Deprecated: Constant FILTER_SANITIZE_STRING is deprecated in /home/songambele/public_html/wp-content/plugins/blogger-to-wordpress-redirection old/b2w-redirection.php on line 91
Uchambuzi Wa Kitabu: How To Stop Worrying and Start Living - SONGA MBELE

Uchambuzi Wa Kitabu: How To Stop Worrying and Start Living


NB: kusikiliza makala hii kwa njia ya sauti. Bonyeza hapa

Kitabu: How To Stop Worrying and Start Living

Mwandishi: Dale Carnegie

Mchambuzi: Hillary Mrosso

Simu: +255 683 862 481

Utangulizi

Jina la kitabu hiki lenye maana ya Namna ya kuachana na hofu na kuanza kuishi. Ni kitabu bora sana kinachoelezea namna ya kukabiliana na hofu kwenye maisha yetu ya kila siku. Hofu imewalaza wengi katika vitanda vya hosipitali, hofu imewanyang’anya wengi afya, furaha, amani, utajiri, na fedha nk. Mwandishi wa kitabu hiki ametumia muda mwigi sana kufanya utafiti wa kina kwenye maisha ya watu wengi waliopitia nyakati ngumu zilizotawaliwa na hofu na kupata maoni yao na ndio kwa kiasi kikubwa yametumika katika uandishi wa kitabu hiki. Hiki ni moja ya vitabu bora sana kwa binadamu yoyote, hupaswi kabisa kukosa kusoma kitabu hiki, ni kama dawa na kinga endapo utayatumia yaliyoandikwa humu kukutoa kwenye aina zote za hofu ulizo nazo. Karibu kwenye uchambuzi huu muhimu.

1. Kitabu hiki kinawafaa zaidi wale ambao wapo tayari kutekeleza yaliyoandikwa katika kitabu hiki, hii ndio faida na lengo la uandishi wa kitabu hiki, sio kwa ajili ya kujifurahisha na kufurahia namna kilivyoandikwa, ni kitabu kinachodai zaidi utekelezaji.

2. Mwandishi wa kitabu hiki anasema, soma kurasa 40 za mwanzo za kitabu hiki, na endapo hutapata chochote cha kukusaidia kukabiliana na hofu ulizo nazo, basi, unachotakiwa kufanya ni kukitupa au kukichoma kitabu hiki.

3. Maisha yetu ya baadaye yatakuwa bora kwa kufanya yale yaliyopo kwenye siku yetu ya leo, usifanye mambo ya kesho leo wala usifanye mambo ya jana kesho, wekeza kwenye kufanya yaliyopo kwenye siku yako.

4. Mwandishi Dale Carnegie anasema tukumbuke moja ya maombi ambayo Yesu Kristo aliwafundisha wanafunzi wake, aliwaambia waombe mkate wa siku, na sio mkate wa kesho au jana, au mwezi ujao.

5. Mkate wa siku hiyo ndio wa muhimu zaidi, maana yake kila siku ina mambo yake, huenda kesho usihitaji mkate ukahitaji kitu kingine, Mungu anakupa kile unachokihitaji sasa, yaani leo na sio unachokihitaji kesho au jana.

6. Katika moja ya mafunzo muhimu Yesu Kristo aliyowafundisha wanafunzi wake ni kuacha kujisumbua au kuhangaika kwa ajili ya mambo ya kesho, aliwaambia iacheni kesho ijisumbukie yenyewe.

7. Usighairishe mambo ya leo kwa kuhofia utaishije kesho, kesho ina mambo mengi na kuna mengi hutaweza kuyathibiti hivyo wekeza nguvu zako kufanya yale yaliyomo mbele yako, mbele ya siku yako, hii ndio njia nzuri ya kuondoa hofu kwenye maisha yako.

8. Kuwa na mawazo mazuri kuhusu siku yako, itakufanya uipangilie na kufanya yote kwa ufanisi, mawazo mabaya yanaleta hofu na msongo wa mawazo ambao hupelekea kuairisha mambo muhimu ka kuhofia mambo usiyoyajua na usiyo na ukakika nayo.

