Aina Tatu Za Ujuzi Unaohitaji Ili Kuongeza Thamani Yako Na Kula Mema Ya Nchi


Kwenye hii makala ningependa tuongelee aina tatu za ujuzi ambao ukiwa nao kwenye hizi zama ni wazi kuwa unaenda kufanya vizuri na hata kuweza kufikia viwango vikubwa na vya hali ya juu sana kuliko unavyotegemea. Najua umewahi kushauriwa kujifunza aina nyingi za ujuzi, ila kwenye aina hizo zote za ujuzi ambao umewahi kushauriwa kuwa nao, hapa kuna aina tatu tu za ujuzi ambapo ukiwa na ujuzi mmojawapo ni wazi kuwa utaweza kufika mbali na hata kufanya makubwa zaidi.

Kama umewahi kusikia kuwa kuna watu wanakula mema ya nchi, basi kwa aina hizi za ujuzi ambao utajifunza hapa, ukiweza kuzifanyia kazi vizuri, ni wazi kuwa na wewe lazima tu utaenda kula mema ya nchi. Nadhani mpaka hapo umenielewa vizuri. Sasa aina zenyewe za ujuzi hizi hapa:

Ujuzi wa kwanza ni ujuzi wa uandishi.

Na hapa siyo tu kuandika, bali kuandika ilimradi umeandika, bali kuandika andiko ambalo linavutia na linashawishi watu kusoma na hata andiko ambalo linasukuma watu kutoa fedha mfukoni na kukulipa wewe.

Lakini ngoja kwanza tujiulize hili swali la muhimu

Uandishi Ni Kitu Gani?

Uandishi ni ujuzi wa kuwasilisha mawazo kwa watu kwa lengo la kuhamasisha, kuelemisha, kuburudisha, kuchekesha au lengo lolote lile analokusudia mwandishi. 

Uandishi umebaki kuwa ni ujuzi muhimu sana kwenye uliwengu wa leo. Mbali na kuwa sasa hivi kuna watu wanapenda kuangalia video kwenye mitandao inayoonesha video kama youtube na tiktok, au picha kwenye mitandao ya picha kama instagram, ila ukweli ni kwamba, uandishi unabaki kuwa moja ya ujuzi muhimu sana kwenye zama za leo. Uandishi haujachuja na pengine ni ujuzi ambao unaweza kukutoa wewe hapo.

Zama Zimebadilika

Kwanza nipende kutangulia kwa kusema kwamba tunaishi kwenye ulimwengu ambao umebadilika sana. Yes sure, ulimwengu wa sasa umebadiika sana kuliko ilivyokuwa zamani. Kuna kipindi ambacho watu walikuwa wanawinda kwa ajili ya kupata chakula.

Baadaye kikaja kipindi ambapo watu walikuwa wanalima kupata chakula, na tena baadaye kikaja kipindi ambapo watu walikuwa wanafanya kazi viwandani kwa ajili ya mshahara ambao ungetumika kununu chakula. Ulimwengu wa sasa hivi umehamia mtandaoni. Na hata unasoma makala hii mtandaoni.

Uandishi umebaki kuwa mfalme kwenye ulimwengu huu wa mtandao. Kwa hiyo hizi picha zinazosambaa mtandaoni na kuvuma, hazisambai tu kwa ajili ya kusambaa, nyingi zinazosamba, utakuta kwamba zina maneno fulani, hata kama maneno kidogo. na hayo maneno yanaandikwa au kuandaliwa na mtu mwenye uelewa mzuri wa uandishi. Kwa hiyo vitu kama nukuu au maandishi mengine yanayosambaa kwa kasi, niseme pia ni sehemu ya uandishi. Ukiujua uandishi vizuri vitu vingine vidogo havitakuhangaisha.

Uandishi ni ujuzi wa karne ya 21

Ukiwa vizuri kwenye uandishi, hutakaa uhofie uwepo wa vitu vingine kama mitandao ya picha au video kwa sababu, huku kama mwandishi bado unafit vizuri tu.

Kwa mfano, unaweza kuandika andiko lako, na kulisoma kwa sauti au hata kuligeuza kwenye video kwa kuongeza picha na vitu mbalimbali. kwa hiyo ukajikuta kwamba unafanya vizuri kwenye ulimwengu wa uandishi lakini pia unafanya vizuri kwenye ulimwengu wa sauti na video pia.

