Uchambuzi Wa Kitabu: 25 Hours a Day; Going One More to Get What You Want



Mwandishi: Nick Bare
Mchambuzi: Hillary Mrosso
Simu: 255 683862481

UTANGULIZI
Karibu katika uchambuzi wa kitabu bora sana cha 25 Hours a Day. Kikiwa na maana ya kwenda hatua moja zaidi kupata kila unachokitaka. Mwandishi ametumia uzoefu wake wa kijeshi kutengeneza nidhamu kubwa kwenye maisha yake binafsi, maisha ya biashra na mafanikio. Kama unavyojua jeshini kikubwa ni nidhamu ya kufanya mambo. Jeshini hawataki maelezo kwanini umeshindwa kufanya jambo ulilotakiwa kufanya, jeshini ni matokeo ndio yanayotakiwa. Kama umekosa nidhamu, umakini, kujituma, na hamasa ya kufanyia kazi ndoto zako. Basi hiki ndio kitabu kinachokufaa zaidi kukisoma.

Katika uchambuzi nimekuandalia mambo 75 niliyojifunza katika kitabu hiki. Karibu tujifunze.

  1. “Usipomlilisha ng’ombe wako atakufa”. Hii ni kauli inayotumika kila eneo la maisha, usipolisha ndoto zako zitakufa, usipolisha biashara zako zitakufa, usipolisha kampuni yako itakufa. Maana yake vitu havitatokea tu kwenye maisha yako bila kuvifanyia kazi ili vitokee.
  2. Vitu vikubwa unavyoviona vimetokea kwa watu wengine inamaana kuwa walivifanyia kazi, waliingia gharama kubwa kuvifanya vitokee. Jifunze kupitia wao, hasa uvumilivu na nidhamu iliyowafanya wafikie ndoto zao.
  3. Ili uweze kufanyia kazi ndoto zako lazima uwe na umiliki mkubwa wa muda, usikubali mambo na changamoto zikupeleke zinavyotaka, unatakiwa kushika usukani, uwe dereva na ufanye yale yalio ya muhimu kufikia ndoto zako.
  4. Kila unachotamani kukifanya kwenye maisha yako, itakuhitaji kujitoa vya kutosha kabisa. Mfano, mwandishi wa kitabu hiki Nick Bare anasema, chochote alichotamani kwenye maisha yake, aliingia gharama na kujitoa kukifanyia kazi kwa asilimia 100.
  5. Mwandishi wa kitabu hiki cha kipekee Nick Bare anasema, hakuna anayefanikiwa kwenye maisha yake kwa kutofanya chochote. Hakuna mafanikio yatakuja kwako ukiwa umekaa tu au umesimama tu, mafanikio yanataka ujitoe kwa viwango vya juu sana.
  6. Tunatakiwa kuwa na shauku na njaa kali sana ya kufanikiwa na kufanyia kazi malengo na ndoto zetu, chochote unachoona unapaswa kukifanya ili ufanikiwe unatakiwa kujitoa kwa asilimia zote ili ufanikiwe.
  7. Mwandishi anasema, vifuatilie vitu vigumu unavyotakiwa uvifanye ili ufanikiwe kwenye maisha yako. usiache magumu ndio yakufuate wewe, wewe ndio unatakiwa kuyafuata magumu na kuyatatua ili ukue na kufanikiwa.
  8. Kuwa tayari kukabiliana na mambo magumu na vikwazo kwenye safari ya maisha yako; mafanikio yamejificha kwenye mambo magumu yaliyopo kwenye maisha yako.
  9. Kuwa tayari kupokea upinzani kutoka kwa watu wako wa karibu, maana wanaweza kukukatisha tamaa, wanaweza kukuumiza, wanaweza kukutenga, wanaweza kukuonea wivu; mwandishi anasema kuwa tayari kukabiliana nayo.
  10. Kuna wakati miili yetu inachoka na inapeleka taarifa kwenye fahamu zetu ili tusitishe tunachokifanya. Mwandishi anasema, hali hiyo ikitokea hutakiwi kuacha unachokifanya badala yake unatakiwa kuendelea kufanya kazi.
