Kuamka Asubuhi Na Mapema Ni Tabia (Njia Sita Za Uhakika, Zilizothibitishwa Na Zisizoshindwa Zitakazokuwezesha Kujenga Tabia Ya Kuamka Asubuhi Na Mapema)


 

 

Benjamin Franklin ambaye anafahamika kama mwananchi wa kwanza Marekani alikwahi kuandika kwamba kulala mapema na kuamka asubuhi na mapema kunamfanya mtu awe na afya njema, tajiri na mwenye busara. Haya maneno aliyaandika zaidi ya miaka 200 iliyopita kwenye moja ya barua aliyokuwa anaandika kwa mwanae. Pengine Franklin angekuwa anarudi leo hii angeshangaa kwa jinsi maneno hayo machache yalivyopata umaarufu hasa kwenye ulimwengu maendeleo binafsi na hamasa. Maneno yake sasa yanatumika kama sehemu ya kuwahamasisha ili wajenge tabia ya kuamka mapema.

Leo hii ukiingia kwenye mtandao wa Google, na kuandika neno early to bed, early to rise utapata matoke zaidi ya laki mbili na elfu sabini. Hii ndio kusema kwamba huu usemi ni miongoni mwa semi zinazotumika sana.

 

Kipindi Benjamin Fraklin anasema hivyo hakukuwa na maendeleo makubwa kwenye teknolojia na sayansi kama ilivyo sasa hivi. Tafiti za kisayansi zimethibitisha kwa asilimia 100 kuwa maneno ya Benjamin Franklin ni ya ukweli na uhakika. Hivyo, kulala mapema na kuamka mapema kuna uwezo wa kukufanya uwe na afya njema, uwe tajiri na mwenye busara.

 

Pengine unaweza kujiuliza nawezaje kuwa na afya njema kwa kulala na kuamka mapema tu? Unaweza kuendelea kujiuliza pia kuwa nawezaje kuwa na utajiri kwa sababu ya kulala na kuamka mapema? Na mwisho unaweza kujiuliza nawezaje kuwa na busara kwa kulala na kuamka mapema?

Sasa hapo naomba uvute kiti chako ili nikuoneshe jinsi kulala mapema kulivyo na nguvu hizo zote na zaidi ya hapo.

 


JINSI KULALA MAPEMA NA KUAMKA ASUBUHI NA MAPENDA KUNAVYOWEZA KUKUFANYA UWE NA AFYA NJEMA

 

Imethibitishwa kuwa muda wa kulala kwa mwanadamu yeyote unapaswa kuwa kati ya saa sita mpaka nane. Suala la nani analala masaa sita au saba au nane linategemea na mtu mmoja mmoja. Kuna wale ambao mwili wao unawahitaji kulala saa saba, kuna wale ambao mwili wao unawaruhusu kulala saa nane. Mwili ukiunyima usingizi wa kutosha utakuwa unajichosha na itafikia hatua ambapo wewe mwenyewe utapoteza nguvu na uwezo wako wa kufanya kazi kwa weredi.

Nimewahi kusikia hadithi ya mzee mmoja aliyekuwa bahiri na hakutaka kupanga chumba cha kulala. Hivyo, akawa anajibana na kulala kwenye jiko la kazini kwake. Kadiri siku zilizyokuwa zinasogea mzee huyo akawa kama anaumwa. Ila hospitali walipokuwa wanapima ugonjwa wakawa hawaoni chochote. Ndipo watu walimshauri apange chumba na apate muda wa kutosha wa kulala. Alipopanga chumba ndani ya wiki moja ya kupata usingizi unaoeleweka, afya yake ikawa imerudi kwenye hali ya kawaida.