Kwenye ulimwengu wa leo baadhi ya taaluma zinachukuliwa na mashine. Kwa mfano, taaluma ya ukarani inachukuliwa na mashine, sasa hivi kuna roboti ambazo zinaweza kufanya upasuaji, kwa hiyo kama wewe ni daktari, upo hatarini kuondolewa na mashine.

Siku hizi kuna hoteli na migahawa haina wahudumu au zina mhudumu mmoja tu. tangu unafika kwenye hoteli mpaka unatoka, unahudumiwa na mashine tu, kwa hiyo kama wewe ulikuwa ni mhudumu wa hoteli au mgahawa, kazi yako ipo hatarini…..

VIDEO FUPI YA ROBOTI ZINAVYOHUDUMIA WATEJA HII HAPA

Sasa vipi kuhusu uandishi..

Ndio, kuna roboti ambazo zinaandika pia…Hahah

Lakini ni kitu gani kinaufanya uandishi kuwa kitu cha kipekee?

Ni kweli kuna roboti ambazo zinaweza kuandika, lakini hizi roboti haziwezi kuja na kitu original (O.G). Zinaandika kwa kutumia taarifa ambazo zipo mtandaoni kwa sasa. lakini haziwezi kutengeneza kitu cha tofauti ambacho hakijawahi kuwepo…na wala hicho kitu hakitatokea kwa siku za karibuni kwa sababu uandishi ni kitu ambacho kinahusisha hisia pia.

Mwandishi anapokuwa anaandika, kuna hisia fulani hivi anakuwa nazo, kwa hiyo uandishi ni kama sehemu ya kuhamisha zile hisia na kuziweka kwenya maandishi

Mashine hazina uwezo wa kuwa na hisia

Kwa mfano mtu anayeandika juu ya sherehe ya jana iliyofana. Hisia anazokuwa nazo wakati anaandika andiko lake, ni hisia ambazo roboti haiwezi kupata.. hata kama roboti ilikuwepo kwenye sherehe, haiwezi kuwa na hisia hizo…Ebu sema oyooo…

Kwa hiyo hicho kitu kinafanya sasa uandishi uwe wa kipekee na ujuzi ambao unapaswa kuwa nao kwenye karne hii ya 21

Lakini pia kama ambavyo nimekwambia, ukijua uandishi tu, unaweza kwenda mbele na kuhakikisha kwamba, unautumia kwenye maeneno mengine kama mafunzo ya picha, mafunzo ya sauti, video n.k.

Ukiujua uandishi vizuri unaweza kuutumia kwenye mauzo na ukafaa.. unaweza kuhamia kwenye kilimo na ukaandika kitu kinachoeleweka na watu wakakisoma

Unaweza kuandika kuhusu michezo

Unaweza kuhamishia uandishi wako kwenye tasnia ya uigizaji. Yaani, popote pale utakapoenda na ujuzi wako wa uandishi, unakubalika. Hapa ningekuwa naandika kwa kimombo, ningesema the sky is the limit, ila kwa kuwa siandiki kwa lugha hiyo, naacha sisemi. hahaha

Halafu kabla sijasahau, ujue uandishi ni ujuzi ambao ukishaujua,, umeujua!

Kuna ule usemi wa kwamba kama ipo ipo tu… Ni kweli kwamba utapaswa kuendelea kunoa ujuzi wako wa uandishi mara kwa mara. Ila walau kuna kitu kimoja ambacho mimi nina uhakika nacho, uandishi ni kitu ambacho hakiwezi kuondolewa kwako… ukishaujua umeujua na unaweza kukuumia kwenye sekta yoyote ile…

Ufanye uandishi ukutambulishe kwa namna kipekee

Nimesema kwamba zama za sasa zimebadilika, nimesema kwamba uandishi ni kitu pekee ambacho kwa sasa hakitachukuliwa na roboti, lakini pia nataka niseme kwamba, utumie uandishi kukutambulisha na kujenga ujuzi mpya katika namna mbayo hakuna roboti inaweza kufanya kufanya kazi yako.