  11. Mafanikio hayaji kwa watu wanaoacha kufanya jambo ambalo linawapeleka kwenye mafaniko yao pale wanapochoka. Mafanikio yanakuja pale unapoenda zaidi ya uchovu unaoupata kwenye mwili wako.
  12. Akili yako haitakiwi kukubaliana na kila kinacholetwa na mwili, kuna wakati akili zinataka tuendelee kufanya kazi na kujituma, lakini mwili hautaki unakwambia umechoka, unakuletea uchovu, maumivu, usingizi. Bare anasema, unatakiwa kuwa na nguvu juu ya mwili wako ili kufanyia kazi ndoto zako.
  13. Nick Bare, anasema wakati wakiwa katika ratiba za kijeshi, huwa hawaachi kwasababu wamechoka, au miili yao inaleta maumivu, wanaacha pale wanapokamilisha ratiba ya siku au jambo hilo au mtu anapoumia au kuvunjika.
  14. Ili kufanikiwa na kufikia mafanikio makubwa, nguvu za mwilini pekee hazitoshi, tunatakiwa kuwa na nguvu za akili ambazo hazitakubaliana na taarifa za mwili kwamba tumechoka, tunaumia, tunahitaji kupumzika, tuna njaa.
  15. Bare anatufundisha kuwa akili ndio inatakiwa kuendesha mwili na sio mwili uendeshe akili. Akili ikiwa na nguvu na ushawishi itakutoa kwenye kufanya mambo ya kinyonge, utajituma sana, utaondoka kwenye comfort zone.
  16. Furaha kubwa tunaipata pale tunapotatua mambo magumu kwenye maisha yetu. Zifuatilie ndoto unaziona ni ngumu kwenye maisha yako, ifuatilie biashara uanayoina ni ngumu kwenye maisha yako kuifanya, ifuatilie kazi unayoina ni ngumu kuipata au kuifanya na uifanye; endapo utafanikiwa kuvuka hapo utakuwa mwenye furaha sana.
  17. Nick Bare ansema, juhudi na kujitu kwenye maisha yake kunatokana na mfano mzuri kutoka kwa wazazi wake ambo walikuwa wanafanya kazi kwa bidii sana. Bare anasema kuna wakati anamuona baba yake akifanya jambo kwa kujituma kwa muda mwingi kuliko ilivyo kawaida.
  18. Ukiusikiliza mwili wako kwenye kila taarifa inayokupa hutaweza kukabiliana na mambo magumu yatakayotokea maishani mwako, hutafurahia mafanikio makubwa, utakuwa mtu wa kawaida na masikini.
  19. Usighairishe mambo muhimu kwenye maisha yako, usikatie tamaa ndoto zako au mafanikio yako. Kuwa msitari wa mbele kabisa kutetea ndoto zako, jitoe kwa isivyokawaida ili kufikia mafanikio yako.
  20. Unatakiwa kuwa na ufahamu wenye nguvu sana ili uamue kufanya mambo muhimu kwenye maisha yako. Usipofanya hivyo mwili utakunyanyasa sana, na hutaweza kufikia mafanikio yako unayoyatamani.
  21. Yafanye maumivu unayoyapata mwilini mwako ndio yawe mafuta, yawe kichocheo cha wewe kuzidi kusonga mbele na sio yawe ndio njia ya kuacha kufanya ulichokuwa unafanya. Yafanye maumivu yakusukume kuchukua hatua za ziada zaidi.
  22. Zivunje rekodi zako mwenyewe, vunja ukomo uliojiwekea, sehemu ambazo uliona huweza kuzifikia dhamiria kuzifikia hata kama ni kwa maumivu makali, utajiona mwenye furaha sana utakapofikia matumizi makubwa ya uwezo wako.
  23. Ondoa kabisa ukomo unaoletwa na mwili wako, hata kama mwili wako unakuomba upumzike au uache jambo muhimu unalolifanya kwasababu ya maumivu au uchovu, usikubali, ufanye mwili wako uwe sehemu kubwa ya kukulea mafanikio makubwa unayoyatamani.
  24. Usikubali mwili wako uwe kikwazo cha wewe kufikia ndoto zako, dhibiti hisia za mwili wako na ulazimishe mwili wako kufuata ratiba yako muhimu.
