Uchambuzi wa Kitabu: The Leader Who Had no Title (Kiongozi Asiye na Cheo); Mambo 200 Niliyojifunza katika kitabu hiki.


Mchambuzi: Hillary Mrosso
Mawasiliano: 255 683 862 481

Utangulizi
Dhana ya uongozi imekuwa na maana nyingi, na watu wengi hawajui maana halisi ya uongozi, wengi wameshindwa kufanya makubwa, wengi wameshindwa kufanya maamuzi muhimu kwenye maisha yao kwasababu wanajiona hawapo kwenye nafasi ya kufanya hivyo. Mwandishi wa kitabu hiki, Robin Sharma anaweka wazi maana halisi ya uongozi, amefafanusha kwa kina umuhimu na nguvu ya uiongozi katika maisha ya kila binadamu, pia ameeleza dhima kuu ya ujumbe wake uliobeba kitabu hiki kuwa ili ufanikiwe na kufanya mambo makubwa huitaji cheo wala nafasi za uongozi, unahitaji tu kujitambua na kutumia nguvu ya uongozi iliyolala ndani yako ili ikusaidie kuwa kiongozi kwako mwenyewe na kwa jamii nzima. Karibu katika uchambuzi wa kitabu hiki tujifunza mambo 200 niliyoyaona katika kitabu hiki.

 1. Kila mmoja wetu amezaliwa na uwezo mkubwa wa kipekee sana, lakini wengi wanakufa wakiwa hawajautumia ukuu na upekee waliozaliwa nao.
 2. Watu wengi wanadhani wameshafanya kila walichotakiwa kufanya, wameshatumia kila uwezo, na vipaji walivyo navyo, ukweli ni kwamba kama bado unaishi bado kuna mengi makubwa unaweza kuyafanya zaida hayo uliyoyafanya.
 3. Usiruhusu ukaja kuwa na majuto kwenye maisha yako ya baadaye kwa kushindwa kufanya vitu muhmu ulivyotakiwa kuvifanya wakati huu. Mara nyingi ni rahisi sana kuchukulia mambo poa, kupuuzia vitu kwa kuwa vipo na vinaonekana kila wakati.
 4. Kama wazazi wako wote wapo, fanya kila unachoweza na kilichopo kwenye uwezo wako wote kuwafanyia mema, kuwaheshimu, kuwatembelea, kuwajali, usipofanya hivyo utakuwa mtu wa majuto wazazi wako watakapoondoka hapa duniani.
 5. Usomaji na kujifunza kupitia vitabu unakufanya kuwa mtu bora na inafungua milango mingi hata ile ambayo ulidhani haipo, inakufungulia dunia ya fursa, furaha, amani na kujiamini, kamwe usiache kujifunza kupitia usomaji wa vitabu.
 6. Mwandishi wa kitabu Robin Sharma anasema, watu bora ni wale wenye maktaba kubwa. Maana yake wanajielimisha kila wakati, wananunua vitabu na kuvisoma na kupata maarifa bora ambayo yanawafanya wawe watu bora.
 7. Huitaji cheo chochote ili ufanye makubwa kwenye maisha yako. Mwandishi wa kitabu hiki anasema ili ufanye makubwa kwenye maisha yako unahitaji tu kuwa binadamu anayepumua.
 8. Usisubiri uwe na cheo ndio uanze kufanya makubwa kwenye maisha yako, huitaji kuwa meneja, mkurugenzi, mbunge, diwani, au afisa fulani ili ufanye makubwa.
 9. Kama kuna ujumbe mkubwa kwenye kitabu hiki basi ndio huu; huitaji kuwa na cheo chochote kuwa kiongozi bora, huitaji cheo ili uwe na mafanikio.
 10. Mwandishi Robin ansema, kamwe usitetereshwe, au kuyumbishwa na mambo ya vyeo, maana vyeo ni mambo ya muda tu, huja na kuondoka, lakini unatakiwa kuwa kiongozi asiye na cheo.
 11. Mwandishi anasema, wakati mwingine kupotea njia ndio njia sahihi ya kuifahamu njia sahihi. Kuna nyakati zinapita kwenye maisha yetu na tunajiona tupemepotea na hutana tena msimamo, lakini huu ndio wakati sahihi wa kujua kwa usahihi tuhachotakiwa kufanya.
 12. Kuna wakati maisha yanatakiwa yakuangushe, yakuumize na kukukandamiza chini, ili uinuke na kujijenga na kujiimara kuwa mtu bora na imara.
 13. Chagua kwenye maisha yako kuwa hutayaendesha maisha yako kwa kufuata vibandiko au lebel kama vile umri, vyeo au nafasi za uongozi. Ishi maisha yako bila kujiwekea mipaka au ukomo wowote.
 14. Njia nzuri ya kufanya kampuni au shirika lolote kuwa na ufanisi mkubwa ni kuwajengea uwezo wa kiuongozi wafanyakazi wote, na kuwafundisha falsafa ya kuongoza bila cheo au wanaweza kufanya makubwa bila kuwa na cheo cha uongozi.
 15. Ili uwe kiongozi sio lazima uwe na cheo, uongozi wa kweli unahusiana kidogo sana na cheo, uongozi wa kweli ni uongozi usiozingatia vyeo ili kufanya mambo.
 16. Huitaji kuwa na cheo cha uongozi ndio ufanye maamuzi muhimu kwenye maisha yako. unaweza kufanya maamuzi bora na yenye maana kwenye maisha yako bila kuwa na cheo chochote.
 17. Namna tunavyoelewa na kufikiri kuhusu dhana ya uongozi ni muhimu sana, maana uongozi ndio huamua mafanikio ya mtu binafsi na ya kampuni au shirika.
 18. Kila mmoja wetu anatakiwa kuwajibika katika kutoa matokeo bora sana, na endepo kila mmoja atafanya kilicho bora, kila kitu kitakachofanywa kitakuwa bora sana na shirika litakuwa na huduma bora.
 19. Kila mtu ndani ya timu anatakiwa kufanya na kuamua kama mkurugenzi wa shirika, kila mtu ajione ana wajibu wote wa kufanya makubwa na kufanya maamuzi muhimu kwenye maisha yake na maisha ya shirika au kampuni bila kutegemea vyeo kufanya hivyo.
 20. Mahali popote ulipo ndio mahali sahihi pa kuonyesha uongozi wa kweli, ni sehemu ya wewe kuchanua na kutumia vipawa vyako kufanya makubwa. Na huitaji cheo cha uongozi kufanya hayo.
 21. Kila mtu anatakiwa kutengeneza ushawishi kwa chochote kila anachokifanya, kazi zako unazozifanya zinatakiwa kuwa kazi bora sana, ili ziweze kufanya maisha ya wengine kuwa bora kabisa.
 22. Kati ya uwezo mkubwa tulionao kama binadamu ni namna tunavyoweza kuchagua kuchukuliana na hali zozote za mazingira ambayo tunajikuta tupo ndani yake.
 23. Uongozi hauhusiani na mahali ulipo, au yale unayoyapata, uongozi ni zaidi sana namna unapofanya maamuzi muhimu kwenye maisha yako.
 24. Uongozi ni huduma bora unazotoa kwa ajili ya kuinua na kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi, maisha ya wote wanaokuzunguka yanatakiwa kuwa bora kwasababu ya huduma na maisha unayoishi kama kiongozi.
 25. Kwa jinsi usivyojali kupata na kupokea mambo mengi ambayo wengi wanayataka wakiwa kazini, ndivyo unavyotengeneza nafasi kubwa ya kuyapokea mambo hayo.
 26. Wengi wanaingia kazini wakiwa na mitazamo kwamba endapo watapata nafasi ya uongozi au cheo ndio wataanza kufanya makubwa, wataanza kutoa huduma bora, na ndio watajisukuma zaida kufanya kazi kubwa ili kuleta matokeo makubwa.
