Washindi Huwa Wanafanya Hivi Baada Ya Changamoto


Mara nyingi unapoanza kufanya kitu mwanzoni matokeo mrejesho wake huwa ni mdogo sana. Kwa mfano unaweza kuanzisha biashara ukiwa na timu kubwa ya watu ambao wako nyuma yako na wanakuahidi kununua ila baada ya kuanzisha biashara ukawa huwaoni watu hao kwenye biashara.
Au pengine unaweza kuanzisha biashara ukitemgemea kupata mwitikio mkubwa wa wateja kuanzia siku ya kwanza, ila ukashangaa kuwa watu wenyewe huwaoni.
Kitu hiki huwa kinawakatisha tamaa watu walio wengi kiasi cha kuwafanya waache kile walichoanza. Ndio maana watu wengi wenye vipaji vya kuimba, kuigiza, kuchora, kuandika n.k. huwa wanajikuta wanakata tamaa kwa sababu tu ya mrejesho kuwa mdogo mwanzoni.
Kabla sijaendelea zaidi napenda kujua kama wewe rafiki yangu kitu kama hiki hapa kimewahi kukukuta?
Ukweli ni kwamba kitu kama hiki huwa kinamtokea karibia kila mtu. Japo sio wote huwa wanasema hiki kitu.  Najua umezoea kusikia hadithi tamu tamu za watu. yaani huwa unasikia kwamba mtu fulani alianzisha kitu fulani, baada ya siku chache kikafanikiwa. Ukweli ni kwamba ni watu wachache sana ambao huwa wanafanikisha vitu vyao kwa njia hii.
Na wewe pia unapaswa kujua kuwa kitu chako hakitafanikiwa siku ya kwanza kama unavyofikiri. Ila utahitaji kuendelea kuweka juhudi, kazi na kujituma bila kuacha. Endelea kuonesha kazi zako kwa watu zaidi. Endelea kutangaza biashara yako kwa watu zaidi. Endelea kuongea na wateja zaidi juu ya biashara yako.
Kuna watu ambao leo hii hawakujui wewe. Kama utakata tamaa leo hii ukaacha hawatakuja kukujua kabisa. ila kama utaendelea baada ya mwaka mmoja watu hawa watakujua na wataanza kuja kwako.
Kuna watu leo hii hawajui kwamba wewe una kipaji cha kuimba. Kama utaimba wimbo mmoja na kuacha ni wazi kwamba, watu hawa hawatakufahamu milele. Ila kama utaendelea kutoa kazi zaidi, kuzitangaza na kuwafikia watu zaidi basi watu hawa ni wazi kwamba watakujua tu.
Ngoja nikwambie kitu. Washindi huwa sio watu ambao wanaacha baada ya kuwa wamekutana na changamoto. Bali changamoto kwa washindi ndio huwa kichocheo chao kufanya zaidi na zaidi. Sasa sijui wewe upo kwenye taifa la washindi au waliokata tamaa?
Asili ya wasindi ni kusonga mbele baada hata baada ya kikwazo kikubwa
Uchaguzi ni wako.
Mimi nakutakia mwanzo mwema wa wiki hii. Ebu hakikisha kwamba wiki hii unaitumia vyema kabisa rafiki yangu. Kila la kheri.  

SOMA ZAIDI: NI MARUFUKU KUKATA TAMAA

Ni mimi anayejali mafanikio yako,
Godius Rweyongeza
0755848391

KUWA MIONGONI MWA WATU AMBAO WANAPOKEA MAKALA MAALUMU KWA WATU MAALUMU KWA KUBONYEZA HAPA

SUBSCRIBE KWENYE CHANNEL YANGU YA YOUTUBE HAPA


JIUNGE NAMI KWENYE NURU ANGAZA


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X