  25. Kabiliana vikali na hisia za uchovu na raha ambazo mwili unataka uzifuate ili uache kufanya mambo muhimu kwenye maisha yako. kabiliana vikali sana dhidi ya comfort zone.
  26. Mwandishi anaseama, alipoteza fedha nyingi, muda mwingi, na masaa mengi ya kulala alipokuwa anapambana kusimamisha biashara yake ya virutubisho, lakini hakukata tama hata siku moja.
  27. Mafanikio tunayoyataka kwenye maisha yetu yatatugharimu vingi sana, hvvyo ili kuyafikia hatutakiwi kuwa bianadamu wa kawaida, tunatakiwa kuwa wavulivu sana na kujifunza kwenye kila mabaya na mazuri yanayokuja.
  28. Bare anakiri kufanya makosa mengi sana kwenye safari yake ya mafanikio. Lakini anasema kwa kiasi kikubwa makosa hayo yalimfanya awe imara na kuongeza umakini kwenye kazi zake.
  29. Bare anasema, dhambi kubwa sio kufanya makosa, bali dhambi kubwa ni kufanya makosa na kutojifunza kutokana na makosa hayo.
  30. Makosa ni kiashiria kuwa kuna vitu unavifanya kwenye maisha yako, sehemu yenye usalama hakuna ukuaji, hakuna mapinduzi ya kweli hakuna mabadiliko.
  31. Watu wengi wanaona jambo zuri au kitu kizuri na kuishia kusema “natamani” ningefanya kama vile ili kuwa kama yeye, mwandishi anasema ondoa natamani au wish, fanya kazi inayohitajika kufika unayoyatamani kwenye maisha yako.
  32. Weka matendo kwenye matamanio yako, hakuna kitakachotokea kwa kuishia kutamani pekee. Wekeza nguvu, umakini na akili zako kwenye kufanyia kazi yale unayoyotamani kwenye maisha yako.
  33. Kama kweli una dhamira ya dhati kufikia mafanikio makubwa, basi unatakiwa kuachana na mambo yasio na tija kwenye maisha yako, weka kando kabisha mambo yote yasiyochangia ukuaji wako, au mafanikio yako.
  34. Watu wenye mafanikio wanaona mwanga na furaha kubwa iliyopo mbele ya changamoto wanazopitia. Hii ndio huwafanya wawe wavumilivu kukabiliana na changamoto wanazokuna nazo.
  35. Nick Bare anasema katika shule ya kijeshi alijifunza mambo magumu sana, alipitia nyikati nyingi ngumu na za giza ambazo zilimfanya imara sana. Mafunzo hayo aliyojifunza akiwa jeshini ndaio kwa kiashi kikubwa anayatumia katika kufanya jambo lolote hata kuanzisha kampuni yake ya Virutubisho.
  36. Kikubwa alijifunza nidhamu, bila nidhamu huwezi kukamilisha jambo lolote. Wengi wanashindwa kufanya makubwa kwenye maisha yao kwa sababu hawana nidhamu ya kuvumilia na kukaa kwenye jambo wanalolifanya ili likamilike.
  37. Nidhamu itakufanya kukabiliana na kuishi kwenye nyakati ngumu na kufanyia kazi malengo yako, nidhamu itakufikisha kwenye kilele cha ndoto zako.
  38. Mwandishi wa kitabu hiki anashuri tujifunze kama mashine. Anasema jigeuze uwe kama mashine linapokuja suala la kujifunza na kujiongeze maarifa.
  39. Hakuna kitu muhimu kwenye maisha yetu kama muda. Muda ndio huamua mafanikio yetu, muda ukishaenda hauudi tena. Muda ni maisha. Utumie vizuri kufanya yale muhimu kwenye maisha yako.
  40. Ili uwe na matumizi mazuri ya muda wako jifunze kuweka vipaumbele. Vipaumbele ndio vitakufanya utumie muda wako vizuri na kwa ufanisi mkubwa.
  41. Mwandishi anasema kwenye jambo lolote unalotaka kufanya kwenye maisha yako, kuna taarifa nyingi kuhusu jambo hilo kwenye mitandao kama google, youtube, nk. hivyo usiogope kuanza kwasababu ya kukosa taarifa.