 27. Mwandishi wa kitabu hiki anasema, namna nzuri ya kudhihirisha ubora wako wote sio lazima upewe cheo, au upewe fedha, au mali au zawadi, fanya makubwa bila cheo chochote, fanya makubwa bila kusubiria cheo.
 28. Mambo mengi kwenye maisha yetu tunayapata kwa kulipa gharama kwanza. Ni mghahawani tu ndio utapewa huduma ndio ulipie baadaye.
 29. Usijali kuhusu kupata zawadi au mambo mazuri kwenye maisha yako, kama unafanya mema, kama unajisukuma, kama unajitoa kufanya yaliyo bora usijali kuhusu matokeo maana yatakuja tu.
 30. Mwandishi anasema, hakuna jambo jema utakalolifanya litaenda bure, hivyo wekeza kwenye kufanya kazi, wekeza na chukua hatua za kufanyia kazi ndoto zako kila siku maana matokeo yake yatakuja tu.
 31. Tukijifunza kwa watu waliofanikiwa na kufanya makubwa hapa duniani kama vile Roosevelt, Mandela, Thomas Edson au Albert Einstein hawakufanya makubwa kwasababu ya fedha, au mali, walifanya makubwa kwasababu ya kiu ya kuleta mabadiliko na kuona maisha ya binadamu yanakuwa bora hapa duniani.
 32. Hapa haimaanishi kuwa fedha haina umuhimu kwenye maisha, pesa ina umuhimu sana kwenye maisha yetu, pesa itakupa uhuru, pesa itakupunguzia msongo wa mawazo, pesa itakufanya utoe huduma bora kwa unaowapenda, pesa itakufanya pia uwe na vitu vizuri na muhimu.
 33. Kuna msemo maarufu unasema, njia nzuri ya kuwasaidia masikini ni kutokuwa mmoja wao. Pesa itakufanya uwasaidie masikini.
 34. Siku zote za maisha yako kumbuka, huitaji cheo ili kuwa kiongozi, huitaji cheo au nafasi ya uongozi ili uonyeshe kuwa wewe ni kiongozi.
 35. Uongozi sio kwa ajili ya wakurugenzi, maafisa wa jeshi, au watu wanaoongoza mataifa, uongozi ni kwa ajili ya kila mtu.
 36. Kitu pekee unachotakiwa kuwa nacho ili uweze kukidhi vigezo vya kuwa kiongozi ni pumzi, unahitaji tu kuwa binadamu anayepumua.
 37. Tunatakiwa kukumbushwa zaida kuliko kutoa maelekezo, kwa asili binadamu hawapendi maelekezo, hawapendi amri, hivyo njia nzuri ya kufikisha ujumbe muhmu kwa mtu mwingine ni kuutoa kwa namna ya kumkumbusha.
 38. Uongozi sio kitu kigumu na maalumu sana ambacho kinapatikana kwa watu wachache waliotunukiwa shahada katika vyuo vikuu bora duniani kama Harvard.
 39. Katika ulimwengu tulionao sasa umejaa mambo mengi na kuendeshwa kwa mihemuko na hisia nyingi, kitu pekee kinachoweza kutufanya kufanya maamuzi sahihi na kuchukua hatua sahihi ni kuwa na uongozi makini na shahihi.
 40. Kila eneo la maisha yetu ili liwe bora, tunahitaji kusimika roho ya uongozi. Bila uongozi hakuna mipango, hakuna, malengo, hakuna mafanikio; uongozi ndio kila kitu.
 41. Ili tufikie kilele cha juu sana cha mafanikio kwenye maisha yatu, tunatakiwa kuonyesha uongozi kwenye afya zetu, kwenye mahusiano yetu, kwenye masuala yetu ya kifedha, na kwenye jamii yetu.
 42. Mwandish Robin Sharma amesisitiza sana kuwa, uongozi anaomaanisha hapa ni uongozi binafsi. Kwasababu usipoweza kujiongoza mwenyewe kamwe hutaweza kumuongoza mwingine.
 43. Jiongoze wewe mwenyewe kwanza kwa mafanikio makubwa, ndio utaweza kuongoza wengine kwa mafanikio makubwa.
 44. Tafuta kwanza nguvu zilizo ndani yako zikusaidie kabla hujaenda kutafuta nguvu za watu wengine kukusaidia. Jiangalie ndani yako, kama kuna kitu unachoweza kukitumia ili kikusaidie kuwa mtu bora basi fanya hivyo kwa nguvu zako zote.
 45. Mwandishi anasema wanaoishi kwa falsafa hii ya uongozi bila kuwa na cheo wana tabia ya kuamka mapema zaidi ya wengine wanapoenda kuianza siku yao.
 46. Benjamin Franlin, moja ya watu mashuhuri kuwa kuisha hapa duniani aliwahi kusema, kutakuwa na muda mwingi wa kulala baada ya kufa, hivyo usione kama unakosea unapojiongezea muda wa kufanya makubwa kwenye maisha yako wakati ukiwa hai.
 47. Jifunze kuamka mapema zaidi, ili upate muda mwingi wa utulivu kufanyia kazi ndoto na maono yako yanayokukosesha usingizi. Ukiweza soma kitabu cha 5 AM CLUB, ni kitabu bora sana kinachoeleza kwa kina tabia ya kuamka mapema umuhimu wa kuamka mapema na kuanza kuziishi ndoto zako, tafuta nakala yako uisome.
 48. Ndugu msomaji wa uchambuzi wa kitabu hiki tambua kuwa ni rahisi sana kulala sana, ni rahisi sana kutumia masaa mengi kitandani, mwandishi anasema tunapoteza muda wa thamani sana kwa kulala sana, amka mapema upambanie ndoto zako.
 49. Oneza muda wa kufanyia kazi ndoto zako kwa kujizoeza kuamka mapema kila siku, utaongeza masaa mengi kwa wiki kwa mwaka. Jilazimishe uamke mapema kabla ya dunia haijaamka ili ufanye makubwa.
 50. Ukiamka mapema zaidi kila siku, labda saa moja kabla ya muda wa zaida, kwa mwezi utakuwa una masaaa 30, sawa na wiki nzima, ambayo ni mengi sana na unaweza kuyatumia kufanyia kazi ndoto zako.
 51. Kama kiongozi unatakiwa kuboresha kila kitu kwenye maisha yako, kuwa na shauku na njaa kali ya kuboresha kila eneo la maisha yako, fanya hivyo kila siku.
 52. Wakati mwandishi anajaribu kuelezea umuhimu wa muda na Matumizi ya vipawa vyetu, ametumia muda mwingi kuelezea dhana ya kiongozi asiye na cheo maeneo ya makaburini ili kutukumbusha muda wetu wa kukaa hapa duniani ni mchache sana na pia tunatakiwa kutumia vipawa vyetu na uwezo tuliopewa kuboresha maisha ya dunia na sio kwenda navyo kaburini.
 53. Makaburi yanatukumbusha kuwa ndio sehemu ambayo tutakuja kuishia baada ya kuishi hapa duniani, hivyo, vitu vyote tulivyodhani ni muhimu maishani kama vile vyeo, fedha, nafasi kwenye jamii havitakuwa na maana tena.
 54. Kitakachokuwa na maana wakati huo ni endapo uliishi kama kiongozi bila kujali vyeo, utakufa kwa amani endapo utajua ulitumia vipawa vya uongozi vilivyo ndani yako ili uboreshe maisha yako na maisha ya wanaokuzunguka.
 55. Wakati mwingine inafaa kufikiria kuhusu kifo na siku zako za mwisho, maana zitakufanya ujitafakari na kuamsha moto wa kufanyia kazi maono na ndoto zilizopo ndani yako.