Ebu fikiria kama wewe ni daktari na tayari roboti zimeshaanza kutibu watu, sasa unaonaje ukiunganisha utalaamu wako na uandishi (idea sexing), hapa uhakika ni kwamba, uandishi unaenda kukutambulisha vizuri sana.

Kumbe kwa kuunganisha uandishi na kitu chochote kile ambacho unajua sasa hivi, utakuwa mtu wa pekee na wa tofauti sana.

Kama wewe ni mhasibu, ukiongeza na uandishi kwenye uhasibu wako, utakuwa umetengeneza kitu kingine cha tofauti.

Kama wewe ni mwalimu, ukiongeza na uandishi, utakuwa umetengeneza kitu kingine cha tofauti kabisa.

Sasa nataka kuanzia leo uanze kuufanyia kazi uandishi. Swali langu kwako unaenda kuwa unaandika kuhusu kitu gani? Ni kitu gani?

Kama mpaka hapo huelewi ni namna gani unaweza kuandika, naomba upate kitabu changu cha JINSI YA KUWA MWANDISHI MBOBEVU. Hiki kitabu kitakufumbua macho kwa namna ambayo hukutegemea kwenye suala zima la uandishi.

Kwenye makala hii nilitaka tu kukuonesha nguvu ya uandishi, na jinsi ambavyo uandishi ni ujuzi muhimu unaopaswa kuwa nao kwenye hizi zama tunazoishi kwa sasa.

Ujuzi wa pili ni UJUZI WA KUUZA

Huu ni ujuzi mwingine muhimu sana. Ujue kwa namna moja au nyingine katika maisha utalazimika kuuza. Ukisimama mbele ya watu kuongea ujue unauza. Ukimshawishi mtu au ukitaka mtu akubali falsafa au hoja yako basi ujue kwamba unakuwa unafanya mauzo, ukitaka kumpata mwenza lazima utatakiwa kufanya mauzo, na hata kama unahubiri bado ni uuzaji, ukitaka mwajiri wako akuongezee mshahara hayo ni mauzo pia.

Kwa hiyo jifunze namna bora ya kuuza ambayo itawafanya watu wanunue unachouza. Jua saikolijia ya watu ili ikusaidie katika aina ya mauzo unayofanya.

Ukiweza kuwa muuzaji mzuri basi ni wazi utaongeza thamani yako kwa viwango vikubwa sana. Ila kama haujui kuuza utalala njaa rafiki rafiki yangu.

Unaweza kushangaa na kujiiuliza hivi kuwa si bora niwe na bidhaa nzuri? Ndio unapaswa kuwa na bidhaa nzuri, ila kama huwezi kuiuza haitasaidia. Bidhaa nzuri bila kujua kuuza vizuri utakaa nayo wewe tu.

Kwenye kitabu cha Rich Dad Poor Dad, mwandishi amesema kwamba kuna siku alikutana na mwandishi mchanga ambaye alikuwa anataka kujua ni kwa jinsi gani anaweza kutengeneza fedha kupitia uandishi.

Kiyosaki akawa amemwambia kwamba anapaswa kujifunza kuuza. Kiyosaki aliendelea kumwambia yule mwandishi mchanga kuwa, mimi sio mwandishi bora ila muuzaji bora. Hata ukichukua kitabu changu, hakuna sehemu utakuta imendikwa kuwa mimi ni mwandishi bora. ila imeandikwa kuwa mimi ni muuzaji bora (bestselling author).

Kwa hiyo kitu kimoja cha kuondoka nacho siku ya leo ni kuwa unapaswa kuhakikisha unajifunza uuzaji.

Uuzaji ndio unaleta fedha kweye biashara na kwenye maisha ya kila siku. Bila kufanya mauzo biashara zinakufa, bidhaa zinakufa, vipaji vinapotea na mengine mengi.

Lakini kinyume chake ni tofauti, ukiweza kufanya mauzo vizuri, maana yake utapata fedha na ukiwa na fedha hakuna kitu ambacho kinaweza kukushinda kufanya. Na mauzo ndiyo yanaleta fedha.

Ukifuatilia vizuri, watu wanaolipwa zaidi hapa duniani siyo watu wengine bali ni watu wa mauzo (salesmen and women). Watu ambao wameujua vizuri ujuzi huu hawalipwi mshahara, bali wanalipwa kwa kamisheni.

