Uchambuzi wa Kitabu: The Psychology of Money: Mambo 94 niliyojifunza katika kitabu hiki.


Mwandishi : Morgan Housel

Karibu katika uchambuzi wa kitabu hiki muhimu sana kuhusu masuala ya fedha, tamaa, na tabia za watu wanazozionyesha wanapokuwa na fedha, kwenye uchambuzi huu utaelewa kwa kina kwanini tabia zina mchango mkubwa kukufanya kuwa tajiri au kuwa masikini. Yote haya tutajifunza katika uchambuzi wa kitabu hiki. Karibu!

  1. Linapokuja suala la fedha hapo ndipo tunapoanza kutofautiana, maana fedha inahusisha sana tabia na tabia ndio huleta utofauti na utofauti huo ndio hufanya wengine kuwa matajiri na wengine kuwa masikini.
  • Kufanya vizuri kifedha hakuhusiani na kuwa na uwezo mkubwa kiakili bali kunahusisha zaidi tabia za mtu na hulka.
  • Tabia ndio huamua matumizi mazuri na mabaya ya kifedha na sio uwezo wake wa kiakili, ndio maana tabia ni ngumu kuifundisha hata kwa watu wenye uwezo mkubwa kiakili.
  • Matumizi mabaya ya fedha huchangiwa sana na mtu kushindwa kuzuia hisia zake ambazo huathiriwa na tabia alizonazo.
  • Mtu wa kawaida mwenye elimu ya kifedha anaweza kuwa tajiri endapo atakuwa na udhibiti mzuri wa tabia zake linapokuja suala la fedha.
  • Kufanikiwa kifedha sio kujua mahesabu mengi ya kifedha, uhasibu na uchumi, inahusisha zaidi tabia za kila siku za mtu.
  • Jinsi ninavyoamua kifedha inaweza isiwe na maana kwa upande wako, lakini ikawa na maana upande wangu.
  • Ukitaka kujifunza na kuelewa kwanini watu wanaingia kwenye madeni, huitaji kujufunza kuhusu riba, unahitaji kujifunza kuhusu historia ya binadamu.
  • Mara zote historia huwa haijirudii, watu ndio hurudia historia, na hii inaenda hadi katika masuala ya kifedha tunaona yanavyojirudia mara kwa mara.
  • Kinachoonekana cha ajabu kwako kwangu kinaleta maana. Hii ni kutokana na kuwa tuna maisha yaliyopitia vitu tofauti ambayo vinatufanya tuamue tofauti kwenye masuala ya fedha.
  • Uzoefu unaonyesha hatuwezi kuwa sawa katika masuala ya kifedha, utofauti wa malezi, makuzi na maamuzi ya watu kuhusu fedha yanatofautiana sana.
  • Mfano, mtu aliyekulia na kuishi kwenye umasikini atafikiri zaidi kuhusu hatari na zawadi tofauti na mtoto aliyekulia katika utajiri.
  • Utofauti tulionao ndio hutufanya tuione dunia katika mtazamo tofauti, na lipapokuja suala la fedha hutazamwa hivyo pia.
  • Wakati mwingine tunaposoma historia tunadhani tumeelewa kila kitu, ukweli ni kwamba hatujaelewa kila kitu kwa sababu hatukuwepo na hatukuhusika katika matukio hayo tunayoyasoma, kwa sababu hiyo hatuwezi kupata maelezo mazuri ya kutufanya tubadili baadhi ya tabia zetu kuhusu fedha.
  • Kwenye maisha kuna baadhi ya vitu inabidi tukutane navyo na tuviishi ili tuvielewe zaidi, sio kila kitu tutakielewa kwa kusoma historia yake.
  • Uzoefu unaonyesha uwezo wa mtu kustahimili hatari unatokana na aliyoyapitia katika maisha yake binafsi.
  • Wakati mwingine mafainikio hayahusishi uwezo mkubwa wa kiakili, wala elimu, wala ujuzi na teknolojia, bali inaweza kuwa ni bahati na mahali mtu alipozaliwa.Maamuzi yote wanayayafanya watu kuhusu fedha yanatokana na taarifa walizonazo na wanazozipokea kila siku kuhusu fedha, taarafa hizo ndio hujenga mitazamo tofauti kwa kila mtu.
  • Hakuna kitu kizuri sana kama unavyodhani wala hakuna kitu kibaya kama unavyofikiri na kutazama, ni kwa vile umeona sehemu moja tu ya shilingi.
  • Tuwe makini na watu ambao tunawasifia na kutamani kuwa kama wao, lakini pia tuwe makini na watu ambao tunawachukulia poa na hatutamani kabisa kuwa kama wao, kasababu hujaona kila kitu.
