AMRI KUMI ZA MAISHA


Huwa likitajwa neno Amri mara nyingi huwa linahusishwa na Amri za Mungu ambazo ndizo amri maarufu. Leo nataka nikwambie pia amri za maisha. Hizi amri hizi hakuna mtu yeyote ambaye anakubembeleza kuzifuata au kuzivunja. Ni au unazifuata kwa faida yako au unazivunja kwa hasara yako.

Kama umewahi kusikia usemi kwamba malipo ni hapahapa duniani. Ukizifuata  amri hizi malipo yake unayapata hapahapa duniani na ukizivunja, unalipwa hapahapa duniani.

Hizi amri hizi hazina cha kusubiri mpaka moto milele ili kuadhibiwa. Adhabu yake ni papo kwa hapo au baadaye kidogo, lakini adhabu yake haisubirishwi wala zawadi yake siyo ya kusubiri pepo, ni hapahapa duniani.

AMRI YA KWANZA: UTAVUNA ULICHOPANDA ( Hii pia inatokea kuwa ndio amri kuu kwenye hizi amri za maisha).

Kulingana na amri hii ni kwamba huwezi kupata kitu, tofauti na vile unavyostahili kupata. Unavuna kile ulichopanda. Huwezi kupanda maharage, baadaye ukaja kuvuna mahindi. Haiwezekani.

Kulingana na amri hii ni kwamba pale unapokuwa unataka matokeo fulani, basi panda mbegu inayoendana na matokeo unayotaka.

Kama unataka karanga, panda mbegu ya karanga.
Kama unataka utajiri panda mbegu ya utajiri. Kama unataka mahusiano mazuri basi panda mbegu yake.
Unavuna ulichopanda.

Ikitokea kwamba, ukataka kwenda kinyume na hii amri. Ukweli ni kwamba utaishia kuadhibiwa maana malipo ni hapahapa duniani.

Ukienda kuvuna mahindi pasipo kupanda maana yake utakuwa umevunja hii amri na mwisho wa siku utapaswa kuadhibiwa kama mwizi.

Ukitaka utajiri bila kupanda mbegu yake maana yake utakuwa umeenda kinyume na asili na utakuwa fisadi. Na malipo yake ni hapahapa duniani.

Kama Kuna kitu unapaswa kufahamu ni kwamba mara zote na sehemu zote utavuna ulichopanda.
Ukitaka matokeo fulani, basi panda mbegu zake.

AMRI YA PILI: KITU CHOCHOTE KIKIRUSHWA JUU, KITARUDI CHINI

Hii ni kanuni ya fikizia lakini inatokea kuwa ndiyo kanuni ya asili pia. Si unajua kuwa fizikia ndio tawi kongwe kwenye matawi yote ya masomo. Fikizikia ilikuwepo tangu uumbaji au wakati wa Bing bang.

Kanuni hii ukiijua utaifurahia sana. Na ubora hakuna mtu anayekulazimiaha wewe kuifuata. Ni au unaifuata wewe kwa faida yako au unaachana nayo kwa hasara yako.

Ukiivunja amri hii kwa kupanda juu na kujirusha chini, utavunjika. ukiifahamu amri hii maana yake utajua wapi unapaswa kuruka na wapi hupaswi kuruka. ni wapi ujiachie na wapi usijiachie.

AMRI YA TATU: UTAENDELEA KUKAA KATIKA HALI ULIYONAYO MPAKA PALE NGUVU YA ZIADA ITAKAPOTOKEA

Hii ni amri nyingine unayopaswa kuijua. Kitu chochote ambacho kimetulia kitaendelea kutulia mpaka itokee nguvu ya ziada ya kukiweka kwenye mwwndo. Na kitu chochote ambacho kipo kwenye mwendo kitaendele kuwa kwenye mwendo mpaka itokee NGUVU YA ZIADA ya kukitoa kwenye mwendo.

Na kwenye maisha ni au upo kwenye mwendo au umeitulia. Ni hivyo tu.