 56. Mwandishi wa kitabu hiki amefafanua baadhi ya mambo yanayoleta majuto siku zako za mwisho hapa duniani, (The 10 Human Regrets).
 57. Utafikia siku zako za mwisho ndipo utajuta kuwa ulipata nafasi na fursa nyingi nzuri za kuboresha maisha yako na kutumia vipawa vyako.
 58. Utakuja kujuta sana endapo utafika mwisho wa maisha yako, na kukumbuka hakuna hata mtu mmoja uliyemvutia na kumfanya bora kwa mtindo wa maisha uliyoishi.
 59. Utafikia siku zako za mwisho hapa duniani ukiwa na uchungu mwingi na majuto kwasababu ulishindwa kuchukua hatari zilizokuja kwako na hivyo hakuna makubwa uliyofanya na maisha yako hapa duniani.
 60. Utajutia sana utakapofika katika siku zako za mwisho hapa duniani, kwasababu ulishindwa kuishi kwa ujasiri, na hukuwa mfano bora kwa wengine.
 61. Kila mtu anatengeneza maisha anayoishi, hivyo amua kutengeneza maisha yako yawe jinsi unavyotaka kulingana na maono na ndoto zako.
 62. Jehanamu kubwa iliyopo hapa duniani ni kwa watu ambao wanakufa bila kuonyesha na kutoa ukuu na vipawa walivyozaliwa navyo. Wanapeleka utajiri na ukuu wao kaburini badala ya kuutumia wote kuibariki dunia na kuifanya kuwa sehemu bora sana ya kuishi.
 63. Siku zote mafanikio yanakuja kwa kuwa na nidhamu kubwa ya kufanya na kuchukua hatua ndogo ndogo kila siku bila kuacha. Tabia ndogo ndogo za kuleta mafanikio ni rahisi sana kuzifanya kila siku, ndio maana watu wengi wanafikiri haziwezi kuleta mafanikio kwa haraka, hivyo wanaachana nazo hawazifanyi.
 64. Mwandishi anasema, mafanikio yanahusisha vitabia vidogo vidogo tunavyoweza kuviishi kila siku bila kuacha. Ukiwa na tabia sahihi na ukaziishi kila siku bila kuacha, vinaleta matokeo makubwa sana baadaye, usipuuzie tabia njema kwenye maisha yako.
 65. Mwandishi ametolea mfano wa mkulima ambaye huotesha mbegu zake kila wakati, huandaa shamba lake kila wakati, hupalilia shamba lake kila wakati humwagilia maji shamba lake, na hatimaye wakati wa mavuno hufika na huvuna alichopanda, ndivyo inavyotakiwa kuwa kwenye tabia zetu za mafanikio.
 66. Kuna wakati unaweza juhudi sana, kuna wakati hakuna matokeo yataonekana, kila kitu kitakuwa giza, hapo ndipo unapohitaji uvumilivyo maana mchakato wa ukuaji huchukua muda. Tujifunze kwa wakulima.
 67. Kushindwa na kutofikia mafanikio makubwa ni matokeo ya kupuuzia hatua ndogo ndogo tunazoweza kuzichukua kila siku. Hakuna utakacho kifanya kisilete matokeo, hivyo wekeza kwenye kufanya mambo ambayo unataka yakuletee matokeo bora. Rafiki yangu Godius Rweyongeza ameandika kitabu “Nguvu ya Vitu Vidogo Kuelekea Mafanikio Makubwa” ni kitabu kizuri sana kinachoelezea umuhimu wa kufanya vitu vidogo ili kuleta mafanikio makubwa, kitafute ukisome.
 68. Inatakiwa ufikie mahali kwenye maisha yako uachane kabisa na kutoa sababu kwanini huwezi au hutaki kufanya mambo yanayoweza kukuletea mafanikio kwenye maisha yako. Izike kabisa tabia ya kutoa sababu kwanini huwezi kuishi tabia za mafanikio.
 69. Amua kuwa kiongozi kwako mwenyewe, shika hatamu na jiwekee utaratibu mzuri wa kuishi maisha yako, jisimamie na jiongoze bila huruma ili utekeleze mambo muhimu ya kukuletea mafanikio. Jiongoze kwa mafanikio kwa kutumia nguvu ya uongozi iliyopo ndani yako.
 70. Kuna nguvu kubwa sana ya uongozi na ushawishi ndani yako, amua kuitumia nguvu hiyo juu yako mwenyewe, kujiongoza na kujishawishi ili ufikie ndoto zako. Hapa huitaji cheo chochote kuwa kiongozi kwako mwenyewe.
 71. Tuishi siku zote tukijua, siku zetu zinahesabika na miaka yetu ya kuishi hapa duniani ni michache, tufanye tunayotakiwa kuyafanya kwa ubora mkubwa, tujitoe na kujisukuma kila siku kufikia malengo yetu kabla mwisho wa siku zetu kufika.
 72. Kuna wakati mabadiliko ya kweli kwenye maisha yanahusisha zaidi yakigusa hisia zetu, badala ya kuwa na mlolongo wenye mantiki, moyo ukiguswa ndio huleta mabadiliko, na sio kichwani tu.
 73. Unapokuwa na nguvu nyingi za kuamua na kufanya maamuzi, ndivyo hivyo maamuzi yako yanakuwa na nguvu. Jitambue kama kiongozi mkuu na una nguvu nyingi za kuyaamulia maisha yako.
 74. Utakuwa na amani sana pale utakapofikia mwisho wa siku zako za kuishi hapa duniani endapo utajua ulitumia kila kipawa ulichopewa na Mungu kwa ukamilifu, na umeacha kazi bora hapa duniani kwa ajili ya kuboresha maisha ya watu wengine.
 75. Utakuwa na mwisho mwema wa siku zako za kuisha hapa duniani pale utakapojua ulifanya mambo yote ambayo yalikuwa mbele yako kwa viwango vya juu sana na kwa umakini wa hali ya juu.
 76. Utakuwa na mwisho mwema wa siku zako hapa duniani pale utakapokumbuka uliinua maisha ya wengi, uliboresha maisha ya wengi na uliwasaidia wengi kwa kazi zako, vipawa vyako na mali zako.
 77. Utakuwa na mwisho wenye furaha plae utakapokumbuka jinsi ulivyopitia nyakati nyingi za giza, hofu, mashaka, kushindwa, kuanguka lakini kila ulipoanguka uliinuka na kusonga mbele kwa ujasiri.
 78. Utakuwa na amani sana katika siku zako za mwisho pale utakapokumbuka kuwa hukusubiria cheo au nafasi yoyote ya uongozi ili ufanye makubwa kwenye ofisi, shirika au kwenye jamii yako.
 79. Utajishikuru sana katika siku zako za mwisho hapa duniani endapo hukutegemea cheo au nafasi ya uongozi mahali popote ili uishi kama kiongozi au ufanye mambo yako kama kiongozi. Utajishukuru kwa kuwa ulikuwa kiongozi asiye na cheo.
 80. Kuna kauli moja yenye nguvu sana iliyowahi kusemwa na Dr. Martin Luther kuhusu kufanya mambo kwa ubora wa viwango vya juu, alisema, kama mtu ameitwa kama mfanya usafi wa mtaa, anatakiwa kufanya usafi kwa viwango vya juu sana kama Michelangelo au Beethoven na sanaa yake ya muziki, au kama mshairi maarufu Shakespeare na mashairi yake. Anatakiwa afanye usafi wa mtaa kwa ubora kiasi kwamba jeshi lote la malaika wa mbinguni na duniani watasimama na kusema, hapa anaishi mfanya usafi bora wa mtaa aliyefanya kazi yake kwa ubora sana.