9. Ili maisha yetu yawe bora, tunahitaji siku moja bora, ili tuweze kufanya yote yaliyo bora kwenye siku hiyo. Siku zote jifunze jambo hilo, unahitaji siku moja tu.

10. Andika hii sentensi kwenye karatasi na uibandike ofisini kwako au nyumbani kuwa, unahitaji siku moja tu kufanya makubwa. Siku moja, ukiipata siku hii moja fanya makubwa na ya muhimu kwenye siku hiyo.

11. Fanya jambo moja kwa wakati, hatua moja kwa wakati hii dhana itakusaidia sana kuwa mwenye ufanisi unapofanya mambo muhimu kwenye siku yako.

12. Epuka kuwa na mrundikano wa mawazo, au majukumu mengi ndani ya siku yako, maana hayo yatakufanya ushindwe kuianza siku yako kwa ushindi na pia yanaweza kukukatisha tamaa na utaishia kuchanganyikiwa na kukosa cha kufanya hii itapelekea uanze kuwa na hofu.

13. Ukweli ni kwamba nusu ya vitanda vya hosipitalini vimetengwa kwa ajili ya wagonjwa hofu, ambao neva za miili yao zimeharibika kwa hofu waliyoitengeneza kwenye maisha yao kwa kuhofia mambo ya jana na kuwa na mashaka na kesho wasiyoijua.

14. Panga kuishi maisha yako kikamilifu ndani ya siku moja, achana na usiyoyajua kuhusu kesho, achana na kujibebesha mizigo ya mambo yaliyokwisha kupita.

15. Jifanyie wepesi kwenye maisha yako, amua kuishi maisha marefu kwa kuondoa hofu kwenye maisha yako, hofu inafupisha sana siku zako za kuishi, inakufanya uonekane mnyonge muda wote hofu ni mbaya jamani.

16. Hadi unapofikia wakati wa kulala usibebe mzingo wowote wa madeni, hofu, chuki, uchungu, hasira kwnda nao kitandani, achilia, samehe, na ingia kitandani ukiwa mwepesi na ukilala usingizi wako utakuwa kama wa mtoto mchanga.

17. Jikumbushe kila siku unapoianza siku yako, jiambie maneno haya, “wacha niishi siku hii moja tu vizuri”, jiambie hivyo kila siku. Kwa kufanya hivyo utawekeza nguvu zako zote kwenye kuifanya siku yako kuwa bora sana, na hatimaye maisha yako ya sasa na ya baadaye yatakuwa bora.

18. Moja ya asili ya binadamu ni kughairisha kuishi, na kuanza kufikiria vitu ambavyo hata havipo kabisa, wengi wanaghairisha furaha, amani, upendo au mambo muhimu yaliyopo mbele yao na kuanza kufikiria vitu ambavyo hata havipo.

19. Maisha ni yako, shughulika na yako, acha kutoroka maisha yako, maisha yako ni jukumu lako, yafanye maisha yako kuwa yenye furaha, amani na upendo wakati wote, uwezo huo unao.

20. Mambo ya leo ndio muhimu, usiache kuishi sasa na kuanza kutatua matatizo ya kesho ambayo hujui itakujaje.

21. Ifurahie siku yako, na panga kufanya makubwa uwezavyo ndani ya siku hiyo, Carpe diem. “Enjoy the day.” 

22. Fanya kama mtunga zaburi aliyosema, Hii ndio siku aliyoifanya Bwana, tutaifurahia na kuishangilia. Hakusema hizi ndizo siku, au hii ndio kesho au jana aliyoifanya Bwana, alisema hii ndio SIKU aliyoifanya Bwana.

23. Unapoamua kukabiliana na hofu zilizoko kwenye maisha yako, jiambie bila kuogopa, na agalia hali zote unazoweza kukabiliana na hofu hizo bila kujali. Unaweza kujiambia endapo nitafanya jambo hili ninalolihofia nitaenda jela? Au nitakufa?

24. Pambanua kwa undani bila mashaka yoyote endapo utafanya unachohofia, ni kitu gani kibaya sana kitatokea kwenye maisha yako, ni kifo, au utaenda jela au ni nini kitatokea, ukiona hakuna kibaya basi acha kuogopa na ufanye jambo hilo.

