Njia Ya Uhakika Ya Kutoboa Kwenye Biashara


Rafiki yangu, siku ya leo ningependa kukwambia njia ya uhakika ya wewe kutoboa kwenye biashara yako, unajua njia hii ni ipi?

Ngoja kwanza nikwambie kitu. Tafiti nyingi kwenye biashara zimeonesha kwamba asilimia 90 ya biashara ambazo huwa zinaanzishwa kila mwaka, huwa zinakufa. hii ndio kusema kwamba kati ya biashara 100 ambazo huwa zinaanzishwa kila mwaka ni biashara kumi tu ambazo huwa zinauvuka mwaka wa kwanza.
Na kati ya hizo biashara kumi ambazo huwa zinauvuka mwaka wa kwanza, bado ni biashara chache sana ambazo huwa zinaweza kuvuka mpaka kufikia miaka mitano.

Hili wewe mwenyewe unaweza kulishuhudia kwenye maneneo yako unayoishi. Ni wazi kuwa kuna watu wengi ambao huwa wanajitahidi kila mwaka kuhakikisha kwabna wanaanzisha biashara mpya, ila ni wachache sana ambao huwa wanaweza kuendeleza biashara hizo kabla hawajafunga.

Unadhani shida hapa ni nini?
Kuna vitu kadha wa kadha ambavyo watu wanaoanzisha bishara kila mwaka wanakosa. Ukiwa na hivi vitu, ni wazi kuwa utaweza kufanya makubwa, naam, utaweza kufanya makubwa sana.

Kwanza unapaswa kufanya biashara ambayo unapenda. Haupaswi kufanya biashara au kitu ambacho hupendi. Kwa sababu unaenda kuwa unaamka kila siku kwenye hii biashara maisha yako au kwa miaka mingi ijayo. Sasa haifai hata kidogo kwako kufanya biashara ambayo wewe mwenyewe hupendi, au hujisikii kufanya.

sasa kosa kubwa ambalo watu huwa wanafanya ni kufanya biashara kwa mkumbo. Kisa eti kasikia watu wanasema kwamba biashara fulani inalipa, basi na yeye anakimbilia kwenye kufanya biashara hiyo. Rafiki yangu, naomba unielewe kitu kimoja na cha uhakika. Fanya biashara unayopenda, tena biashara unayopenda kutoka moyoni, ila siyo biashara ambayo umesikia watu wanasema kwamba inalipa.
Hii siyo ngoma ya kuingia ili ubahatishe tu. Unapaswa kuchagua kitu ambacho kuwa tayari kukifanya kwa muda mrefu

Pili, unapaswa kufanya kwa muda mrefu. Siyo unaingia leo hii kwenye biashara halafu kesho unategemea kuwa umetoboa na kupata mafanikio makubwa. Kitu kama hiki hakipo rafiki yangu. inahitaji muda. ndio maana hata serikali huwa zinapewa muda. Unakuta kwamba muda wa uongozi wa serikali tangu wanapoingia madarakani mpaka uchaguzi mwingine unapofanyika ni miaka mitano. Hiki ni kipindi ambacho inatarajiwa kama jambo au mambo fulani yatafanyiwa kazi kwa mwendelezo kila siku na bila kuacha yatakuwa yameweza kuonesha matokeo.
Lakini siyo suala la kulala leo na kuamka kesho.

Sasa nikuulize wewe kitu chako umeshakifanya mfululizo, tena kila siku kwa miaka mitano mfululizo. Kama bado hujakifanya kwa miaka mitano ujue wazi kuwa bado unahitaji kuweka nguvu na juhudi kubwa kwenye kukifanya hiki kitu.

Tatu, unapaswa kujituma kwenye kazi na kuwa tayari kufanya kazi kwa viwango vya juu kuliko watu wengine. Hiki ni kitu muhimu sana rafiki yangu, na hakikisha kwamba unakifuatilia kwa umakini mkubwa sana na bila ya kuchoka.

Nne, jali afya yako. kwa kuwa hii ngoma siyo ya muda mfupi, basi hakikisha kwamba unajali afya yako. Yaani, hakikisha kwamba afya yako imekuwa ni kipaumbele chako nambari moja. Mara zote na siku zote, ipambanie afya yako. Hakikisha kwamba afya yako ndiyo kipaumbele chako nambari moja kila siku. Kula vizuri, pata muda wa kulala pia na fuata taratibu zote za kitalaamu kwenye afya. Hili jambo litakufanya uwe na afya njema, mara zote uwe kwenye mapambano.

Makala hii imeandikwa na Godius Rweyongeza.

Baadhi ya makala za Godius Rweyongeza zimechapwa kwenye magazeti makubwa nchini Tanzania likiwemo gazeti la MWANANCHI.

Kupata vitabu vya Godius Rweyongeza unaweza kwa kuwasiliana na 0755848391/ +255755848391 kwa simu au whatsap.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X