 81. Mwandishi amemnukuu Dr. Martin Luther kutuonyesha kuwa tunatakiwa kufanya kwa ubora wa viwango vya juu sana mambo yote ambayo yataangukia kwenye mikono yetu. Hata kama ni kazi ndogo kiasi gani, jifunze kujitoa kwa uwezo wako wote kuifanya kwa viwango bora sana.
 82. Pale unapodhani huna nguvu zozote hapo ndipo unapopoteza nguvu zako. Wengi wanajiona dhaifu, hawana uwezo wa uongozi, na wana dhana kuwa kiongozi lazima awe na cheo kama vile meneja, afisa fulani hivi au watu wenye vyeo serikalini.
 83. Ulikuja duniani bila cheo chochote na utaondoka duniani bila cheo chochote, lakini uliumbwa na silika ya uongozi ndani yako, kuna nguvu zote za kukufanya kuwa kiongozi bora unayetamani kuwa. Na ili kufikia viwango vya juu vya utendaji huitaji cheo, unahitaji kutumia nguvu ya asili ya uongozi iliyopo ndani yako.
 84. Mafanikio kwenye maisha hayaji tu kwasababu una nyota nzuri, mafanikio yanahusisha sana juhudi za makusudi za kila siku. Huwezi kujikuta tu umefanikiwa bila kufanya kazi, bahati kwenye maisha zinatengenezwa kwa juhudi na hatua za kila siku.
 85. Tumia maisha na muda wako hapa duniani kufanya vitu vyenye maana, usikazane kushilikilia vitu vya kupita ukaacha kuwekeza kwenye vitu muhimu zaidi, kama vile tabia yako, na kuboresha ujuzi wako ili uwe mtu bora sana.
 86. Ondokana na maoni ya watu kuhusu wewe, watu wataendelea kuwa na maoni juu yako hata ufanye jambo zuri kiasi gani. Hivyo usijali kuhusu maoni ya watu, jishindanishe wewe na wewe mwenyewe, jifanye bora kuliko jana.
 87. Hata kama jamii nzima inakupongeza kwa kufanya mambo mazuri na makubwa, hutakiwi kuishia hapo, unatakiwa kuendelea kutoa ubora na kujisukuma kila siku ili ufanye makubwa zaidi ya unayoyaona umefanya.
 88. Usipokuwa na imani imara juu yako, usipojiamini na kujikubali, ni rahisi sana kuyumbishwa na jamii, unatakiwa kuwa na imani thabiti kwako mwenyewe kuwa bado unaweza kuzalisha matokeo chanya kwenye maisha.
 89. Kama vile mwanamahesabu maarufu Albert Einsein alivyowahi kusema, kama unafanya makuu kwenye maisha yako, utakutana na upinzani mkubwa sana kutoka kwa watu wenye mitazamo duni.
 90. Mwandishi anasema kama watu hawaelewi unachotaka kukifanya, kwanini uwaruhusu wa kuvute chini, usiwaruhusu wakuangushe maana hawajui maono na ndoto zako. Tumia mawe wanayokurushia kujengea malengo yako.
 91. Wakati mwingine wanaotukosoa sana wanatukumbusha kuwa tunachokifanya kina maana sana na kinawaumiza, au ni kitu bora sana. Hivyo wakosoaji wanatufanya tusilale na tuendelee kupambania ndoto zetu.
 92. Vyeo vinaleta nguvu, lakini nguvu hii huondoka pale mtu anapokosa cheo. Suala la vyeo kwenye maisha lisikuumize kichwa, wewe wekeza nguvu zako kwenye kujifanya kuwa mtu bora na kiongozi bora kwako mwenyewe.
 93. Fikiria nguvu anayokuwa nayo mtu anapokuwa kwenye cheo cha ukurugenzi, au afisa wa juu, au waziri anaweza kuamuru hiki na kile. Lakini vyeo hivyo ni vya muda mfupi, hutakiwi kuwekeza kwenye vitu vya muda mfupi hivyo, wekeza kwenye kuwa kiongozi bora asiye na cheo.
 94. Kuna nguvu nyingi sana za uongozi ndani yako kuliko nguvu zilizopo kwenye vyeo unavyopewa, tuna nguvu nyingi za asili za kutufanya kuwa viongozi, nguvu hizi zipo ndani yetu, tumezaliwa nazo, nguvu hizi ni nyingi sana, nguvu hizi za ndani zina nguvu kuliko nguvu zilizopo kwenye vyeo vya kidunia.
 95. Mwandishi anasema, tukizitambua nguvu ziliyopo kwenye nguvu za uongozi ulio ndani yetu, hatutababaika na vyeo au nafasi za kuwa kiongozi tunazopewa na jamii. Vyeo vya uongozi tunavyopewa na jamii ni vya muda, na nguvu yake ni ya muda, lakini asili na nguvu ya uongozi wa kweli hauitaji cheo kudhihirika na kufanya makubwa.
 96. Mbaya zaidi ni kwamba nguvu hizi za uongozi zimelala ndani ya watu wengi, hazijadhihirika, hivyo watu hawajajitambua na wanafikiri uongozi wa vyeo vya kupewa na jamii ndio bora na una nguvu.
 97. Nguvu za asili za uongozi zilizopo ndani yetu haziwezi kuchukuliwa na mtu yoyote, na wala hazitengemei mambo yanayoendelea huku duniani. Ni nguvu takatifu, ni nguvu za asili, ni silika ya kweli tuliyoumbiwa na Mwenyezi Mungu, ni nguvu kubwa mno za kiutawala na kiumiliki.
 98. Kila binadamu aliye hai hapa duniani anahizi nguvu za uongozi ndani yake, na anaweza kwenda kwenye eneo lake la kazi na kuzidhihirisha kwa viwango vya juu; na huitaji cheo kufanya hivyo.
 99. Kila binadamu aliye hai hapa duniani ana nguvu za uongozi ndani yake za ushawishi, kuhamasisha, na kuwatia wengine moyo ili watumie vipawa vyao na kuwa mifano ya kuigwa; na huitaji cheo kufanya hivyo.
 100. Kila mtu aliye hai hapa duniani anaweza kuwa chanzo cha mabadiliko chanya licha ya mazingira hasi yanayomzunguka; na huitaji cheo kufanya hivyo.
 101. Kuna watu walikuwa na vyeo vikubwa kazini, kwenye mashirika, kwenye jeshi, na serikalini, na watu waliwaheshimu sana kwasababu ya vyeo na nafasi zao, lakini baada ya kuondoka kazini na kurudi mtaani walidhani watu watawachukulia na kuwaheshimu kama mwazo, jambo ambalo haliwezekani, hivyo kupelekea wengi kuwa na msongo wa mawazo na kukosa furaha.
 102. Haijalishi nafasi yako kazini, au unaishi kona gani ya hii dunia, bado una nguvu, haki na wajibu wa kudhihirisha haki yako ya kuzaliwa ambayo ni uongozi. Hakuna atakayekuzuia kuionyesha, ni wajibu wako kuifanya ifanye kazi.
 103. Kuongoza bila cheo ni falsafa ya kidemokrasia kwenye uongozi, maana inampa kila mtu nafasi ya kutumia nguvu ya uongozi iliyopo ndani yake kufanya makubwa bila kusubiria vyeo.
 104. Hakuna mtu hapa duniani asiye na umuhimu, na hakuna mtu mwingine hapa duniani kama wewe, upo wewe tu hapa duniani, hivyo ishi kwa falsafa ya kuongoza bila cheo ili ufanye makubwa kwenye kazi, biashara na jamii yako.
 105. Hakuna kiongozi aliyefikia ubora wa juu kwa kuwa mtu wa vising’izio na sababu. Watu ambao wapo bize kutengeneza sababu na visingizio hawana makubwa waliyowahi kufanya, na wala hawatakumbukwa na historia kwa nguvu wanazowekeza katika kutoa sababu na visingizio.
