USHAURI: Jinsi Ya Kutunza Fedha Itakayokusaidia Kuanzisha Biashara


Moja ya eneo muhimu sana kwenye maisha ya kila siku Ni fedha. Upende usipende fedha ni muhimu tena sana.

Maana hakuna hata siku inapita bila ya wewe kutumia fedha.

Ukiamka tu asubuhi, ujue kitanda ulichokuwa umelalia ni FEDHA.
Ukivaa nguo zako, ujue umevaa fedha.
Ukipata kifungua kunywa, ujue hizo ni fedha pia.
Ukipanda daladala, hiyo nayo ni nini….

Sikiliza sasa, fedha ni muhimu sana, kiasi kwamba baada ya hewa ya oksijeni ambayo tunaipata bure, fedha ndio inafuata kwa umuhimu…
Sijui unanielewa hapo bwashehe….

Sasa mbali na umuhimu wote huo wa fedha, bado kuna watu wanaifanyia masihala.
Lakini wengine wanapata changamoto wanapokuwa na fedha.

Fedha ni chanzo Cha furaha yote

Na siku ya leo, nataka nitoe Ushauri kwa ndugu yangu na rafiki yangu Isack

Anasema hivi

Brother m n kijan delev bajaj nataman san kufug kuku ila kinacho nishind upend w kuifaz hela kutafut mtaj kilanikipat ela kidog matumiz yanaongezeka

Isack kutoka Mbeya

Ok vizuri sana ndugu yangu Isack. Kwanza nikupongeze kwa kuwa na ndoto na lengo la kufuga kuku.
Maisha yanaanza na malengo. Maana vijana wengi wanashindwa kufanya makubwa kwa sababu tu hawana ndoto wala malengo makubwa

Ili uvuke hiki kizungumkuti unapaswa kuwa na malengo au ndoto kubwa.

Labda ka ushauri kidogo tu kuhusu ndoto Yako. Usiishie tu kusema natamani kufuga kuku. Bali iweke sawa ndoto yako katika namna ambayo itakusuma zaidi

Kwa Mfano, ndoto Yako ikiwa ni kuwa mzalishaji na msambazaji nambari moja wa mayai kwa mbeya nzima.
Au mzalishaji nambari moja wa kuku wa nyama mkoa wa mbeya au hata nyanda za juu Kusini.
Yaani, kwamba ujenge jina kiasi kwamba yakizungumziwa mayai mkoa wa mbeya, au kuku wa nyama, basi jina Isack ndio liwe la kutajwa masikioni mwao.

Ni kweli hii ni ndoto kubwa, Ila sasa ubora wake ni kwamba unaweza kuanza kuifanya hata kwa udogo. Lakini pia hii ndoto itakusukuma siyo tu, uanze kufuga kuku. Bali utaenda zaidi ya hapo. Ujue ukiwa na lengo la kufuga kuku, hata baadaye ukijenga bada na kufuga kuku kumi tu, utaona Ni sawa. Ila Unapokuwa unajua mkoa mzima wa mbeya unakutegemea wewe kwa ajili ya mayai, au nyama ya kuku. Hapo utaweka juhudi zaidi.

Sasa tuongelee upande wa fedha.

Ili uweze kufanikishaa ndoto yako hiyo, jua wazi kuwa fedha haikwepeki. Utahitaji fedha tu. Na sehemu ya kuanza kupata fedha ni hiyo kazi uliyonayo. Ngoja nikwambie kitu rafiki yangu, nataka wewe uvunje rekodi ya KUWA dereva wa Bajaji wa kwanza, kutoka kwenye udereva mpaka kujenga ngome kubwa.

Unajua utaendaje. Fuatilia kwa umakini hapa

Kila siku kwenye kazi yako, jiwekee kiwango ambacho utakuwa unaweka akiba kuanzia leo. Kwa mfano, labda unaweza kuniambia nitaweka akiba ya elfu kumi kila siku. Kwa hiyo, kwenye kazi yako utakayokuwa unafanya utapaswa ujitume kwanza upate pesa uliyokuwa unapata kawaida, lakini pia utapaswa ujisukume uweze kutengeneza fedha ya ziada ya akiba, ambayo ni elfu kumi.

Najua lengo hili linaweza kuwa kubwa, lakini sasa hakuna jinsi. Kwa sababu kwanza umeshakuwa na ndoto kubwa, wewe pia unapaswa ujitume kiasi cha kutosha, ili hii ndoto yako uweze kuifanikisha. La sivyo, itabaki KUWA ndoto ya Habunwasi.

Ndoto kubwa zinahitaji kujitoa. NDOTO KUBWA ZINAKUHITAJI ULIPE GHARAMA. Na hii ni gharama mojawapo.

Kwa hiyo basi, kwa mpango huu maana yake, Kuna wakati utalazimika kuamka mapema sana kwa ajili ya kuanza kazi. Utalazimika kuwasiliana na watu mbalimbali ambao unawajua huwa wanasafiri kutoka eneo moja kwenda jingine, ili uwachukue wewe wakupe fedha.
Utalazimika kuacha kuangalia mechi hata kama ulikuwa unaipenda ili upige kazi ya kukuingizia kipato.
Na hata mchepuko wako,…au basi, utajua mwenyewe unafanyaje na mchepuko wako.

Bwana Isack nataka uanze kufanya hivi vitu kitalaam zaidi. Yaani, usiishie tu kutafuta hela na kuweka akiba chini ya godoro.