25. Unapodhamiria kufanya jambo muhimu kwenye maisha yako usiache hofu zikakuzuia kufanya, jifanyie tathimini fupi ya faida na hasara kisha chukua hatua sahihi.

26. Mara kwa mara jiulize swali, kuna faida gani kwenye haya ninayoyaogopa? Hii hofu inanisaidia nini? Fikiria na chukua hatua mara moja uachane na hofu zinazokusumbua.

27. Hofu inadumaza na kutufanya tushindwe kuchukua hatua kwenye maisha yetu, hofu zinaturudisha sana nyuma, amua kuondoka kwenye hofu uishi maisha yenye furaha na afya tele.

28. Hofu nyingi tulizonazo zitapungua endapo tutajua uhalisia wa jambo na kukubaliana na matokeo yake. Wengi wamelimbikiza hofu zinazowaua taratibu kwa kushindwa kukubaliana na uhalisia wa mambo.

29. Usipokuwa tayari kukubaliana na uhalisia ulivyo, siku zote utaishi kwenye hofu, mashaka, hasira, chuki na magojwa yatakuandama.

30. Wachina wana msemo wao wa ajabu sana, wanasema amani ya moyo unaipata pale unapokubaliana na yaliyokwisha kutokea. Kama mambo yameshatokea huna unachoweza kufanya tena zaidi ya kukubaliana na matokeo yake.

31. Wengi wameingia kwenye hofu kwasababu wameshindwa kukubali matokeo, na wanatumia muda mwingi, nguvu, na hisia zao kufikiria mambo yaliyopita. Hii ikiendelea ilaleta hofu, uchungu na hasira.

32. Kubaliana na mabaya yaliyokwishatokea au ambayo hayajatokea, hii inatakufanya uishi kwa amani, tegemea mabaya yanaweza kutokea kwako au kwa mtu mwingine, hivyo usiogope maana kwa kuogopa au kuwa na hofu hutabadili chochote.

33. Namna nzuri ya kukabiliana na kupanda au kushuka kwa sukari mwilini mwako ni kuwa tayari kuyapokea yote yatakayokuja kwenye maisha yako, haijalishi ni mazuri au ni mabaya, yapokee kama yalivyo, kwa kufanya hivyo utalinda afya yako na mwili wako.

34. Kama wewe ni mfanyabiashara na hujui kupambana na hofu, unaweza kufa mapema. Kwenye biashara kuna mengi yasiyotarajiwa, hata ujiandae vipi, lazima kuna mengine yatakuja tu kukushangaza, hivyo kama wewe ni mtu wa hofu unaweza usifanikiwe na ukafa mapema.

35. Mwandishi Dale anasema, asilimia 70 ya wagonjwa wanaoenda kumuona daktari wanaweza kupona maradhi na magonjwa yao endapo watakaa mbali na hofu na mashaka.

36. Hofu na mashaka zinafanya mfumo wa neva za miili yetu kushindwa kufanya kazi vizuri, hivyo kupelekea madhara kwenye mfumo wa umeng’enyaji wa chakula na kusababisha neva za tumbo kupeleka taarifa za uzalishaji mwingi wa acidi ambazo huleta madhara kama vidonda ya tumbo.

37. Mwandishi anasema, taarifa za kitabibu zinaonyesha wengi wenye vidonda vya tumbo ni kwasababu ya hofu na mashaka waliyo nayo kwenye maisha yao. Hivyo wengi wanaweza kupona au kutoingia kwenye madhara ya kupata magonjwa hayo kwa kuziepuka hofu.

38. Hofu pia zinazalisha msongo wa mawazo ambao pia una madhara kwenye mwili wa binadamu kama vile kusababisha vidonda vya tumbo.

39. Daktari Joseph Montague anasema, hatupati vidonda vya tumbo kwa vyakula tunavyokula, tunapata vidonda vya tumbo kwa vile vinavyotula. Anamaanisha sio aina ya vyakula ndio huleta vidonda vya tumbo, bali vidonda vya tumbo vinatokana na vile vinavyotula.