 106. Watu wengi wanapenda sana kutoa sababu na visingizio vingi kama vile, mimi sio meneja kwa hiyo siweza kufanya kitu hiki kwa kiwango bora, mimi sio mkurugenzi ndio maana sijafanya jambo hili kwa kiwango kinavyotakiwa, au nikipewa cheo au uongozi kwenye shirika au cheo ndio nitaonyesha dunia mimi ni nani.
 107. Mwandishi anasema, wengi wanakwama na kuwa watu duni na wasio na utukufu au mafanikio makubwa kwenye maisha yao na kwenye jamii kwasababu wanaendekeza sana sababu na visingizio vya kutokufanya mambo muhimu kwenye maisha yao.
 108. Robin anasema, watu siku hizi wamekuwa waoga sana kuwa halisi, sio wabunifu tena, wanabadili tu kanuni zilizofanya mambo yaenda kipindi cha nyuma, hawana ujasiri wa kuvumbua kanuni mpya, wanagusa gusa tu na hawana uhalisia wowote kwenye kazi zao.
 109. Izoeshe akili yako ifanye kazi kwa namna ya ufumbuzi na ubunifu, mfano kila unapoianza siku yako, angalia ni jambo gani muhimu la kuboreha, usifanye mambo yako kwa mazoea, boresha kila idara kwenye maisha yako.
 110. Unajua unaweza kuwa duni au wa kawaida bila hata wewe kujua, kama hutajisukuma kila wakati na kuchukua hatua za ziada kila siku utashangaa unaishia kuishi maisha ya chini sana na utaona kawada tu, kila siku jifanyie tathimnini.
 111. Katika ulimwengu wa biashara, inahitaji sana ubunifu na kufanya mambo kwa namna mpya kila siku. Mwandishi anasema kama unataka biashara yako ife mapema, basi fanya mambo kwa mazoea bila ubunifu.
 112. Unahitaji kujua mambo mengi sana muhimu kuhusu biashara unayoifanya, huwezi kufanya biashara katika zama hizi kama vile ilivyofanyika miaka 10 iliyopita, dunia ya biashara na ushindani inadai ubunifu na uelewa mkubwa sana ili ikue na uyaone mafanikio kwenye biashara.
 113. Usiache kujifunza na kuwekeza katika kuwa mtu bora, biashara itakuwa bora kwa jinsi ulivyo bora, wekeza na tumia fursa za teknologia zilizopo kuinua na kuboresha biashara yako kila siku.
 114. Mwigizaji maarufu Steve Martin aliwahi kusema, kuwa mtu bora kweli kweli kiasi kwamba watu washindwe kabisa kukupotezea.
 115. Viongozi wanahakikisha yale yote muhimu waliyoyapanga kuyafanya wanayafanya bila kughairisha. Kamilisha kazi zako na mambo yote muhimu kwenye siku yako, haijalishi upinzani ni mkubwa kiasi gani, kamilisha kazi zako kwa viwango bora.
 116. Jiongezee mategemeo makubwa kutoka kwako mwenyewe, na jitoe kwa namna isivyo kawaida ili ukamilishe mategemeo makubwa uliyojiwekea. Tegemea makubwa na vitu vingi zaidi kutoka kwako mwenyewe kuliko kutegemea kutoka kwa wengine.
 117. Jinsi unavyojituma na kufanya kazi kila siku ndivyo unavyogundua nguvu za uongozi zilizopo ndani yako. Kazi zinakufanya uendelee kujigundua na kuibua vipawa na nguvu ambazo hukudhania kama unazo.
 118. Kazi ni jukwaa la kutufanya tugundue vipawa, ubunifu na nguvu zilizolala ndani yetu, kazi ni moja ya jambo ambalo linaongeza furaha katika maisha yetu, hivyo jitoe kufanya kazi bora kila siku.
 119. Moja ya kazi kubwa unayotakiwa kufanya hapa duniani na kuondoa kila aina ya ngome na imani potofu zinazoweka ukomo kwenye uwezo wako.
 120. Imani na mapokeo yanamchango mkubwa sana katika kuunda tabia zetu za kila siku, vitu tunavyoviamini kwa muda mrefu vinaushawishi sana kwenye tabia zetu za kila siku, na tabia ndio huamua maisha tunayoishi na matokeo yake.
 121. Watu sio duni tu kwasababu ni duni, watu ni duni kwasababu wana tabia duni; watu sio masikini tu kwasababu ni masikini, watu ni masikini kwasababu wanaishi tabia za kimasikini na wanaziishi kila siku.
 122. Watu ni viongozi na matajiri kwasababu wanaishi tabia za kiuongozi na za kitajiri kila siku; hivyo tunatakiwa tuyapitie tena maisha yetu tuone kama mwenendo wa tabia zetu unatupeleka kwenye mafanikio na ndoto zetu. Kuna rafiki yangu anaitwa Dr. Makirita Amani, ameandika kitabu kizuri sana kuhusu “Tabia za Kitajiri”. Kitafute kitabu hiki, ni kitabu bora sana kwa mafanikio na utajiri.
 123. Jihesabu kuwa wewe ni moja watu wanaweza kufanya makubwa, usijichukulie kama mtu duni, fukara na asiye na matumaini, jehesabu wewe kuwa mbarikiwa, mtu anayeweza kupata mafanikio, siku zote ishi maisha yako ukiwa na mawazo chanya.
 124. Tumia muda wa kutosha kujifunza ili kufikia ubobezi wa jambo lolote, bobea kwenye taaluma yako, biashara yako au kipaji chako. Utafiti unaonyesha ili kuwa mbobezi kwenye jambo lolote unahitaji zaidi ya masaa 10000 ya maandalizi na kujifunza sana.
 125. Njia ya mafanikio imejaa gharama nyingi sana, kuna vitu utaachana navyo, kuna vyakula hutakula, kuna vinywaji hutakunywa, kuna marafiki utaachana nao, kuna wengine watakutenga, kuna fedha utapoteza, kuna masaa mengi ya usingizi utapoteza ili kupigania ndoto zako.
 126. Unapoianza safari mara zote ni ngumu sana mwanzoni, ni nguvu kubwa sana inahitajika ili uanze jambo fulani, lakini unapolianza na linapokuwa kwenye mwendo ugumu unapungua. Mfano, wakati roketi inaanza kuruka kwenda kwenye anga la juu sana huwa inatumia nguvu na nishati nyingi sana kutoka katika anga la dunia; hivyo ndivyo ilivyo kwa mwanzo wa jambo lolote, mwanzo wa biashara, tabia mpya au mafunzo, utatumia nguvu nyingi mwanzoni mwa jambo.
 127. Unapokua kiongozi hutakiwi kuwa na kauli mbili, unasema hivi na kufanya vile, fanya unachosema na sema utakachofanya. Hutakiwi kuwa na maisha ya aina mbili, maisha yako ya mchana ndio yawe hayo hayo ya usiku.
 128. Jinsi unapojipa ruhusa ya kuwa muwazi, huru, halisi na wa mwenye akili kwa wengine ndivyo na wengine wanavyokuwa huru, wazi na halisi kwako. Wafanye watu wanaokua pamoja na wewe wajisikie wapo salama, huru na wazi.
 129. Nyakati ngumu huzalisha viongozi imara. Uwezo wa kustahimili dhoruba za maisha na namna ya kufanya maamuzi sahihi wakati wa nyakati ngumu ndio sifa kuu ya viongozi bora.
 130. Viongozi bora ni watulivu sana katika nyakati ngumu, mambo yanapoharibika na kwenda mrama, hapo ndipo ilipo sanaa ya uongozi bora.