Watanzania wengi hawajui malipo ya kamisheni hivyo huwa wanapenda mshahara, ila malipo ya kamisheni ukiyaelewa vizuri, unaweza kumwabia bosi wako leo aache kukulipa kwa mshahara, badala yake akulipe kwa kamisheni.

Unajua kamisheni ipoje, malipo ya kamisheni ni pale ambapo mnakubaliana na mtu uakulipe kulingana na mauzo unayokuwa unafanya. Kadiri unavyoongeza juhudi kubwa zaidi kwenye kuuza na kufanya mauzo zaidi, ndivyo ambavyo unaweza kulipwa zaidi.

Kwa mfano mkkikubaliana kuwa ulipwe kwa kamisheni ya asilimia 5, 10 au 20 malipo yako yatakuwa hivi kwa kila mauzo utakayofanya.

KAMISHENI YA ASILIMIA
Mauzo5%10%20%
10,0005001,0002,000
100,0005,00010,00020,000
1,000,00050,000100,000200,000
10,000,000500,0001,000,0002,000,000
100,000,0005,000,00010,000,00020,000,000

Kwa aina hii ya malipo, ukomo kwenye kulipwa ni wewe mwenyewe. Yaani, wewe ndiye unaweza kuamua ulipwe sana au ulipwe kidogo kwa sababu kadiri unavyokuwa unaweka juhudi kwenye kazi ndivyo ambavyo unalipwa zaidi. hivyo, juhudi zaidi maana yake zinaleta matokeo makubwa zaidi.

Sasa unajifunzaje ujuzi huu. Anza kwa kusoma kitabu cha How I raised myself from failure to success in selling. Hiki kitabu kitakupa mwongozo na mbinu za mauzo ambazo huwezi kuzipata sehemu nyingine.

Ukizutimua mbinu zilizo kwenye hiki kitabu, ni uhakika kuwa utaweza kufika mbali, tuwasiliane kwa songambele.smb@gmail.com ili niweze kukutumia kitabu hiki usome.

Ujuzi wa tatu ni KUNENA

Siku moja kuna kijana alimwuliza Warren Buffet kuwa ni ushauri gani ambao unaweza kuutoa kwa kijana mwenye umri wa miaka 21 au 22 kuhusu mafanikio? Bila kusitasita Warren Buffet alimweleza kuwa ushauri wangu kwa kijana mwenye umri wa miaka 21 au 22 ni kuwa ajifunze na kuelewa kwa undani ujuzi wa kuwasilisha hoja kwa watu, na hii inaweza kuwa ni kwa njia ya maandishi au kuongea.

Kama umegundua kitu, ni kuwa makala hii inajihusisha zaidi na ujuzi huu mmoja wa kuwasilisha hoja zako kwa watu. ila ujuzi huu tumeugawa kwenye aina tatu ndogo za ujuzi ambapo hapa tayari tumeongelea ujuzi wa kuandika, ujuzi wa kuuza na sasa tunaongelea ujuzi wa kunena.

Huu ni ujuzi mwingine ambao unaweza kuongeza kipato mpaka asilimia 50 au hata zaidi.

  • Wanasiasa
  • Wafanyabiashara
  • Wanamichezo na wengine wengi huwa wanatumia huu ujuzi

Huu ni ujuzi wa tatu muhimu sana. Kunena au kama kunavyofahamika kwa kiingereza ni public speaking. Huu ni ujuzi mwingine ambao ukiwa nao utaongeza thamani yako kwa viwango vikubwa sana.

Ni wazi kuwa huwa tunapenda sana watu ambao huwa wanaongea na kutoa hoja zinazovutia. Kuna mtu akisimama kuongea mwili unasisimuka kwa kuona jinsi anavyowasilisha mada yake. Hiki ni kitu ambacho na wewe unaweza kukijua na kukifanyia kazi kwa manufaa yako. Wanasiasa wanatumia sana hiki kitu wakati wa kampeni kwa ajili ya kuomba kura. Wasemaji wa timu za mpira wanatumia ujuzi huu pia kwa ajili ya kuvuta umakini kwenye vyombo vya habari.