40. Utafiti wa gazeti la Life magazine nchini Marekani unaonyesha kuwa, hofu, mashaka, uchoyo uliopitiliza, chuki na kushindwa kukubaliana na uhalisia wa mambo vimekuwa ndio chanzo kikuu cha vidonda vya tumbo, na vidonda vya tumbo vinaripotiwa kuwa moja ya janga kubwa linaliua watu watu duniani.

41. Madakari bingwa kutoka katika kitengo cha hosipitali ya Mayo nchini Marekani wanasema nusu ya vitanda vya hosipitali vimejaa wagonjwa ambao wana matatizo ya neva. Matatizo ya neva huathiri utendaji kazi wa sehemu kubwa ya mwili, na kwa kiasi kikubwa husababishwa na hofu.

42. Matatizo hayo ya neva sio kwamba yanasababishwa na neva kuharibika kutokana na michubuko ya nje, bali ni kutokana na hisia za kuchanganyikiwa, hofu, huzuni, hasira, kushindwa na kukata tamaa.

43. Mwanafalsafa maarufu sana duniani Plato aliwahi kusema, madaktari wanakosea sana pale wanapojaribu kutibu mwili bila kutibu nafsi, ambayo imebeba hisia zote za mtu kama vile hisia za chuki, furaha, hasira, hofu nk. Huweze kutengenisha kutibu mwili pekee bila kutibu na eneo lake muhimu la hisiaa.

44. Ni ukweli sayani ya utabibu imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kutibu na kuondoa kabisa magonjwa mabaya kwa binadamu kama vile, surua, pepopunda, kipindupindu, ugonjwa wa manjano, malaria nk. Ambayo yalipeleka watu wengi kaburini.

45. Hata hivyo, sayansi ya udakatri bado inakabiliwa na changamoto sana katika kutatua changamoto za magojwa ya kiakili, hisia, hofu, chuki, na msongo wa mawazo ambayo kwa kiasi kikubwa yanawasumbua sana watu wengi.

46. Taarifa za kitabibu kutoka nchini Marekeni zinaonyesha kuwa mtu mmoja kati ya watu 20 anatatizo la kiakili, ambalo limechangiwa na msongo wa mawazo na hofu.

47. Tafiti nyingine kuhusu afya ya akili zinaonyesha mtu mmoja kati ya sita walioitwa kwa ajili ya kushiriki kwenye vita ya pili ya dunia alikataliwa kutokana na matatizo ya kiakili. Matatizo haya ya kiakili kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na hisia za hofu na mashaka

48. Kama unakabiliwa na nyakati ngumu kwenye maisha yako, ushauri ni kwamba usichukue nyakati ngumu ukazipeleka kwenye mfumo wako wa upumuaji au hisia, ukifanya hivyo utafupisha maisha yako.

49. Utafiti wa Dkt. Wiliamu McGonigle kutoka taasisi ya meno nchini Marekani unaonyesha kuwa hofu na mashaka yanasababisha meno kuoza, hii ni kutokana na hisia mbaya za hofu na mashaka zina haribu uwiano wa mfumo wa madini ya Calciam mwilini na hivyo kusababisha meno kuoza.

50. Hofu inaharibu hata mwonekano wako wa nje, hofu inaweza kukujengea muonekano usiovutia kabisa, ukaonekana wa ajabu, ukaonekana mzee kumbe ni kijana.

51. Hakuna kitu kinaharibu mwonekano wako wa nje haraka kama hofu, mwonekano wako wa nje una maana sana kwenye maisha yako, hivyo usikubali uharibiwe kwa hofu.

52. Hofu inakufanya ujioni mkosaji, hufai, hustahili na inakufanya ujione unaonewa, hofu inakujengea picha na taswira ambazo hazina uhalisia wowote.

53. Ukiruhusu tu hofu kwenye maisha yako, ujue umeruhusu pia majirani zake wa karibu ambao ni vidonda vya tumbo na matatizo ya moyo kama shinikizo la damu nk.

54. Hofu inaharibu nywele zako, zinaweza kupoteza rangi yake ya asili, hofu inaweza kufanya hata nywele zako za kichwani kupotea au kushindwa kuota.