 131. Nyakati za kiza huwa hazidumu, lakini watu imara hudumu kwenye nyakati zote, moja ya sifa ya kiongozi ni uvumilivu na matumaini makubwa kuwa haya yanayopita kwenye maisha yataisha, hayatadumu milele, hivyo hawapaniki.
 132. Mwandishi Og Mandino alinukuliwa akisema, atavumilia hadi afanikiwe, hajaja hapa duniani kushindwa. Yeye ni simba na sio kondoo anayehitaji kuongozwa na mchungaji, yeye ni simba na amekataa kuongea, kutembea na kulala na kondoo. Nitavumilia hadi nishinde.
 133. Nyakati ngumu zilizojaa changamoto ndio huibua namna bora ya kuishi, mipango mipya ya maisha na utaratibu imara wa kujenga biashara na uwekezaji. Ukiweza soma kitabu cha Dr. Myles Munroe kinachoitwa “Overcoming Crisis”, utajua umuhimu wa dhoruba, majanga, na changamoto kwenye maisha.
 134. Nyakati ngumu tunazopitia kwenye maisha ndio hufanya mambo magumu yaende, au yafanyike. Tunapopitia changamoto na hali nguvu huwa tunatumia nguvu na akili nyingi sana ili mambo yakae sawa na yaende, ndio kipindi hiki kigumu ndio hufanya mambo mangumu na tuliyoyaona hayawezekani kuwezekana na kufanyika.
 135. Hivyo ili tuwe bora na kujenga misuli ya kusimama kwenye nyakati ngumu inatakiwa tuache kuzikimbia changamoto, tuache kizikimbia hofu, tunatakiwa kufanya yale yote muhimu tunayoyahofia.
 136. Ukuaji upo katika ratiba ngumu, mafunzo magumu, na uzoefu wa kupitia changamoto na nyakati ngumu. Usikimbie changamoto zako, zikabili zikusaidie kuwa imara. Kama alivyoimba msanii nguli na maarufu wa wa Bongo Flava, Mwana FA, shida hazikwepeki, zipo ili zitutoe misuli, zitokomaze, zitotoe macho, zitutoe jasho, zitupe akili na zituandae kwa kesho.
 137. Mwanamama mashughuri Hellen Keller aliwahi kusema tusingekuwa na watu wastahimilivu na majasiri kama dunia ingekuwa na furaha na raha pekee. Maana yake anasema majanga, dhoruba, vita, kuonewa, ubaguzi, utumwa, kukosekana kwa haki na usawa, ndio kumezalisha watu mashujaa, watu mahiri na viongozi imara.
 138. Dhana ya uongozi inahitaji zaidi kutumia nyakati ngumu, changamoto za maisha kwa faida yako. Maana yake viongozi wanatakiwa kunufaika na kufaidika na changamoto za maisha ili wawe bora na imara.
 139. Unapofikia kwenye kingo za mwisho kabisa za uwezo wako, nakujiona huwezi kuendelea hata hatua moja, na mwili wako kuanza kujisikia hovyo hovyo na akili yako vikianza kupiga kelele kama vile unataka kufa kutokana na jinsi ulivyojisukuma kuchukua hatua zaidi, mwandishi anasema hapo ndipo unapojihisi kuwa upo hai kama binadamu na ukuaji mkubwa hutokea kwenye nyakati kama hizi.
 140. Chukua hatua hata kama haupo tayari, chukua hatua hata kama kuna hofu zinakutisha, chukua hatua hata kama unajisikia huwezi tena kuchukua hatua. Miili yetu ina tabia ya kutoa taarifa za vitisho kwamba tunaweza kufa, tunaumia nk pale unapochukua hatua za ziada. Ukiweza soma kitabu cha 25 Hours a Day cha Nick Bare, kitakupa sababu nyingi kwanini hutakiwi kuusikiliza mwili wako unapofanya maamuzi muhimu.
 141. Kila mtu anaweza kujiona yeye ni mshindi katika nyakati za amani ambazo hakuna upinzani, biashara inaenda vizuri, uchumi upo imara, na mambo mengine yanaenda. Lakini mwandishi wa kitabu hiki anasema ukitaka kujua upo imara kiasi gani, pitia changamoto na magumu bila kutetereka.
 142. Kila mara unapofanya vitu vinavyokutia hofu na mashaka unadhihirisha uwezo wa kiuongozi. Uwezo wa kiuongozi huonekana pale unapofanya mambo yako licha ya upinzani kuwepo.
 143. Watu majasiri hawazikimbii hofu, huwa wanazila hizo hofu kabla ya hofu kuwala wao. Usikubali hofu zikakumeza mzima mzima, una uwezo mkuu ndani yako wa kukabiliana na hofu zinazokuja kwenye maisha yako, kuwa wa kwanza kuzimeza hizo hofu kabla hazijakumeza wewe. Kama unaweza soma kitabu cha “How to Stop Worrying and Start Living” cha Dale Carnegie ujue namna ya kuachana na hofu.
 144. Kumbuka, hutajua una uwezo kiasi gani, au una nguvu kiasi gani, au unaweza kufika mbali kiasi gani kama hutaanza na hatua moja. Anza mapema ili ujue nguvu, uwezo na vipawa vyako.
 145. Kila wakati unapokuwa tayari kukabiliana na hatari, au unapoandamwa na hatari nyingi, ujue upo karibu zaidi na mafanikio.
 146. Itakugharimu sana kukaa kwenye mchakato, mchakato utadai zaidi matumizi ya nguvu na uwezo ambao hujawahi kuutumia ambao umelala ndani yako. Rafiki yangu Alfred Mwanyika ameandika kitabu kizuri sana kinachoitwa “Amsha Uwezo Wako Halisi”, Kitafute kitabu hiki ujisomee utajua mengi sana.
 147. Fanya kile kinachokitia hofu, fanya kile kinachokuogopesha kila siku, kwa kufanya hivyo utaondoka kwenye hofu, na utageuza hofu na mashaka yako kuwa nguvu za kukusukuma mbele zaidi.
 148. Watu unaowaona wenye bahati hawapati tu bahati, wanatengeneza bahati kwa kwa kuwa tayari kufanya mambo hatari kwa ujasiri na kutumia vizuri fursa zinazokuja mbele yao.
 149. Ondoka na acha kucheza ligi ndogo ndogo za daraja la kwanza, ingia kwenye ligi za mabingwa, ujifunza na kupambana na mabingwa wenzio. Wakati umefika uondoke kwenye ligi za mchangani, uingie kwenye ligi za mabingwa duniani.
 150. Huwezi kuingia kwenye ligi kubwa za mabingwa kama utaendelea kufikiri na kufanya mambo yako kama unajiandaa kucheza ligi za mchangani. Maandalizi ya kucheza ligi za mabigwa ni makali sana, yanahitaji kujitoa sana na kujisukuma sana maana hakuna myonge anayecheza ligi za mabingwa. Mwandishi na bilionea wa Marekani Donald Trump, aliandika kitabu kizuri sana, kuhusu namna ya kufikiri kama mabingwa na kufanya kama mabingwa, kinaitwa “Think Like a Champion”, kitafute ukisome.
 151. Matatizo ni matatizo pale tunapoyafanya kuwa matatizo. Namna unayochukuliana na changamoto zinazopita kwenye maisha yako ndio huamua namna unavyotumia matatizo kama fursa au matatizo kama matatizo. Angalia namna unavyoyatafsiri matatizo, usiyaangalie matatizo kama laana, au kitu hasi na kibaya kwenye maisha yako, yaangalie matatizo kama fursa za kukufanya uboreshe maisha yako, ili uwe bora kuliko changamoto unazopitia.
