Nguvu ya fedha; Itumie Ikubebe


Hivi umewahi kujiuliza fedha kama fedha ina nguvu gani maishani mwangu, kwenye maisha ya familia yangu au hata maisha ya watu wengine wa karibu sana kwenye andiko la leo ambapo unaenda kujifunza nguvu hizi muhimu za fedha na jinsi ambavyo unaweza kutumia nguvu hizi hapa kwa manufaa yako.

1. Nguvu ya kufanya maamuzi. Kwenye hili andiko ninaenda kuandika mengi kuhusiana na nguvu ya pesa. ila kitu kimoja ambacho pesa itakupa kama utakuwa nacho ni nguvu ya kufanya maamuzi, yaani, ukiwa na pesa yako, utakuwa na uwezo wa kuamua chochote kile unachotaka. Unaweza kuamua utembelee eneo gani na eneo gani usitembelee. Hata kwenye vikao vya familia, ukiwa na pesa, nguvu ya wewe kufanya maamuzi inakuwa kubwa ukilinganisha na yule ambaye anakuwa hana pesa. SIyo tu kwenye familia, hata kwenye ngazi za maamuzi ya kitaifa, mpaka kimataifa. Leo hii Marekani linafahamika kama taifa lenye nguvu, kwa sababu wanatumia nguvu ya pesa kufanya maamuzi ambayo kama huna pesa hawezi kuyafanya.

Chukulia mfano, wa kawaida tu. kuna nchi za Afrika zinawekewa vikwazo kwa sababu ya kuwa na uhusiano na nchi ya urusi au washirika wake, ila wakati huohuo, nchi ya Marekani ambayo inaziwekea nchi za afrika hivyo vikwazo, yenyewe ina uhusiano wa karibu sana na washirika wa Urusi, na haiwekewi vikwazo.

Aah, halafu umewahi kusikia wapi maishani kwako kwamba nchi maskini imeiwekea nchi tajiri vikwazo. Hiyo ndiyo nguvu ya pesa aiseee. Yaani, ukiwa na pesa, ni kama vikwazo vinakuwa hamna. Ndio maana unapaswa kuwa nayo, pesa ni sabuni. Hahaha, sabuni ya roho. Kuwa nayo aisee!

2. nguvu ya kununua. Ukiwa na fedha unakuwa na nguvu ya manunuzi. Kwa pesa yako unaweza kuamua kununua jambo fulani au la unaweza kuacha. Unaweza kuamua kununua sasa hivi, au la unaweza kuamua kununua baadaye.

Unaweza kuamua kuringa kidogo kabla ya kutoa hela. Hata hivyo, hela si ya kwako tu. Hii ni nguvu ya fedha. Ndio maana wewe unahitaji kuhakikisha kwamba unakuwa na pesa.

Hata ukiomba mtu akupunguzie bei, siyo kwamba unakuwa upungiziwe bei kwa sababu ya mtu akuonee huruma, bali kwa sababu una pesa.

3. nguvu ya kuwekeza. Fedha unaweza kuitumia kuwekeza kwenye eneo lolote. Kuwekeza ni kuifanya fedha ikutumikie, yaani, unaifanya pesa ikuingizie pesa zaidi hata pale unapokuwa umelala. Hicho ni kitu ambacho unahitaji ukifanyie kazi rafiki yangu.

Kama hujaanza kuwekeza, mwaka huu kuwekeza kunapaswa kuwa kwenye vipaumbele vyako.

Na kwa kuanzia hakikisha kwamba unasoma kitabu changu cha MAAJABU YA KUWEKEZA KWENYE HISA, HATIFUNGANI NA VIPANDE

Hakikisha una pesa, na hakikisha kwamba unaitumia pesa yako kuwekeza.

4. nguvu ya kutoa na kusaidia jamii. Rafiki yangu, huwezi kusaidia watu kama hauna pesa. Huwezi kusaidia watu kama wewe mwenyewe unahitaji msaada. hahah, unahitaji uwe na pesa ili uweze kusaidia watu. Ni rahisi tu hivyo. Fedha ndiyo inakupa nguvu ya kusaidia watu. Kama unayo unaweza kuwasaidia watu, kama hauna, daah, ni ngumu kuasaidi watu.