55. Hofu inaweza kukuletea magonjwa ya ngozi, inaweza kubadili hata rangi ya ngozi ya mwili wako, inafanya ngozi kusinyaa na kusababisha vipele majipu na muwasho.

56. Unapokuwa na hofu huwezi kuzalisha chochote, zaidi sana utajiletea madhara makubwa yatakayokugharimu uhai, kama vile magonjwa ya moyo na vidonda vya tumbo.

57. Hofu ni kama dripu za maji ya matone, ukiiruhusu inakutafuna hadi unaishia kujiua au kukufanya kuwa kichaa. Usiruhusu hofu kwenye maisha yako.

58. Changamka na uwe mtu wa furaha, hii itaongeza kinga za mwili wako na kuimarisha afya ya mifupa yako, kumbuka mifupa yako inaweza kuharibika kwasababu ya hofu, hivyo ukaishia kupata kansa.

59. Mwandishi Dale Carnegie anasema nusu ya majanga ya hofu yanayowapata watu ni kwasababu wanafanya maamuzi bila kuwa na taarifa za kutosha kuhusu jambo fulani.

60. Tafuta taarifa za kweli kuhusu kinachokutia hofu, kwa kufanya hivyo utakuwa umetatua sehemu kubwa ya tatizo linalokusibu.

61. Kuwa na utaratibu wako wa kuandika kila changamoto unayoipitia, pia ainisha njia utakazotumia kukabiliana na hiyo changamoto, fikiria unachoweza kufanya kuitatua changamoto hiyo na kisha chukua hatua mara moja.

62. Jinsi unavyojikita kwenye kufanya majukumu yako kila siku ndivyo unavyoachana na hofu. Hofu inatabia ya kumtawala na kumtesa mtu ambaye hana cha kufanya kutwa nzima amekaa tu au amelala tu bila kufanya jambo lolote.

63. Mfano, kama unasumbuliwa na hofu sana, nenda shambani, tengeneza bustani, nenda kwenye mazoezi, au nenda ukacheze mziki hii itakufanya uache kuwaza kuhusu hofu, (occupational therapy).

64. Tafuta wastani wa jambo unaloliogopa kwamba litatokea kwenye maisha yako, mfano kama unaogopa kusafiri kwasababu kuna ajali, basi tafuta wastani wa magari yote yanayosafiri kisha angalia yanayopata ajali ni mangapi angalia wastani, ukiona ni mdogo, usiogope kuchukua hatua.

65. Changaoto hazitufanyi kuwa na furaha au kutokuwa na furaha, ni jinsi tunavyozichukulia ndio huamua hisia zetu kwenye hizo changamoto.

66. Bwana Yesu aliwahi kusema, Ufalme wa Mungu upo ndani yetu, hivyo ufalme wa shetani unaweza kuwa ndani yetu pia. Maana yake kama wema unakaa ndani yetu hata ubaya unaweza kukaa ndani yetu, hivyo wema na ubaya kukaa ndani yetu ni kutegemeana na maamuzi tunayoamua.

67. Binadamu ni viumbe wa ajabu sana, wanaweza kubeba majanga, kushindwa na hata mambo machungu sana, hivyo pia anaweza kubeba ushindi furaha, amani na mafanikio. Tumeumbwa na uwezo mkubwa sana wa kuweza kupitia kila hali kwenye maisha haya, tuna uwezo kuliko tunavyodhani.

68. Henry Ford aliwahi kusema kauli moja nzuri sana kuhusu mambo yanayotushinda maishani, alisema kama huwezi kukabiliana na jambo fulani ana achana nalo. Maana yake kama kuna jambo huwezi kulibeba kwenye maisha yako liache lijibebe lenyewe.

69. Kuna mambo yapo kabisa nje ya uwezo wetu kama binadamu na hatuwezi kuyaathiri kwa namna yoyote ile, tutayaacha tu yatokee kama yaliyo. Ukitambua hilo hutakuwa na hofu na mashaka kwenye baadhi ya mambo, utakuwa na amani na utulivu.

70. Mwanafalsafa mashughuri wa Roma, Epictatus aliwahi kusema, njia moja ya kuwa na furaha ni kuacha kuhofu na kuogopa vitu ambavyo vipo nje ya uwezo, au nguvu zetu kuvikabili.