 

Kumbe usingizi ni muhimu sana kwa afya yako. Kitu kingine kuhusu kulala mapema ni kwamba, saa moja  unalola kabla ya saa sita usiku ni bora zaidi kuliko masaa matatu unayolala baada ya saa sita za usiku. Yaani,  mwili huwa una mpangilio wake wa kibaiolojia (biological rythm) ambapo katika masaa fulani kuna shughuli zainafanyika. Muda wa kuanzia saa nane mpaka saa 10 ni mida ambayo mwili unakuwa unajitengeneza, hivyo ni muda ambao mtu ananufaika kama ameshalala kwa muda na kuwa kwenye usingizi mzito. Hivyo, kulala mapema kunaufanya mwili kukamilisha zoezi hilo vizuri. Pia mtu anapowahi kulala anapata muda mzuri wa kuwa kwenye usingizi mzito (REM SLEEP) kuliko anayechelewa kulala. Usingizi mzito ndiyo wenye manufaa zaidi kwenye mwili

 

Kama huamini, toa siku moja ulale saa nne usiku na uamka saa kumi na moja ambayo hayo yatakuwa ni masaa nane kamili. Kisha toa siku nyingine ulale saa saba usiku na uamke saa moja asubuhi. Utagundua kwamba siku uliyolala saa saba usiku na kuamka saa moja asubuhi ni siku ambayo unaamka umechoka huku ukiwa hauna nguvu ila siku uliyoamka saa kumi na moja ni siku ambayo unaamka mwili ukiwa umetulia kwa asilimia zote. Hii ndio maana napenda kukwambia kwamba kulala mapema na kuamka mapena kunamfanya mtu awe mwenye afya njema.

 

 

JINSI KULALA MAPEMA NA KUAMKA MAPEMA KUNAVYOWEZA KUKUFANYA UWE TAJIRI

 

Kuna usemi kwamba ndege anayeamka asubuhi ndiye ambaye hupata chambo mzuri. Au kwa lugha yetu ya wahenga ni kwamba biashara ni asubuhi na jioni ndio hesabu huwa zinapigwa. Kwa hiyo mtu aliyeamka asubuhi na mapema kamwe huwezi kumlinganisha na mtu aliyechelewa kuamka.

Kuamka asubuhi na mapema kutawezesha wewe kuanza kufanya kitu ambacho watu wengine hawawezi kufanya. Na kwa kuwa asubuhi ndio akili inakuwa bado inachangamka basi kuamka asubuhi na mapema kunakufanya uweze kutekeleza majukumu yako kwa weredi wa hali ya juu sana. kitu kingine ni kwamba hata kama umeajiriwa, kuamka asubuhi na mapema kunakuwezesha wewe kufanya hata kijibishara chako na baadaye ndio unaenda kufanya biashara au kazi za watu wengine.

Hata kama umebanwa na ratiba kwa viwango vikubwa,  bado kuamka asubuhi na mapema kunaweza kuwa ndio chanzo cha wewe kupata muda wa kufanya kitu chako.

Ebu tuchukulie mfano kwamba umeajiriwa na una mradi wako wa kuku. Unaweza kuamka asubuhi na kuhudumia kuku wako kisha ukaenda kwenye ajira yako. Kitu hiki ni wazi kwamba kinaweza kukupa kipato cha ziada ambacho wafanyakazi wenzako hawapati na hivyo kukusogeza kwenye utajiri.

Na kama kila siku utapata saa moja la kufanya kitu cha tofauti ambacho watu wengine hawafanyi basi ni wazi ndani ya mwaka mmoja utakuwa umepiga hatua kubwa kulinganisha na wengine na hivyo  unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kutengeneza utajiri mkubwa.

Lakini pia kuamka asubuhi na mapema kunaweza kukupa mwanya wako kujifunza kuhusu fedha. Hii pia ni faida kubwa ukilinganisha na kwamba watu wengine huwa wanatafuta tu fedha ila hawaweki muda wao kwenye kujua jinsi fedha inavyofanya kazi. ndio maana nasisitiza kuwa kuamka mapema kunaweza kukufanya tajiri.