5. nguvu ya nguvu ya kununua muda kwa ajili yako. Pesa inaweza kukusaidia wewe kununua muda. Unajiuliza pesa inanunuaje muda, ningependa kukwambia kwamba pesa inanunua muda pale ambapo unakuwa umeajiri watu wengine wakusaidie kufanya baadhi ya majukumu, na hivyo kukupa mwanya wewe wa kuendelea na majukumu mengine. Upo hapo rafiki yangu.

6. Nguvu ya kutibiwa. Kuna watu wengi huwa wanakufa kwa sababu tu ya kukosa huduma bora za kimatibabu, na wanakosa huduma bora kwa sababu hawana nguvu ya pesa. Ukiwa na nguvu ya pesa, kwanza ukijisikia vibaya tu utawahi hospitali, unakuwa hauna cha kuanza kusikilizia sijui kuona kama muujiza utatendeka ukapona. Ila kama hauna nguvu ya pesa, utaanza ooh, eti unasikilizia kuona kama utapona. Oooh, sijui imeenda endaje. Tafuta fedha ikuzoee aisee.

7. nguvu ya kujenga mahusiano. Tafiti nyingi zimefanyika, na imegundulika kwamba moja ya kitu ambacho huwa kinafanya watu waachane kwenye mahusiano, ni kwa sababu ya pesa. hivyo, unahitaji uwe na pesa ili uweze kufanya makubwa zaidi. na siyo tu uwe na pesa, bali uwe na elimu sahihi kuhusiana na pesa.

8. Nguvu ya kuchagua aina ya maisha unayotaka. Pesa inakupa nafasi yaw ewe kuchagua aina ya maisha ambayo wewe mwenyewe unataka, usupokuwa na fedha unaweza kuwa mtumwa kwa kulazimika muda mwingine kufanya kazi ambazo hata wewe mwenyewe hupendi.

11. nguvu ya kubadili mwonekano wako

Kuna siku moja kwenye mtandao watu waliweka picha ya msanii Zuhura, maarufu kama Zuchu, akiwa bado na maisha ya kawaida. Aliyeweka ile picha akawa amesema kwamba huyu ndiye Zuchu kabla hajatoka kimaisha.

Lakini sasa hivi nguvu ya pesa imembadilisha.

Pesa rafiki yangu ina uwezo wa kubadili mwonekano wako. Ukiwa nayo, mwonekano wako tu, unaongea.

12. nguvu ya kukufanya ujiamini. Pesa ina uwezo wa kukufanya ujiamini.Yaani, inakufanya ujiamini kuliko yule ambaye hana. Yaani, ukitoka nyumbani ukiwa unajua kwamba hakuna chakula, unadaiwa kodi, na makorokoro mengine kibao, hata kujiamini kwako kunapungua tu. Ila kama unajua una mzigo wa kutosha nyuma ya pazia, hapo unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kujiamini kuliko mtu mwingine yeyote. Hiyo ndiyo nguvu ya pesa.

Rafiki yangum, fedha unapaswa kuwa nayo. Unapaswa kuwa nayo, maana kuwa nayo tu, kutavutia vitu vingi kwenye maisha yako. Hivyo itafute. Lakini usiishie tu kutafuta fedha, bali pia kuwa na maarifa sahihi ya kifedha. Haya yatakusaidia wewe kufanya makubwa zaidi wkenye maisha yako. Kila la kheri

Makala hii imeandikwa na Godius Rweyongeza.

Baadhi ya makala za Godius Rweyongeza zimechapwa kwenye magazeti makubwa nchini Tanzania likiwemo gazeti la MWANANCHI.

Kupata vitabu vya Godius Rweyongeza unaweza kwa kuwasiliana na 0755848391/ +255755848391 kwa simu au whatsap.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X