  • Punguza kuangalia mtu mmoja kama ndio aliyekamilika, jifunze kwa mapana na jipe nafasi ya kuelewa mambo kwa upeo mkubwa, watu wanapitia mengi sana ambayo hayaonyeshwi.
  • Tuelewe kabisa kwenye fahamu zetu, kuwa sio mafanikio yote yanatokana na kufanya kazi kwa bidi, na pia sio kila umasikini unatokana na uvivu. Tuepuke kutoa hukumu haraka.
  • Tunapokubali kuwa bahati hutokea kwenye mafanikio, pia tukubali nafasi ya hatari kama kitu kinachoweza kutokea kwenye safari ya mafanikio, hii itatupa mtazamo tofauti tunaposhindwa kufikia malengo tuliyojiwekea.
  • Tunapotoa nafasi kwa bahati na hatari kama vitu vinavyoweza kumtokea mtu yeyote katika safari yake ya mafanikio, itatupa nafasi ya kujisamehe pale tunaposhindwa kufikia mafanikio, na kutufanya tuhukumu bila lawama.
  • Kamwe epuka maisha ya kujilinganisha, hutaweza kuridhisha kila mtu kweye jamii yako, na gharama ya kuingia kwenye kujilinganisha na wengine ni kubwa, na sio rahisi kufikiwa.
  • Kuridhika ni kutambua kuwa kuendekeza tamaa zisizo na kiasi zinaweza kukupelekea kwenye majuto.
  • Kuna watu walikuwa ni matajiri na waliweza kumudu mambo mengi sana kwenye maisha yao kutokana na fedha nyingi walizokuwa nazo, lakini tamaa ya kupata fedha zaidi iliwafanya waingie kwenye biashara haramu, kamari, utapeli ambao ulipotezea fedha zao na kuingia katika mikono ya sharia na kufilisiwa kila kitu.
  • Usiingize fedha safi kwenye biashara zinazozalisha fedha chafu kwa kigezo cha kupata fedha zaidi, uzoefu na historia inaonyesha waliofanya mambo ya aina hii waliishia jela na majuto makubwa.
  • Tabia walizonazo watu wanapokuwa na fedha ndio hupelekea kupoteza fedha na kutoridhika hata kama wanapata fedha nyingi kwa njia nzuri.
  • Kupata fedha na kuzitunza fedha ni vitu viwili tofauti vinavyohitaji ujuzi tofauti, ndio maana ubepari ni mgumu sana.
  • Uwezo wa kuwa king’ang’anizi kwa muda mrefu, kutokatishwa tamaa, ndio huleta utafauti, uwezo wa kuvumilia hayo yote ndio unatakiwa kuwa ndio nguzo kuu kwenye mikakati yako yote ya uwekezaji, biashara, na kwenye kazi zako.
  • Kwenye biashara, uchumi, uwekezaji na kazi, wanaofanikiwa na kupata faida ni wale wanaovumilia na kustahimili mikiki mikiki wanayokutana nayo kwenye safari ya mafanikio.
  • Kuwa na mpago wa mafanikio ni muhimu sana, lakini sehemu moja muhimu katika mpango wowote ni kupanga pale ambapo mpango ulioupanga hautaenda sawa na mpango wako wa mafanikio.
  • Mwandishi anasema moja wapo ya aina ya juu ya utajiri ni kuamka kila siku asubuhi na kufanya chochote unachokitaka.
  • Uwezo wa kufanya kile unachokipenda, kwa wakati unaoutaka, na mtu unayemtaka, na kwa jinsi unavyotaka, ni zaidi ya fedha na dhahabu.
  • Binadamu yoyote hakuna kitu kitamfanya ajisikie vizuri na mwenye nguvu zaidi kama anapokuwa na hisia za umiliki na kudhibiti mambo kwenye maisha yake. Hakuna hisia nzuri kama hizi kwenye maisha na ndio huleta furaha ya kudumu.
  • Kwa asili binadamu wote tunapenda kuendesha maisha yetu wenyewe, tunataka tuwe waamuzi kwenye maisha yetu, tunataka tuamue vitu kwenye maisha yetu. Hakuna binadamu anayetaka kuendeshwa na kupelekeshwa kwenye maisha yake.
  • Kutawala na kuutumia muda wako vizuri ni zaidi ya jinsi fedha inaweza kukulipa, ni uhuru mkubwa sana.
  • Wahenga wanasema, sikiliza zaidi, kuwa na muda mwingi wa kuchakata mambo katika ubongo wako, kwa kufanya hivyo utapata nafasi ya kuanzisha jambo lako kwa mafanikio.
  • Watu wanadhani wanahitaji magari ya gharama, kuvaa saa za gharama, mavazi ya gharama au kuwa na nyumba kubwa ya gharama, ukweli ni kwamba hawahitaji vitu hivyo, watu wanahitaji heshima na kupendwa na watu wengine.