 152. Kama kuna kitu ni muhimu kwa mtu ambaye ni muhimu kwako, basi kitu hicho kinatakiwa kuwa na umuhimu kwako pia. Mfano, kama unaniona mimi nina umuhimu kwako, na pia nina kitu ambacho ni muhimu, kitu hicho ambacho ni muhimu kwangu kinatakiwa kiwe muhimu na kwako pia.
 153. Chagua vizuri maneno ya kuongea na watu, usiongee tu chochote kwa namna ambayo sio nzuri. Unaweza kuwa una ujumbe mzuri na muhimu lakini ukatumia lugha ambayo sio nzuri, ambayo inawashushia watu heshima, watu hawatakusikiliza wala kutekeleza ulichosema. Maneno yako yanaweza kuonyesha watu njia, maneno yako yanaweza kuwafanya watu wakaona fursa mpya, maneno yako yanaweza kuwafanya watu wakawa na furaha. Tumia lugha nzuri kufikisha ujumbe wako.
 154. Tumia lugha sahihi ya kuwasilisha ujumbe wako, hata kama jambo unalotaka kuliwasilisha kwa hadhira yako ni gumu kiasi gani, unapochangua maneno mazuri na ukalisema kwa namna nzuri watu watalielewa jambo hilo na watalifanyia kazi.
 155. Kabla hujaianza siku yako, changua mambo machache muhimu ambayo utayafanya siku hiyo, baada ya kuyachagua weka umakini wako wote na nguvu zako zote katika kuyafanya, kamwe usijihusishe na mengine, fanya hayo machache uliyoyachagua hadi yakamilike.
 156. Unaweza kutumia kanuni ya Pareto katika kufanya mambo yako; kanuni ya Pareto ni 20/80, kati ya mambo machache unayochagua kufanya ndio yatakupa matokeo makubwa au 20% ya mambo unayoyafanya ndio yatakupa 80% ya matokeo, na kinyume chake pia.
 157. Upande mwingine wa kanuni hii maarufu inaaleza kuwa endapo utafanya 80% ya mambo yako, utapata matokeo ya 20% tu, hivyo mambo machache tu muhimu utakayochagua kuyafanya ndio yanaweza kukupa matokeo makubwa. Tafuta kitabu kilichoandikwa na Richard Koch “The 20/80 Principle” ili ujufunze kwa undani kanuni hii.
 158. Chagua vitu vichache na nyeti sana uvifanye, vitakuwa na matokeo makubwa sana kwenye maisha yako, usifanye tu mambo mengi, chagua kwa umakini vitu nyeti, vichache na vifanye kwa nguvu, akili, na moyo wako wote.
 159. Mwandishi wa kitabu hiki anasema, huwezi kujulikana kwa kufanya mambo mengi, mambo mengi yatakuchosha na yanafanyika bila ufanishi, mambo mengi hayatakufanya uwe mbobezi. Mambo muhimu machache ndio yatakufanya kuwa mbobezi.
 160. Robin Sharma anasema, tuna nguvu ngingi sana kuliko nguvu ambazo tunasifiwa kuwa tunazo. Nguvu hizi mara nyingi huibuka pale changamoto zinapotokea kwenye maisha yetu. Endelea kujisukuma na kuchukua hatua hata kama unaona ndio kitu cha mwisho kabisa kufanya.
 161. Mambo yote ya mafanikio na kufanikiwa yanategemea sana maamuzi yetu. Hata kuamua kutoamua pia ni maamuzi.
 162. Wajapani wana msemo wao maarufu sana, unasema ukianguka au kuangusha mara saba, amka mara nane zaidi. Maana yake mchakato wa kuendea ukuu wako na mafanikio yako, kuna kila upinzani na kuna wakati utaanguka na kuangushwa, hivyo haijalishi unaanguka mara ngapi, unachotakiwa kufanya baada ya kuanguka ni kuinuka na kuendelea, na sio kulala hapo hapo.
 163. Kamanda wa kivita wa jeshi la uingereza kipindi hicho Winston Churchill aliwahi kusema, kamwe usikate tamaa, kamwe, kamwe, kamwe, usije kukata tamaa, kwa vitu vikubwa au vidogo kamwe usikate tamaa, endelea mbele kupigania ndoto na maono yako.
 164. Mwandishi anasema, ni bora ukaingia na kushindwa vibaya, kuliko kukaa tu nyumbani ukiwa unaangalia televisheni, maana ukishindwa utajifunza, ukianguka utainuka ukiwa imara na mwenye uzoefu zaidi.
 165. Inuka mara nane zaidi kwa kila ulipoanguka, changamoto zinakupima ni kwa kiasi gani unahitaji unachokitafuta. Ukiwa katika biashara ndio kabisaa, hutakiwi hata kuwa na wazo la kukata tamaa, maana ulimwengu wa biashara una mambo mengi mapya kila siku.
 166. Wakati wengine wakisubiria amri na matamko ya viongozi ndio waanze kuchukua hatua, wewe unatakiwa kuwa wakwanza kufanya mambo yote muhimu bila kusubiria matamko.
 167. Kama kuna kanuni muhimu ya mafanikio basi ni kujua namna ya kuishi na kuchukuliana na watu. Unahitaji watu ili ufanikiwe kwenye jambo lolote, biashara, kazi, elimu. Weka mahusiano yako yawe bora na watu, katika jamii yetu ya sasa watu wanaweka pesa mbele zaidi ya utu. Mwandishi anasema ukiwafanyia watu vizuri watakuletea fedha zao, na mali zao.
 168. Kama unataka kushinda, basi wasaidie wengine kushinda, kama unataka fedha wasaidie wengine kupata fedha hivyo ndivyo dunia inavyofanya kazi.
 169. Ni asili ya binadamu kuwa unapowasaidia na wao wanafanya kila wanachoweza kukusaidia pia. Unaweza ukawasaidia watu na usiwe na matarajio ya kuja kusaidiwa nao baadaye, lakini ukweli ni kwamba, lazima watakuja kukusaidia tu.
 170. Mwandishi Robin anasema, toa kile unachokitamani sana kupokea, mfano kama unapenda msaada basi toa zaidi misaada kwa wengine, wasaidie wengine, kama unataka upendo toa zaidi upendo, kama unataka heshima toa heshima.
 171. Kanuni hii ya utoaji ipo pia katika Biblia, Yesu Kristo aliwahi kuwaambia wanafunzi wake, “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa” Soma Kitabu cha Luka 6:38.
 172. Watu watashawishiwa zaidi na mwenendo na matendo yako kuliko kauli zako. Ni asili ya binadamu hawapendi kuongozwa au kuamrishwa, hivyo njia nzuri ya kuwafanya watu wanaokuzunguka kufanya unayoyataka, unatakiwa uwe mfano mzuri wewe mwenyewe.
 173. Mwanamahesabu Isaac Newton aliwahi kusema, ukiona naona mbali kuliko wengine ni kwasababu nimesimama kwenye mabega ya watu hodari. Hapa alimaanisha mafanikio yote niliyonayo, mambo yote ninayoyajua ni kwasababu nimejifunza kwa watu wakuu zaidi.
 174. Kuwa tayari kuwasilikiliza watu na kuongea na watu, wape watu heshima na utu, mnapokua pamoja na wenzako, onyesha ushirikiano, sio upo na watu huku unatumia simu yako, umeweka earphone masikioni.
 175. Mahusiano imara yanajenga uongozi imara. Kuwa tayari kushiriki kwenye mambo ya wenzako, onyesha kujali kwenye mambo ya wenzako.
 176. Jifunze kuwa msikilizaji mzuri, onyesha umakini wako wote unapomsikiliza mtu, sikiliza zaidi kuliko unavyoongea. Wengi wanadhani wale wanaoongea sana ndio wana majibu au wanajua mambo mengi, kumbe sio kweli.