71. Kuna nguvu kubwa tunaipata pale tunakubali kuwa kwenye maisha kuna vitu vipo nje ya uwezo wetu kuvikabili, kuna vitu hatuna nguvu ya kuvifanyia chochote au kuviamulia, vipo nje ya uwezo wetu.

72. Tunatakiwa kujua wakati wa kuwa chini na kuinama kuruhusu mengine yapite, hatuna nguvu za kukabiliana na kila kinachokuja mbele yetu, tukiwa wakaidi tunavujika, tujifunze kwa minazi na miti mingine.

73. Mfano, miti na misitu minene iliyositawi inajua kanuni hii ya maisha, inajua lazima upepo uje na haiwezi kushindana na upepo maana vinaweza kuvunjika, hivyo hukunja matawi yake, huinama na kusujudu ili upepo upite zake.

74. Tukubali kuomba Mungu atujalie neema ya kukubali vitu ambavyo hatuwezi kuvibadili, na kibali cha kubalidi yale tunayoweza kuyabadili. Na hekima ya kutambua tofauti.

75. Tusiwe wakaidi, tunatakiwa kujifunza kushirikiana na yale yasiyoepukika kwenye maisha yetu, hii ndio siri ya furaha na kuishi maisha marefu.

76. Usilazimishe mamba ambayo yalishatokea, usijaribu kuzoa maji yaliyokwisha mwagika. Imetokea imetokea basi, tafuta namna nyingine ya kuishi.

77. Wacha yaliyopita yajizike yenyewe, huna cha kufanya zaidi, na endapo utayafuatilia basi ujue utapata ulichokitafuta ambacho ni hofu, sura mbaya na vidonda vya tumbo.

78. Kumbuka, unapowachukia maadui zako maana yake unawapa nguvu juu ya amani yako, afya yako, usingizi wako, moyo wako nk.

79. Waliokuudhi wanaweza waziwaze kabisa kuhusu wewe, wanaweza kuwa wapo sehemu wanafurahia maisha na kucheza muziki, wewe unaendelea kuumia na kutoa lawama kwao, kumbuka unajiumiza mwenyewe.

80. Na aliyekuudhi atafurahia sana endapo atajua unaumia, unamuwaza au unamhofia kila mara. Jifunze kusamehe kwa ajili ya afya yako, nafsi yako, moyo wako, amani yako na furaha yako.

81. Ndio maana unaona Yesu katika mafundisho yake alisema, “wapendeni adui zenu” akaendelea kusema semehe mara saba sabini, Yesu alijua njia nzuri ya kuwa na afya, furaha na amani muda wote ni kuishi kwa upendo na kusamehe.

82. Kama utaishi na chuki, utashindwa kusamehe, basi jua hautakiwa mbali na shinikizo la damu, mashambulizi ya moyo, vidonda vya tumbo na magonjwa mengine. Jipende, samehe, achilia ishi kwa amani ukiwa na afya tele.

83. Unajua hofu, uchungu, chuki vinatufanya tushindwe hata kufurahia chakula tunachokula, na hapo ndipo afya zetu zinapodorora.

84. Hofu itakufanya uchoke hata kabla ya kuchoka, itakuondolea kila kitu kizuri kwenye maisha yako. Mwandishi wa kitabu hiki anasema hata kama tumeshindwa kuwapenda adui zetu, basi tujiepende wenyewe.

85. Dale Carnegie anashauri, kabla hujalala usiku, samehe kila kitu na kila mtu, fanya hivyo maisha yako yote. Ili ulinde afya yako, amani na furaha yako.

86. Maneno ya watu wanaokusema hayatakuvunja mifupa, jifunze kuyapuuza uendelee na maisha yako, kuna mambo mengi ya msingi unatakiwa kuyafanya kwenye maisha yako, usiwekeze kwenye maoni ya watu kuhusu wewe.

87. Usijaribu kuwa sawa na adui yako, maana yake usiwe mtu wa visasi au ubaya, yashinde mabaya kwa mema. Usiache mabaya yakutawale ukaishia kuamua vibaya na kutengeneza hofu.