  • Wengi hudhani kuwa na vitu vya gharama wataheshimika na kupendwa na watu wengine. Pia watu wengi hudhani watu wenye mali na wenye vitu vya gharama wanaheshimika na kufurahiwa zaidi yao.
  • Watu wanatafuta utajiri na kumiliki vitu vya gharama ili wapendwe, haitakuwa hivyo mara zote, badilisha mtazamo wako.
  • Kama unatafuta kuheshimika na kupendwa kwa kuwa una vaa au unamiliki vitu vya gharama fikiri tena, heshima haitafutwi hivyo njia hii, itakugharimu sana. Heshima, ubinadamu, na kusaidia wengine ndio vinaleta heshima kwako kuliko nguvu nyingi unazotumia kununua na kumiliki vitu vya gharama kubwa ili uheshimike na kupendwa.
  • Kumbuka siku zote, utajiri wa mtu sio vile unavyomuona navyo, utajiri halisi wa mtu hauwezi kuuona kirahisi.
  • Mara nyingi tumekuwa tunatumia taarifa tunazoziona kwa nje na kufikiri mtu huyu ni matajiri au masikini. mfano, magari, picha za mitandaoni, mwonekano, mavazi anayovaa nk.
  • Vitu ambavyo hatuvijui au kuviona kwa mtu ndio utajiri wenyewe, kama vile kiasi cha fedha katika akaunti yake ya benki, uwekezaji wake, nk.
  • Dunia ya sasa ina waigizaji wengi sana wanaoonekana ni matajiri kumbe hawana kitu, ni rahisi kuigiza na kunekana mtu tajiri hata mitandao ya kijamii inaweza kukusaidia kufanya hivyo, hivyo basi punguza kuhukumu na kufikiri taarifa za nje pekee zinaweza kukuamulia kuwa mtu fulani ni tajiri au masikini.
  • Utajiri ni gari zuri ambalo halijanunuliwa, almasi ambayo haijanunuliwa, saa ya gharama ambayo haijanunuliwa, nguo za gharama ambazo hazinanunuliwa, na vitu vingine vya gharama kubwa ambavyo havijanunuliwa.
  • Hivyo utajiri ni asseti za kifedha ambazo hazijabadilishwa kuwa vitu vinavyoonekana.
  • Siku zote tukumbuke, endapo tutamia hela kununua vitu, tutaishia kuwa na vitu hivyo bila kuwa na fedha.
  • Wengi wanadhani kuwa milionea ni kutumia mamilioni, kitu ambacho ni tofauti kabisa na kuwa milionea. Unaweza kutumia mamilioni ya fedha kununua vitu lakini haimaanishi wewe ni milionea, umilionea haupo kwenye matumizi.
  • Shida kubwa ipo watu wanataka kuonekana matajiri kwa kutumia pesa, utajiri wa kweli haupo kwenye muonekano wa nje, utajiri wa kweli upo kwenye vitu usivyoviona.
  • Watu wengi hujiona na kujisikia ni matajiri kwa kutumia fedha nyingi kununua vitu vizuri.
  • Sio kazi kuwaona watu waliojifanya matajiri, kwasababu kuna wengi wanafanya hivyo ili waonekane na watu.
  • Tunashindwa kuwaona matajiri wa kweli kwasababu wengi wanajifanyisha matajiri kwa nje hivyo inatuwia vigumu kutambua haraka na kupata watu sahihi wa kutuongoza.
  • Ni ngumu kujifunza kwa vitu usivyoviona, na utajiri wa kweli hauonekani, maana vinavyoonekana sio halisi.
  • Mwandishi wa kitabu hiki anasema utajiri unatengenezwa kwa kuweka akiba na sio kwenye matumizi.
  • Utajiri ni malimbikizo ya muda mrefu ya mali na fedha ulizobakiza baada ya matumizi yako, na kama ilivyo huwezi kujenga utajiri bila kuwa na mapato mengi basi hutaweza kuwa tajiri bila kuwa na uwekezaji mkubwa.
  • Kama unataka kukuza uwekezaji wako, unatakiwa pia kukuza na kuongeza uvumilivu wako, maana utajiri na mafanikio yanahitaji muda.
  • Kuweka akiba ni jambo lililopo ndani ya uwezo wa kila mtu, na huhitaji sababu nzuri kwanini usiweke akiba, huhitaji kuwa hata na sababu kwanini unahitaji kuweka akiba, wewe weka akiba.
  • Akiba inaweza kutengenezwa kwa kuwa na matumizi kidogo, au kudhibiti matumizi yako ya fedha, na unaweza kudhibiti matumizi endapo tutapunguza tamaa, na tamaa itapungua endapo hatutajali sana wanachofikiri watu wengine kuhusu sisi.