 

JINSI KUAMKA MAPEMA KUNAVYOWEZA KUKUFANYA MWENYE BUSARA

Moja kati kitu kinachoaminika sana miongoni mwa watu ni kuwa watu wenye busara ni wazee. Inaaminika hivi kwa sababu wazee wanakuwa wamepitia mambo mengi kuliko kijana au mtoto. Hivyo, muunganiko wa hivyo vitu vyote ndivyo vinawafanya wawe wenye busara. Hata hivyo, kwa upande wetu kuamka asubuhi na mapema tu kunawezaje kukufanya kuwa mwenye busara?

Inawezekanaje hii? Iko hivi. Ukiamka asubuhi kwanza ni wazi kuwa utapanglia siku yako kwa umakini. Hiki ni kitu ambacho watu wengi huwa hawafanyi. Na ukishapangilia siku yako itakavyokuwa utapata pia muda wa kujifunza kwa kusoma vitabu. Na katika vitabu kuna busara nyingi. Huhitaji wewe kuwa umefanya makosa au umepitia kwenye kila hali ili uwe na busara, ila tu kwa kusoma vitabu, unaweza kuwa mwenye busara kwa sababu unajifunza kutoka kwa watu wengi na kukusanya busara za watu wengi kwako.

Na hivyo ndvyo kuamka asubuhi na mapema kunaweza kukufanya mwenye busara.

 

Sasa labda mpaka hapo umeshaona kwamba unapaswa kujenga tabia ya kuamka asubuhi na mapema, lakini je, unajua unapaswa kuanzaje? Hapa chini ninaenda kukupa mbinu zitakazokuwezesha kuamka mapema kulivyo ulivyozoea.

 


MOJA, ANZA KWA KUEJGA TABIA YA KULALA MAPEMA

Kama ulikuwa umezoea kulala saa saba au saa sita basi kuanzia leo hii anza kujenga tabia ya kuamka mapema. Kwa kufanya hivi hata ukiamka asubuhi na mapema haitakuwa shida kwako.

 

PILI, AMKA DAKIKA MOJA KABLA

Kama sasa hivi ulikuwa unaamka saa 12 asubuhi unaweza kusema kesho utaamka saa kumi na moja dakika hamsini na tisa. Kesho kutwa ukaamka saa kumi na moja dakika hamsini na nane. Lengo lake likiwa kwamba usishtukize mwili kwa kuanza ratiba mpya ghafla. Badala yake mwili uuzoeshe taratibu. Utafanya hivyo mpaka utakapokuwa umefikia muda ambao ungependa kuwa unaamka kila siku.

Nashauri walau kila siku uamke mapema kiasi wkamba unaweza kupata saa moja na zaidi za ziada

 

TATU, WEKA ALAM

Hiki ni kitu kingine ambacho unaweza kufanya kikakuwezesha kuamka asubuhi na mapema. Siku hizi karibia kila simu ina uwezo wa kutuma alarm. Hivyo, unaweza kutumia hii nafas kuwa unaweza alarm kwenye simu yako ambayo itakusaidia wewe kuamka asubuh na mapema bila kuchelewa. na ubora wa alarm ni kwamba haupaswi kuweka pembeni mwa kitanda chako. Unapaswa kuiweka mbali na pale ulipolala. Kwa kufanya hivyo, ikiita asubuhi usiwe na uwezo wa kuizima na wewe kuendelea kulala, badala yake ule usumbufu wake ukufanye uamke kitandani. kitu kingine ni kwamba hapa katikati yako na alarm ilipo unaweza kuweka vitu vya kukuzonga kiasi kwamba mpaka unaifikia alarm usingizi unakuwa umepotea na hivyo kukuwezesha wewe kuendelea na mambo mengine.

