kwa msumeno wa maarifa ndani ya kitabu hiki.

 

Ndio maana nimependa sana alipoeleza habari ya kujiingiza katika orodha. Ohoo, kumbe mafanikio sio bahati nasibu bali ni suala la kuamua, kutendea kazi uliyoyaamua na kupata matokeo. Suala la kupata mafanikio ni uamuzi wako binafsi na mwandishi anasema hujachelewa kabisa!

 

Hiki ni kitabu ambacho ninapendekezwa kisomwe kuanzia kwa vijana wadogo mpaka wazee. Kwa namna kitabu hiki kilivyo, kina hekima kwa rika zote. Kwa kuwa kina maarifa yenye chembechembe za kutengeneza na kuibua vizazi ni kitabu ambacho kinafaa kusomwa na watu wa elimu zote.

 

Ingalikua amri yangu ningesema kitabu hiki kisomwe na kila mwanafunzi wa chuo kikuu, kisomwe na kila mfanyabiashara na mjasiriamali, kisomwe na kila mfanyakazi na kisomwe na kila mtu mahali popote alipo maadam anajua kusoma. Kuna mambo ndani ya kitabu hiki ambayo yakiingia na kupokelewa katika mioyo ya watu mahangaiko yatapungua sana kwa taifa na kwa mtu mmoja mmoja.

 

Hongera kwa kushika nakala ya kitabu hiki, naamini muda utakaoutumia kukisoma pamoja na fedha uliyotumia kukinunua ni uwekezaji wa thamani sana na utakaokulipa vizuri sana maishani mwako na katika vizazi vyako vingi vijavyo

 

Albert Nyaluke Sanga(SmartMind)

Mwandishi  & Mjasirimali

Mwandishi wa vitabu kama: Gia Kubwa, Umeiweka wapi Talanta yako? na Barua Ya Siri kwa wanandoa miongoni mwa vingi alivyoandika hadi sasa.

 

 Rafiki yangu. naamini sasa utakuwa umejifunza mengi kutoka kwenye Dibaji hii ya kipekee. Itakuwa vizuri uchukue sasa nakala yako ili uweze kuendelea kusoma. Na mimi rafiki yako nimekuandalia zawadi ya kupata nakala hii hapa bure kabisa.

Kitabu kinauzwa kwa elfu 20,000/- Wasiliana na mwandishi sasa kwa 0755848391 ili uweze kupata nakala yako.

 

 

, ,

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X