  42. Bare anasema hana tabia ya kuhaika kuwatafuta watu hovyo ili kuuliza mawali au kuomba ushauri. Anasema kabla ya kufanya hivyo huwa anaingia kwenye mitandao na kuanza kutafuta taarifa za jambo hilo kwanza.
  43. Mwandishi Bare anasema, tunatakiwa kufaidika na fursa zilizopo mtandaoni za kujifunza, anasema kuna mitandao mingi sana ya kijamii kwa ajili ya jambo lolote lile, itumie kusaidie, mfano wa mitandao hiyo ni websites, podcasts, books, blogs, vlogs, YouTube.
  44. Kwa kujifunza utaokoa gharama kubwa sana unazaoweza kuingia, tafuta taarifa za awali wewe mwenyewe kwanza. Jipe Jukumu la kujielimisha ili uondoe mambo ambayo huyajui kuhusu kazi yako, biashara yako, afya yako, au fedha.
  45. Kujifunza ni uwekezaji muhimu sana kwako binafsi, wekeza kwenye kujifunza na kupata maarifa ya kutosha kuhusu jambo unalotaka kulifanya.
  46. Bare anasema kipndi akiwa katika mafunzo ya kijeshi huko Korea, alitumia muda wake wa ziada kujifunza sana namna ya kutengeneza kampuni, namna ya kutengeneza videos nzuri, namna ya kuchukua video, kuongea na kufundisha.
  47. Tumia muda wako wa ziada kujifunza sana, jua sana kila unachokifanya, kuwa na taarifa za kutosha kuhusu jambo hilo. Wekeza kwenye maarifa, jifunze kila siku kama mashine.
  48. Kuna maarifa bora sana katika kipindi hiki kuliko nyakati zote zilizowahi kupita hapa duniani. Bare anasema kipindi cha zamani watu walikuwa wanatunza na kuhifadhi taarifa kama dhahabu, lakini zama hizi mambo ni tofauti kabisa kila mtu anaweza kuwa na taarifa anazozitaka.
  49. Jilazimisha sana kupata maarifa, tengeneza kiu kali ya kujifunza, na kwa kufanya hivyo utakuwa mtu bora sana.
  50. Jua kwa hakika ni taarifa gani unazihitaji, na ukianza kuzitafuta zingatia hilo, usiwe mzururaji, na hujui unatafuta taarifa gani, usije kupoteza muda wako wa thamani.
  51. Maisha sio kitufe fulani unajibonyezea tu na mambo yanaenda, maisha sio hisia hisia fulani tu. Maisha yanataka kujitoa sana, maisha yanataka kazi kweli kweli, maisha hayataki njia za mkato. Maisha yanataka ufanye vitu, ufanye kazi ili mambo yatokee.
  52. Kuna watu wanahisia kwamba kwajinsi walivyo au kwa namna walivyo basi wanastahili kutunukiwa mambo mazuri kwenye maisha yao.
  53. Hakuna anayejali kuhusu wewe, hakuna anayekosa usingizi kutokana na shida zako. Hivyo amka pambana na ndoto zako umiliki maisha mazuri unayoyataka.
  54. Acha kuwa na mategemeo kuwa kwasababu upo mahali fulani, au uko na mtu fulani basi utakuwa na maisha mazuri au unastahili maisha mazuri. Fanyia kazi ndoto zako zinazokunyima usingizi, furaha na amani.
  55. Hakuna atakayekuja na furushi la fedha au dhahbu akupe akwambie,unajua wewe ni mtu mzuri sana au wewe ni mpole au mwema sana basi chukua hizi fedha kama zawadi, jambo hili haliwezi kutokea kwako; mambo mazuri hayaji usipojisukuma fanya kazi kubwa kufikia mafanikio unayoyataka.
  56. Kuna wengine wameridhika na vyeo walivyo navyo na kujiona wameshapata kila kitu. Hivyo wanakuwa na kiburi hawataki kujituma tena, wanaona wamefika. Mwandishi anasema hakuna kitu kibaya kama kupata cheo na kujisahau na kuacha kutumia uwezo wako kufanya mambo makubwa.
  57. Mwandishi anasema kuna wakati anaona hajapata kile anachokitaka, anachofanya ni kuwafikiria wale walio na kitu hicho na gharama kubwa walioingia kupata kitu hicho. Kwa kufikiria hivyo anajisukuma zaidi kufanyia kazi malengo yake.