SOMA ZAIDI: Fursa Tano Ambazo Vijana Wa Siku Hizi Wanachezea (SEHEMU YA TATU)

  • Dunia inabadilika kwa kasi sana, baadhi ya mambo yanatuacha na mshangao, kwasababu hiyo tunasafari ndefu hapa duniai ya kuona mambo mengi ambayo hatujayatarajia.
  • Mambo mengi yanatokea hapa duniani bila hata sisi kujiandaa, dunia haitabiriki nini kinaweza kutokea kesho, hivyo basi tunatakiwa kuwa na fedha nyingi za kuweza kuhimili hali zozote mbaya zinazoweza kutokea baadaye.
  • Kama kuna jambo tunatakiwa kulielewa katika maisha yetu ni kwamba makossa hutokea na tunatakiwa kutoa nafasi ya kukosea kama sehemu ya maisha.
  • Sio kila kitu tutapanga kitaenda kama kilivyopangwa kwa asilimia 100, kuna mengi yasiyotarajiwa huweza kutokea katika mipango yetu, kwa kutambua hilo tunatakiwa kutoa nafasi hiyo ya makosa kutokea.
  • Tukitambua kuwa makossa huweza kutokea licha ya kuwa na mipango mizuri itatusaidia kustahimili misuko suko mingi ya maisha na kutupunguzia majuto.
  • Mambo yasiyotarajiwa yanaweza kutokea wakati wowote katika safari ya mafanikio, hivyo tunaposimama na kuiangalia dunia hatutakiwi kuiangalia kwa mstari mnyoofu wa nyusi na nyeupe.
  • Matarajio yako yasiwe makubwa sana kwasababu ya mipango yako, kuna mengi huyajui yanaweza kutokea kwenye safari yako na kuharibu kabisa au kubali kabisa mipango yako, kuwa tayari kwa hilo.
  • Kila kitu kina gharama yake, hivyo hata kwenye masula ya kifedha, tambua gharama unayotakiwa kuilipa na ulipe ili kufikia ndoto zako.
  • Gharama ya kitu au kufikia ndoto zako inaweza isiwe sawa na ulivyohadithiwa, ukiingia na kuanza utekelezaji wa malengo yako ndio utaona gharama halisi uliyotakiwa kulipa au ya kitu hicho.
  • Kila kazi inaonekana ni rahisi kwasababu hujaingia kuifanya, ukiifanya ndio utajua gharama yake ambayo wengi hatuioni.
  • Ugumu wa kitu upo kwenye kukifanyia kazi, na sio kwenye maneno tu ya mdomoni. Ndivyo ilivyo hata kwenye uwekezaji, ni rahisi sana kuzungumza uwekezaji na faida zake na hasara zake, lakini gharama na ugumu wake upo katika utekelezaji.
  • Usidhani dunia ni nzuri kama unavyofikiria, hakuna kitu cha bure, kila kitu kizuri utakilipia, hakuna cha bure dunia hii ndugu yangu.
  • Hakuna atakaye kupa zawadi ya bure, hakuna hata miungu itayokuja kukupa kitu cha bure hapa duniani, Mungu na malaika, na asili yote inaangalia wanaojitoa na wanaofanya kazi ili wawabariki. Kuna gharama za kulipa ili upate baraka…hakuna baraka za bure.
  • Namna nyingine nzuri ya kutusaidia katika kuweka akiba ni kufikiria akiba kama ada unayotakiwa kuilipa ili upate kitu fulani cha thamani, na sio kama faini ambayo unatakiwa kuikwepa.
  • Suala la kuweka akiba ni juu yako kujishawishi vya kutosha kuwa, kuweka akiba itakusaidia na ni muhimu kama sehemu yoyote ya mwili wako.
  • Dhibiti kabisa matumizi yako ya fedha, matumizi yako ya fedha yasiingiliwe na ushawishi wa watu wanaokuzunguka, amua kutumia pesa zako kwa matumizi muhimu tu.
  • Jamii ina watu wanacheza michezo ambayo huijui na fedha zao, kamwe usishawishike ukaamua kuwa mjinga kutumia fedha zako kawaababu ya ushawishi wao.
  • Cheza mchezo wako mwenyewe na fedha zako kwa faida yako, usiingiliwe na kushawishika kufanya mambo mabaya na fedha zako ikaja kukugharimu.
  • Dunia ina kamchezo cha kuamini na kuzipa umakini mkubwa habari mbaya au hasi kuliko habari nzuri.