88. Haitoshi kujisifia kuwa wewe ni mzalendo wa kweli, mzalendo wa kweli hana uchungu, visasi, chuki na wala hasira kwa mtu yeyote yule.

89. Usiweke mategemeo kwamba kwasababu ulimsaidia mtu sana kwenye maisha yake basi atakuja kukushukuru au kukusaidia na wewe, ukiwa na mategemeo hayo unaweza kuwa mtu wa malalamiko na asiye na furaha.

90. Ondoa mategemeo ya kusaidiwa, kusifiwa, au kupendwa ishi vizuri maisha yako bila kutegemea hayo mambo. Endapo utakuja kusaidiwa, kupendwa au kushukuriwa itakuwa ni jambo la ziada kwako, isiwe uhitaji maana ukitegemea ukikosa utaanza kutengeneza malalamiko na uchungu.

91. Usitegemee watu watakuwa wema kwako, au watakutendea mema, wape watu nafasi kubwa ya kukosea na kukukosea hii itakufanya uwe na uwezo wa kukabiliana na kila hali kwenye maisha yako.

92. Mwanafalsafa mahiri aliyewahi kuitawala Roma kwa mafanikio makubwa, Marcus Aurelius, aliwahi kusema, katika moja ya maandishi yake kuwa kila siku anapoamka asubuhi kwenda kazini anajiandaa kwenda kukutana na watu wachoyo, wabinafsi, wasio na shukrani, wakaidi, wenye kiburi na wakorofi. Alikuwa hashangazwi kabisa kukutana na watu hao maana bila wao hajui dunia ingekuwaje.

93. Ndugu msomaji wa uchambuzi wa kitabu hiki, kumbuka siku zote watu wanaweza kukusahau hata kama uliokoa maisha yao kutoka kwenye kifo, wengine wanaweza wasikushukuru hata kama umewafanyia jambo zuri kiasi gani, ni asili ya binadamu, hivyo yakitokea hayo kwenye maisha yako yasikuumize kichwa kabisa.

94. Mfano mzuri upo kwenye Biblia, Yesu aliponya vipofu 10, lakini ni mmoja tu ndio alirudi kushukuru. Jambo hili lilimfanya Yesu kuuliza nimeponya watu 10, amekuja mmoja kushukuru wengine 9 wameenda wapi? Ni asili ya binadamu kutoshukuru, ilitokea kwa Yesu, inaweza kutokea kwako pia, usishangae.

95. Furaha na amani yako inatakiwa kutokana na wewe kuwafanyia wengine wema, na isiwe kinyume chake. Aristoto, moja ya wanafalsafa maarufu sana alinukuliwa akisema, mtu bora zaidi ni yule ambaye furaha yake ipo katika kutoa na kuwasaidia wengine na sio katika kupokea au kusaidiwa na wengine.

96. Kama tunatafuta furaha kwenye maisha yetu tunatakiwa kujua, furha ya kweli ipo katika utoaji na sio upokeaje, hivyo tuache kabisa kutegemea shukrani au mema kutoka kwa wengine.

97. Kuna wazazi wanapata shida sana, presha zao ziko juu, vichwa vinawauma kwa sababu walizaa watoto na kuwafanyia makubwa kwa mategemeo kuwa watoto hao watakuja kurudisha fadhila kwa wazazi wao au walezi wao. Kumbuka mfano wa Yesu Inaweza isiwe hivyo mara zote.

98. Hapa simaanishi hatutakiwi kuwa watu wa shukrani, la hasha! Tunatakiwa kuwa wakarimu na kuwaonyesha wazazi wetu upendo, shukrani na fadhila. Lakini vitu hivyo visipotokea isiwe ndio wapandwe na hasira na kuishia kuwa na chuki.

99. Kama tunataka kuwa na watoto wenye shukrani, wakarimu, tunatakiwa kuwa hivyo sisi wenyewe kama wazazi.

100. Njia nyingine ya kuiua tabia ya hofu na mashaka ni kuhesabu baraka zako, angalia uliyonayo na sio yale ambayo huna, angalia faida na sio hasara, angalia suluhu na sio matatizo.