Hapa chini Kuna maeneo matatu ambayo napendekeza uweze kuweka akiba yako.


Nenda benki kafungue akaunti
. Kisha weka utaratibu wa kuweka kiwango cha akiba ulichopanga.
Ubora siku hizi benki zimerahisisha. Unaweza kuweka fedha benki ukiwa hata mtaani kwako. Au pale kijiweni baada tu kumshusha abiria…
Sijui unanielewa….

Kuna baadhi ya benki pia zinaruhusu wewe kufungua akaunti kwa mawakala. Hili nalo ni bao kisigino ndugu Isack. Kumbe haulazimiki tena kupanga foleni benki ili ufungue akaunti. UNACHOHITAJI NI KUDANDIA TEKNOLOJIA KIHIVYO.

Ukishafungua akaunti, hiyo hiyo kadi ya benki hiyo. Unaweza hata kuituma kwa bibi yako kijijini. Maana, kadiri unavyoendelea kuweka akiba najua utashawishika kwenda kuitoa fedha ukiwa na kadi. Ni Bora uitume Kijijini kwenu, au la unaweza kuiharibu kadi kabisa. Siriazi. Ujue hapa ninaongelea Mambo siriazi kwa ajili ya malengo na ndoto zako.

Ukikaa na hiyo kadi utashawishika kwenda kutoa fedha benki siku ukikutana na changamoto kidogo. Ila kama kadi huioni, itakusaidia usitoe pesa yako kwa haraka.

Kwa hiyo, unaweza kuiharibu kadi, ukifika wakati wa kutoa fedha benki utaomba kurenew kadi yako.

Ngoja ninywe maji kwanza, kabla sijaendelea…

Enhee, sasa bwana Isack, ukiachana na kungua akaunti benki. Unaweza kufungua akaunti UTT.
UTT, Ni mfuko wa uwekezaji wa pamoja ulio chini ya serikali ambao unawawezesha watanzania wenye fedha kidogo kuzikusanya kwa pamoja. Ambapo hizo fedha baadaye zinawekezwa kitalaam. Kwa fedha yako unayoweka, baadaye ukija kuitoa, unaitoa na faida.

Tena badala ya kufungua akaunti benki, Bora ufungue akaunti UTT mfuko wa Umoja. Au wewe unaonaje?

Huku fedha yako inakaa, Ila siku ukiihitaji, utajaza fomu, na itachukua siku saba tu kuipokea

Ukiona maelezo ya UTT huyaelewi vizuri hapa, unaweza kuwatwangia jamaa wa UTT wenyewe kwa namba hii 0754800455. Watakupa kizima. Halafu namba yenyewe unapiga bure bila hata kulipia . Yaani, hata kama hauna bando sasa hivi, ukipiga inaita na unaongea nao, labda ukipiga muda ambao siyo wa kazi mzee baba.

Sijui niendelee…au niishie hapa

Ngoja niendelee, kwanza…

Ukiona mizunguko yote hiyo mirefu basi kafungue laini ya simu maalumu kwa ajili ya kuweka akiba tu. Halafu unajua utafanyaje. Ukishafungua hii laini ya simu. Mfuate mtu wako wa karibu, labda mama, baba, mke, rafiki au yeyote unayemwamini. Utamwambia aweke namba ya siri.

Kwa hiyo, wewe utakuwa na laini, labda tuseme yenye Mpesa. Ila hujui namba ya siri. Utakuwa unaweka akiba kila Mara, Ila siku ukija kutoa fedha, utapaswa kuomba namba ya siri kwa mtu aliyekusaidia kuweka namba ya siri.

Mtu huyu unapaswa kumshirikish lengo na umwambie asikupe namba ya siri mpaka utakapokuwa umefikisha kiwango fulani Cha pesa.

ONGEA naye, kuwa mimi nataka niweke akiba ya milioni tatu kwenye hii laini. Tafadhali usiniambie namba ya siri mpaka nitakapokuwa nimeweka kiasi Cha milioni tatu kama akiba.

Siku nikikuonesha kuwa nimeweka milioni tatu kama akiba. Basi hapo ndipo utapaswa kuniambia namba ya siri.

Naona maji yangu ya kunywa yameisha, na Mimi naacha kuandika, ngoja nikatafute maji ya kunywa kwanza.

Halafu sikiliza kwanza
Hapa nina orodha, ya vitabu vitakavyokusaidia wewe Kufanikisha haya yote niliyoandika leo.

1. MAAJABU YA KUWEKA AKIBA
2. MAAJABU YA KUWEKEZA KWENYE HISA, HATIFUNGANI NA VIPANDE
3. JINSI YA KUFIKIA NDOTO ZAKO

Kupata vitabu hivi, wasiliana nami kwa 0755838391.

Mimi ni Godius Rweyongeza kutoka SONGAMBELE CONSULTANCY
0755848391
Morogoro-Tz

Una swali, maoni au ushauri? Kuna jambo linakutatiza, unataka ushauriwe?

Basi sikiliza, tuandikie chini


.
 


Nenda benki ufungue akaunti.
Kisha Anza kuweka fedha

Fungua laini ya simu ya kuweka AKIBA tu

Thibutu matumizi yako

Kusanya kiasi Cha kutosha kuanza kuwekeza.


2 responses to “USHAURI: Jinsi Ya Kutunza Fedha Itakayokusaidia Kuanzisha Biashara”

  1. Maandiko yako siku zote hutufunza,kwahiyo kupitia hilo la leo la kuhifadhi pesa nimejufinza pia

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X