Kila siku tunakutana na watu na tukiwa na watu hawa tunaongea, tunawasilisha na kujadili mada, tunacheka na kufurahi

Lakini unahitaji kujifunza kunena. Na kunena ni zaidi ya kuongea. Najua utauliza sasa kunena ni nini? Kwa haraka tu naweza kusema KUNENA ni KUONGEA NA WATU WAKASILIZA.

Sasa kuongea na watu wakusikilize wewe ni kazi. Na sio kazi ndogo. Nadhani imewahi kukutokea  unaanza kumsikiliza mtu ila unagundua kuwa hana pointi za maana. Yaani amesimama mbele yako na wewe unaona wazi kwamba hakuna kitu cha maana anaongea.

Omba isikutokee wewe. Na namna nzuri ya kuomba ni kujifunza uneni kuanzia leo hii

Sasa zifuatazo ni mbinu saba unazoweza kutumia kwa haraka ili kuongeza ujuzi wako wa kunena.

Moja ni kutafuta fursa ya kuongea mbele ya watu, kwa kuanzia unaweza kuanza na hadhira ndogo tu watu wachache pengine hapo hapo nyumbani. Unaweza kuwakusanya ndugu zako wa karibu na kunza kufanya mazoezi mbele yao. Na hata muda mwingine siyo lazima uwaambie.

Kama huwa mnasali pamoja pale nyumbani unaweza kuwashawishi kuongeza na kipengele cha neno la Mungu, halafu kile kipande cha kufafanua neno la Mungu ukakibeba wewe, na ukautumia huo kama muda wako wa kuwasilisha yako na sehemu ya kujifunza uneni.

Lakini pia unaweza kuandaa kikundi cha watu na kuwaeleza kuwa utakuwa unafanya mazoezi ya kuongea mbele yao, hivyo unaomba wakupe mrejesho baada ya kuwa umewasilisha mada yako. Sana sana hawa wawe ni watu ambao wanaweza kukupa mrejeho bila ya kukuogopa.

Pili ni tenga muda wa kufanya mazoezi kwaa ajili ya kunoa ujuzi wako huu. Dakika kumi mpaka thelathini kila siku zitafanya kazi.

Tatu, hakikisha umeandika kwanza hotuba yako, kisha ifanyie mazoezi. Hiki ni kitu kidogo sana ila chenye nguvu kubwa sana. Kanuni muhimu kwenye kufanya mazoezi unayopaswa kuitumia ni kuwa, kama utatakiwa kuongea kwa dakika 12, basi utapaswa kujiandaa kwa  dakika 120 kabla ya kutoa hotuba yako.

Nne, jifunze kwa kusoma vitabu. hiki kitu kitakufanya uongeze maarifa na kuielewa mada husika kwa undani, hivyo utaweza kuwasilisha mada yako huku ukiwa na uelewa mkubwa zaidi. Kadiri unavyosoma ndivyo unavyojua zaidi na watu wanapenda kusikiliza mtu mwenye kitu cha kusema na kadiri watu wengi wataavyokuwa tayari kukaa chini na kukusikiliza, ndivyo ambavyo kipato chako kitakuwa kinaongezeka zaidi.

Tano ukiwa kwenye kikundi cha watu, chagua mtu mmoja ambaye utakuwa unamwagalia wakati unaongea. Ujue ni muhimu sana kuangalia watu wakati uhnatoa hotuba yako, sasa ukianza kuongea mbele ya watu, kama unaogopa kuwaangalia watu, chagua mtu mmoja ambaye utamwangalia na kisha unaweza kuhama kutoka kwake na kuwangalia mwingne kadiri muda unavyoendelea.

USHAURI WANGU: Chagua aina moja ya ujuzi ambao unaweza kuanza kuufanyia kazi leo.

Usianze na kila ujuzi. Anza na ujuzi mmoja, ufikishe kwenye viwango vikubwa. Kisha kuza ujuzi mwingine. Mwisho wa siku utajikuta umeweza kujenga kila ujuzi.

Rafiki yangu hizo ndizo aina tatu za ujuzi ambao unapaswa kuwa nao.


One response to “Aina Tatu Za Ujuzi Unaohitaji Ili Kuongeza Thamani Yako Na Kula Mema Ya Nchi”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X