 

NNE, UKIAMKA KAOGE MAJI YA BARIDI

Kuoga asubuhi na mapema kunaweza kukusaidia sana wewe kujenga tabia ya kuamka itakayodumu. Ukiamka asubuhi na mapema chukua maji ya baridi na nenda kuoga. Hii kwanza itaustua mwili na kuuambia mwili kuwa sasa sio tena muda wa kulala badala yake umefika muda wa kazi. lakni pia inakuwa ni sehemu ya kuuanda mwili kwa ajili ya kashikashi ambazo unaenda kukutana nazo ndani ya siku,

TANO, KUWA NA NDOTO AU SABABU ITAKAYOKUFANYA KILA SIKU UAMKE MAPEMA

Bila shaka imewahi kukutokea walau hata mara moja, siku ambayo ulikuwa na safari iliyokupasa kuamka asubuhi na mapema. Ni wazi kuwa siku hiyo uliweza kuamka mapema bila hata ya kuhitaji kuamshwa. Unajua kwa nini? Moja ya sababu kubwa ni kwamba ulikuwa na kitu kinachokusukuma. Siku hiyo ulikuwa unajua kwamba una safari na huwezi kutulia kwa kitu chochote kidogo isipokuwa safari hiyo tu. Sasa kitu kama hicho kinaweza kukusaidia pia kwenye kuamka mapema kila siku. Kwa mfano, ndoto yako inaweza kuwa ndio msukumo wa wewe kuamka mapema kwa sababu huwezi kutulia kwa kitu kingine kidogo isipokuwa ndoto yako tu. Je, wewe ndoto yako ni ipi?

 

SITA, UKIAMKA ASUBUHI KUNYWA MAJI

 

Sayansi inasema kwamba unapolala usiku unapoteza maji mengi. Yapo yanayopotea kwa njia jasho na mifumo mingine inayoendelea kwenye mwili. hivyo, kunywa maji asubuhi ni njia mojawapo ya wewe kuongeza maji mwilini yaliyopotea ukiwa umelala. Hivyo, kuanzia leo hii ukiamka asubuhi chukua glasi moja ya maji unywe. Ni sehemu pia ya kuuweka mwili sawa kwa ajili ya kuianza siku yako. Unaweza kuandaa maji yako usiku mmoja kabla na kuyaweka sehemu ili unapoamka asubuhi usianze kuhangaika na kuyatafuta yako usiku mmoja kabla na kuyaweka sehemu inayooneka au mezani kwako, ukiamka asubuhi unakunywa maji na kuendelea na mambo mengine. Hapa kwenye maji wewe chagua aina ya maji ambayo utaona yanakufaa. Wapo wanaosema kwamba maji ya uvuguvugu ni bora zaidi wakati wengine wakisema kwamba maji ya baridi ndio bora zaidi. na wengine wanasema maji yaliyochanganywa na limau. Wewe chagua maji unayoona yanakufaa na yatumie hayo.

 

 

Rafiki yangu ni imani yangu kuwa leo hii umejifunza mengi sana kuhusu kuamka asubuhi na mapema. Sasa kilichobaki ni wewe kuweka kwenye matendo haya ambayo umejifunza hapa. nakutakia kila la kheri.

 

Umekuwa nami rafiki yako wa ukweli Godius Rweyongeza

Hakikisha Umesubscribe kwenye Channel yangu ya youtube kwa KUBONYEZA HAPA

Jiunge na mfumo wa kupokea makala maalumu kwa njia ya barua pepe kwa KUBONYEZA HAPA

Jipatie nakala za vitabu vyangu vya kiswahili kwa KUBONYEZA HAPA

Kama ungependa kujifunza kuhusu uandishi kutoka kwangu wasiliana nami kwa 0755848391

 

Kutengenezewa blogu yako kitalaamu tuwasiliane kwa 0755848391

kila la kheri

 


4 responses to “Kuamka Asubuhi Na Mapema Ni Tabia (Njia Sita Za Uhakika, Zilizothibitishwa Na Zisizoshindwa Zitakazokuwezesha Kujenga Tabia Ya Kuamka Asubuhi Na Mapema)”

  1. Asante Sana Kaka Godius kwa Article nzuri Hii,,,Nimejifunza kitu kikubwa Sana,,🙏🙏✌️🤭

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X