  • Habari za kuogofya, habari za vita, mauaji na majanga ndio huteka umakini wa watu zaidi kuliko habari njema za matumaini.
  • Mfano mzuri mwambie mtu mambo yatakuwa mazuri na hali itakuwa shwari hatakusikiliza kiviile, ila mwambie kuhusu hatari, vifo, mambo ya kutisha yatakayokuja, nakwambia atakusikiliza kwa makini sana, na hivyo ndivyo ilivyo duniani kote, habari mbaya huenezwa na hununuliwa na watu hulipwa kuja kuelezea vizuri kuhusu habari mbaya.
  • Watu wenye habari mbaya ndio hutafutwa, hupewa nafasi kwenye radio, TV magazeti na ndio wanaosikilizwa zaidi. Ukiwa na habari nzuri hakuna atakayekutafuta wala kukusikiliza, watu wanapenda kusikia habari hasi zaidi kukiko habari chanya.
  • Angali mafanikio yaliyofikiwa kwenye sekta za uchumi, afya, miundombinu, biashara, masoko na uwekezaji lakini hizi sio habari za kugonga vichwa vya habari, watu wanataka kusikia milipuko ya moto, vita, mabomu, tetemeko la ardhi, vifo, ajali, magonjwa kama corona, na majanga mengine ya kutisha.
  • Habari mbaya na hasi ndio huuza zaidi, habari njema na chanya hazina soko. Kuwa makini na taarifa zinazovuma sana, maana zinaweza siziwe na uhalisia wote.
  • Ndio maana mara nyingi habari za moto moto ni zile zinazoelezea kuyumba kwa uchumi, kushuka kwa uchumi, na sio kupanda kwa uchumi, wataalamu wengi wanapenda kueleza kushuka kwa uchumi kuliko kupanda kwa uchumi.
  • Ni rahisi kuelezea kushuka kwa uchumi, kutengeneza hofu, na kutenegeneza stori nyingi kuhusu kushuka kwa kuchumi kuliko kupanda kwa uchumi.
  • Wengi hupenda kutabiri anguko la uchumi, na majanga mengine yanayoweza kutokea baadaye, lakini imekuwa ngumu sana kutabiri mafanikio na kukua kwa uchumi. Hii ni kwabababu ukuaji wa uchumi hufanyika taratibu na hauonekani kirahisi, ila anguko ni rahisi kuonekana na wengi hupenda kutolea maelezo.
  • Ukweli ni kwamba kuna majanga mengi yanaweza kutokea kwa muda mfupi na kwa haraka, lakini sio hivyo kwa miujiza na mafanikio yanachelewa na kukawia.
  • Lazima tuufikie ukweli kwamba vinatokea vitu vingi hapa duniai ambavyo hatutakuwa na uwezo navyo wa kuvidhibiti, kuna vitu tutaacha tu vitokee maana hatuwezi kuviathiri kwa vyoyote.
  • Hatari ndio kitu pekee hubakia baada ya kufikiria umepanga kila kitu na kila kitu kipo kwenye mstari sahihi. Hii inamaana hata kama una mipango mizuri kiasi gani, bado inaweza kuathiriwa na hatari usizoziona wala kuzijua.
  • Sayansi ya kurusha ndege na roketi ni tofauti sana na sayansi ya uchumi, uwekezaji na biashara. Kwenye sayansi ya kurusha roketi kuna fomula ambazo zimetenezwa, na wanatumia mahesabu na kanuni kufanikisha mambo yao, ni eneo ambalo hisia hukaa pembeni kabisa tofauti na maswala ya fedha, uchumi, biashara na uwekezaji, ambayo huingiliwa na hisia na mitazamo ya watu wenye tabia zinazotofautiana.
  • Kuwa msimamizi mzuri wa fedha zako kwa namna ambayo itakufanya utalala usingizi mzuri usiku. Weka akiba ya kutosha.

Ahsante kwa kusoma uchambuzi wa kitabu hiki, karibu na endelea kufuatilia chambuzi nyingine za vitabu hapa hapa.

Mchambuzi: Hillary Mrosso

Mawasiliano: +255 683 862 481

hillarymrosso@rocketmail.com

Tarehe: 01.03.2022


3 responses to “Uchambuzi wa Kitabu: The Psychology of Money: Mambo 94 niliyojifunza katika kitabu hiki.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X