  58. Kama umeshindwa kuzalisha fedha mwaka huu unatakiwa kujiuliza tatizo ni nini? Nini hukufanya, nini ambacho unatakiwa kufanya ili uzalishe fedha unazotakiwa kuwa nazo.
  59. Jua huna wa kumlaumu kwa umasikini wako, kukosa fedha, kazi au maisha mazuri unayoyataka. Jipe Jukumu la kutengeneza maisha yako yawe bora, acha lawama na uvivu.
  60. Jiondoe kwenye comfort zone, ondoka kabisa kwenye maisha ya usalama. Ingia kwenye mapambano, kuondoa umasikini na ujinga kwenye maisha yako.
  61. Kuondoka kwenye comfort zone ni kufanya zaidi ya hisia za mwili wako, hata kama unahisi umechoka au maumivu, hata kama itakugharimu upoteze masaa mengi ya usingizi, itakugharimu kuacha baadhi ya ratiba za kula, itakugharimu kuacha na marafiki wasio na mchango maishani mwako.
  62. Kuondoka kwenye comfort zone, ni kuweka nidhamu kali sana ili ukamilisha jambo unalolifanya hata kama huna hamu au hamasa ya kufanya jambo hilo.
  63. Kuondoka kwenye comfort zone ni kuacha kutoa sababu kwanini hujafanya jambo ambalo ulitakiwa kulifanya.
  64. Kuondoka kwenye comfort zone, ni kujisukuma isivyo kawaida katika kutumia uwezo wako wote kufikia ndoto zako na mafanikio unayoyatamani.
  65. Kuondoka kwenye comfort zone, ni kuacha kujihurumia, kuwa mtu wa matokeo, kuwa mtu wa matendo kuliko maneno pekee.
  66. Kuondoka kwenye comfort zone, maana yake ni kuachana na raha za muda mfupi kwa ajili ya kuwekeza nguvu zako zote kujenga maisha yako ya sasa na ya baadaye yawe bora.
  67. Kuondoka kwenye comfort zone, ni kuanzisha biashara, kuipambania na kuwa tayari kupokea changamoto zote bila kukata tamaa.
  68. Bila nidhamu hutawaweza kujitoa kikamilifu kufanyia kazi ndoto zako. Hutakuwa na umakini hutakuwa na muda wa kufanya mambo muhimu.
  69. Unapofanya jambo lolote lililopo kwenye ratiba yako, lifanye kwa nguvu zako zote, akili yako yote, hisia zako zote. Nenda mzima mzima kulifanya jambo hilo.
  70. Usifanye jambo huku nusu ya akili yako ipo kwenye mambo mengine, unapojitoa jitoe kweli na sio nusu nusu. Zamia kabisa hadi jambo unalolifanya liishe.
  71. Toa asilimia 100 za umakini wako, akili yako, nguvu zako, kwa kufanya hivyo utazalisha kazi bora, na ufanisi wako utakuwa wa Kiwango cha juu sana.
  72. Unapjitoa asilimia 100 kwenye kufanya jambo lolote, maana yake utakuwa na wakati mzuri wa kutumia uwezo wako wa zaida uliolala, ubunifu wako na nguvu zako zilizolala ambazo hukujua kama unazo.
  73. Usikubaliane na ukomo uliojiwekea kwamba ndio mwisho wako hapo. Usikubaliane na maoni ya watu walioweka ukomo kwenye uwezo wako. Hapa una jambo kubwa la kuwahahikishia kuwa hawakuwa sahihi kukuwekea ukomo kwenye maisha yako.
  74. Weka jitihadi za ziada kuwenda mbali kabisa na ukomo uliojiwekea na waliokuwekea watu wengine. Wewe una uwezo wote wa kufanya makubwa na kufanikiwa kwa viwango vya juu sana.
  75. Kila siku inayokuja kwenye maisha yako, hakikisha unaishinda siku hiyo, hakikisha unapata ushindi, usiache siku hiyo ikushinde. Maana yake fanya yote muhimu uliyoyapanga kuyafanya ndani ya siku hiyo.

Asante kwa kusoma uchambuzi wa kitabu hiki, mshirikishe na mwingine maarifa haya.

@Hillary Mrosso_09.09.2022


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X