 177. Uongozi sio kuongea sana, au kuongea kila mara, kuna watu wanadhani kiongozi ni mtu wa kuongea ongea sana, kushauri sana, kutoa maelekezo sana nk. Uongozi wa kweli ni kushuka chini na kuwa tayari kusikiliza watu wengine wanapoongea.
 178. Uongozi ni kuwa tayari kuwafanye wengine wasikike pia. Uongozi ni kuinua sauti za walio kimya na wao waongee na washauri na kutoa maoni yao.
 179. Kumbuka jambo hili kwenye maisha yako, kuwa watu wanapenda kufanya biashara au kufanya kazi na watu wanaowapenda. Hivyo kama huna mahusiano mazuri na watu hata ufanisi wako kazini utakuwa chini sana.
 180. Kila siku tenga muda wa kuzungumza na watu wako wa karibu, watu wako muhimu. Licha ya fujo zote za utandawazi na ulimwengu wa kidigitali tulio nao tenga muda kwa ajili ya kufanya mawasiliano muhimu. Hii ndio njia nzuri ya kukuza mahusiano.
 181. Hakuna aliye shujaa leo aliyefanya mambo yote mwenyewe bila msaada wa watu wengine. Wajali wengine, wape nafasi wengine wachanue, na wewe utachanua na kuwa mkuu sana.
 182. Ili uwe kiongozi bora inatakiwa uwe mtu bora kabisa. Hii ni kwasababu huwezi kuwapa watu nguvu kama wewe huna hizo nguvu.
 183. Huwezi kuwafanya wengine kuwa bora kama wewe sio bora. Huwezi kuwafanya wengine wajisikie vizuri kama wewe hujisikii vizuri mwenyewe.
 184. Watu wakiwa bora kila wanachokifanya kitakuwa bora, kazi zitakuwa bora, ofisi itakuwa bora, shirika litakuwa bora na watatoa matokeo au huduma bora sana.
 185. Tengeneza mkakati wa kufanyia kazi uwezo wako uliolala, tafuta namna unaweza kujiunganisha na uweze kutumia uwezo wako wa kipekee uliolala ndani yako bila kutumika.
 186. Jisafishe fikra zako na ondoa mawazo na imani hasi kuhusu uongozi, jitambue kwa viwango vya juu sana na wekeza nguvu zako kwenye uwezo wako uliolala ili utumike kukusaidia wewe na jamii nzima.
 187. Jifunze kwa nguvu zako zote namna unavyoweza kuitunza afya yako, maana bila kuwa na afya njema hutaweza kuhimili dhoruba na mikiki mikiki ya dunia hii. Mafanikio yanakuhitaji uwe na afya njema siku zote.
 188. Ili uendelee kuwa na afya njema, unatakiwa kuondoa hisia mbaya za chuki, uchungu, hofu na majuto ambazo zinaweza kudhorotesha nguvu zako na afya yako ukaishia kuwa mtu dhaifu.
 189. Ili uwe na afya bora ya mwili, akili na roho yako, inatakiwa uwe mtu wa rohoni, ishi na wekeza kwenye maisha ya rohoni. Mwandishi anasema kuna nguvu kubwa ya kufanya yasiyowezekana hapa duniani, nguvu hizo hazipo duniani bali zipo katika ulimwengu wa roho.
 190. Jiunganishe na chanzo cha uongozi, jiunganishe na Mungu wako, maana yeye ndie ametoa vipawa na kusimika roho ya uongozi ndani yetu, unaporudi na kujenga uhusiano imara na Mungu wako, maisha yako yatakuwa na ushawishi mkubwa sana na pia utakamilisha hata yale uliyoyaona hayawezi kukamilika. Kama unataka kuelewa zaidi kuhusu kusudi na chanzo cha uongozi ulio ndani yako nakushauri usome kitabu cha Dr. Myles Munroe, kinachoitwa The Spirit of Leadership.
 191. Wakati sahihi wa kufikiri ni alama gani utaiacha hapa duniani ni sasa. Wengi wanagundua vitu wanavyotakiwa kuvifanya wakati ambao muda umeenda sana, na wengine wanakumbuka wakiwa karibu na umauti. Weka mikakati sasa.
 192. Kipimo cha mafanikio kinatakiwa kiwe ni kufikia kuwa mtu bora, mwenye maadili bora sana, mwenye utu, mtu huru, asiye na huzuni, chuki, hofu. Na sio kupima mafanikio kwenye vitu vya muda na vinavyoharibika kama mali na fedha.
 193. Ndio maana watu wakivipoteza fedha, mali au utajiri wanaomiliki wanaishia kuchanganyikiwa, kupata maradhi na wengine wanajiua. Mwandishi anasema, fedha, mali ni vitu vya mud asana, na hivitakiwi kuwa ndio vitu pekee vinavyokutambulisha.
 194. Chukua Jukumu la kusimamia kulinda ufahamu na akili zako, usiruhuru tu kila kitu kingie tu kwenye ufahamu wako na kuanza kuzunguka zunguka humo hovyo. Mwandishi anasema usiruhusu hata sekunde moja wazo hasi likaingia kwenye fahamu au akili yako.
 195. Ufanye ufahamu na akili yako kuwa sehemu takatifu mno, weka ulinzi mkali kwenye mifumo yako yote ya fahamu ili isipitishe mambo hasi na yasiyofaa kwenye akili na fahamu zako. Ilinde akili na fahamu zako kama vile Mwenyezi Mungu alivyoilinda bustani ya Edeni, ili kuzuia vitu au watu waovu wasiingie humo.
 196. Fikra zako, akili zako na fahamu zako ni kiwanda na sehemu muhimu ya kuchakata taarifa. Usiruhusu mambo ambayo hutaki yatokee kwenye maisha yako yakaingia kwenye fahamu zako. Najua hili linaweza kuwa moja ya jukumu kubwa sana la maisha yako, unahitaji nidhamu kubwa sana kufanya jambo hili.
 197. Mahatma Gandhi, baba wa taifa la India na mwanamapinduzi na moja ya watu mashughuri sana waliowahi kuishi hapa duniani alisema, hatoruhusu watu kutembea kwenye fahamu na akili zake wakiwa na miguu yao michafu. Maana yake alikuwa hatoi ruhusa mawazo hasi, vinyongo, uchungu au mambo maovu kuingia katika fahamu zake.
 198. Jifunze kusamehe unaohitaji kuwasamehe, huitaji tena kuishi ukiwa umeshikilia mambo ya zamani, yaache yaliyopita yapite. Huwezi kuwekeza kwenye kufanya maisha yako ya baadaye kuwa bora kama bado umeshikamana na mambo ya kale.
 199. Mwandishi anasema, ni watu walioumizwa ndio huwaumiza wengine. Usiwe mtu wa visasa, visa na magomvi. Kuwa mtu huru, samehe, kuwa mtu wa upendo kwa wote. Uishi maisha yako kwa furaha.
 200. Mwandishi wa kitabu hiki anasema, anatamani sana maarifa na mafunzo yote uliyojifunza kwenye kitabu hiki umshirikishe na rafiki yako, mfanyakazi mwenzako, ndugu au jamaa yako. Unaweza kumnunulia kitabu hiki kama zawadi, au unaweza kumtumia linki ya uchambuzi huu akajifunza. Kama uchambuzi huu umekuwa muhimu kwako, basi mshirikishe na rafiki yako wa muhimu uchambuzi huu. _Gift The Leader Who Had No Title to coworkers, friends, family members, and even strangers. They will learn that they are meant to lead in all they do and live great lives.
  _
  @Hillary Mrosso_30 September 2022


One response to “Uchambuzi wa Kitabu: The Leader Who Had no Title (Kiongozi Asiye na Cheo); Mambo 200 Niliyojifunza katika kitabu hiki.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X