101. Hofu inaweza kufa kabisa kwenye maisha yako endapo utajenga uhusiano mzuri na Mungu, hapa inabidi uwe mtu wa imani, fanya sala, maombi na shukrani kwa Mungu wako.

102. Mahatma Ghandh, moja ya mtu mashughuri sana na baba wa taifa la India, alipigana vita vyote vya rohoni na mwilini na alishinda vita vyote bila kumwaga damu, moja ya kitu ambacho hakikukosekana kwenye maisha yake ni ibada na maombi.

103. Ghandh anakiri katika maisha yake ya kuleta mapinduzi kwa taifa la India, asingeweza kustahimili vitisho, hofu, mashaka mashutumu mengi yaliyokuja kwake kama asingekuwa mtu wa sala na maombi. Maombi na imani yake kwa Mungu yalimfanya apate nguvu za kustahimili kila upinzani kwenye maisha yake.

104. Hofu haiwezi kukaa kwa mtu mwenye imani, mtu mwenye uhusiano imara na Mungu, hofu na mashaka haziwezi kukaa pamoja na imani kwa Mungu. Imeandikwa kuwa, hatukupewa roho ya hofu na mashaka, bali roho ya nguvu.

105. Mwandishi wa kitabu hiki anashauri tusome Zaburi ya 23. Hii itasaidia sana namna ya kukuza imani yetu kwa Mungu na itatuondolea hofu na mashaka.

106. Usije ukakosa usingizi kwa sababu ya maneno ya watu juu yako. fanya mambo yako kwa uwezo wako wote, kwa ubora wa viwango vya juu sana, kisha waachie waendelee na kelele zao.

107. Kama unajihisi uchovu na kuchoka, jipe muda wa kupumzika, relax na tafakari mazuri na namna ya kuboresha kazi zako.

108. Usiogope kufanyia kazi malengo yako, hata kama itakugharimu kukosa usingizi, mwandishi anasema hakuna aliyewahi kufa kwa kukosa usingizi.

109. Tafuta vitabu bora vya kusoma ili uboreshe imani yako, hata mahusiano yako na watu wako wa karibu, hii itaongeza kujiamini na kujiona mwenye mchango kwenye jamii.

110. Hamasika kufanya mambo yako, tengeneza mazingira yote yawe mazuri na yatakayokufanya uhamasike kufanyia kazi ndoto zako, mfano kama ni ofisi hakikisha ipo katika mpangilio mzuri, taa, meza, kalamu nk.

111. Fanya mambo yako kwa vipaumbele, zinagatia vipaumbele kwenye ufanyaji wa majukumu yako, la muhimu ndio lianze na lifuate jingine.

112. Simamia masuala yako ya kifedha vizuri, pangilia bajeti yako na fanya manunuzi kulingana na bajeti yako, usitamani maisha ya mtu mwingine, boresha yako na yafanye unavyotamani yawe.

113. Chukua tahadhari zote muhimu, kama vile kulinda afya yako, kazi zako, biashara yako na utajiri wako, unaweza kukata bima.

114. Kuwa mwanamichezo, pasha misuli yako, furahi, cheka sana, usijichukulie serious saaana. Jicheke kwa uliyoyahofia ambayo hayakuwa halisi kama ulivyodhani.

115. Kumbuka leo ni ile kesho uliyokuwa unaihofia jana, amua kuondoka kwenye hofu maana umeona hakuna uhalisia kwenye mambo mengi unayohofia.

MWISHO:

Kitabu hiki kina mbinu nyingi na mafunzo mengi yenye mifano halisi namna watu walivyotoka kwenye maisha ya hofu na kuanza kuishi maisha yao kwa furaha na kwa ujasiri. Napenda kila mtu akisome kitabu hiki kitatibu magonjwa mengi sana yanayoisumbua jamii yetu. haya ni machache kati ya mengi yaliyoandikwa kwenye kitabu hiki. Tafuta nakala yako ujisomee, utajishukuru siku zote.

©Hillary Mrosso 22.08.2022


5 responses to “Uchambuzi Wa Kitabu: How To Stop Worrying and Start Living”

  1. Are there any books on how to be confident? How to be courageous and believe in yourself? Please share if there any ili nivitafute hata mwenyewe

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X