Kama kuna malengo au ndoto kubwa ulizonazo na unataka kupata matokeo basi ingia kwenye mwendo.
Wengi kwenye maisha hawapati wanachotaka kwa sababu hawapo kwenye mwendo; muda wote wametulia…

Mtu anataka kufikia Mambo makubwa maishani, Ila haweki kazi. Kwa amri hii Ni vigumu sana kuyapata hayo matokeo.

AMRI YA NNE:  TUNZA MUDA
Vitu vyote vitafanyika kulingana na muda uliopo. Kwa siku tuna saa 24 tu na siyo zaidi ya hapo. Kama unataka kufanya makubwa, tumia vizuri muda wako.

Usikubali kuibiwa muda wako. Muda ni Mali Kama zilivyo mali nyingine.

Mtu akija kwako na kubeba runinga, simu yako na samani utasema Ni mwizi kwq sababu amebeba mali zako.

Lakini mtu akija kwako kukupisha stori unamwacha, unaona Ni mtu mwema. Wakati anakuibia muda.

Laiti kama kila mtu angejua umuhimu wa muda na kuutumia muda wake kufanya kazi kwa weredi, Nina hakika hii duniani kusingekuwa na malalamishi wala ufanyaji wa maovu.

AMRI YA TANO: Tunza mawazo yako vizuri

Wanasaikolojia wamethibitiaha kuwa kwa siku moja tu mtu unakuwa na mawazo 6000 kwa siku.

Mawazo mengine huwa yanapita kiasi kwamba wewe mwenyewe hatahufahamu Kama yameoupita. Kumbe Sasa kitu kikubwa kwako ni wewe kuhakikisha kwamba unatunza Yale mawazo yako ya muhimu.

Unapaswa kufanya hivyo ili kutoa nafasi ya mawazo mengine kuendelea kuja.

Lakini pia ili uweze kuyakumbuka mawazo yako yote hapo baadaye.

Hivyo kuanzia Sasa, Jenga utaratibu wa kuandika mawazo yako chini.

AMRI YA SITA: HAKIKISHA UNAJUA UNACHOTAKA
Kinachofanya watu wasipate wanachotaka ni kwa sababu hawakijui. Na wewe usipojua unachotaka utazunguka huku na kule bila kupata matokeo yoyote Yale ya maana.

AMRI YA SABA (A): WAFANYIE WATU KILE UNACHOPENDA UFANYIWE
Kama kuna kitu hupendi kufanyiwa usiwafanyie watu wengine.
Najua hupendi kuibiwa, kwa hiyo usiibe.
Najua hupendi kupigwa, kwa hiyo usipige watu.
Najua hupendi kusemaa vibaya, kwa hiyo usiwaseme watu vibaya.

AMRI YA SABA (B): WAFANYIE WATU WANACHOPENDA WAFANYIWE

Kuna wakati unapaswa kuwafanyia watu kulingana na vile wanavyotaka wao.

Kama mtu ana kiu, mpe maji.
Kama mtu ana tatizo,  msaidie kulitatua.

AMRI YA NANE: KAMA UNATAKA KUPOKEA TOA.

Kutoa ni kitu muhimu sana kwenye maisha. Kama unataka kupokea toa. Na hivi vitu viwili vinaendana sana. Kutoa na kupokea. Yaani, ni kama mzani vile. Unapaswa kujenga utaratibu mzuri wa kutoa, lakini pia unapaswa kuwa na utaratibu wa kupokea.

Ni muhimu kutoa, ni muhimu pia kupokea.

Kuna watu ni wabovu kwenye kupokea ndio maana fursa nyingine za kifedha huwa zinawapita.

Nakumbuka nilijiwekea utaratibu wa kutoa kitu hata kama Ni kidogo kila siku.

Siku moja nilikutana na mtoto na kuamua kumpa shilingi mia moja kama sehemu ya utoaji wangu. Yule mtoto aliikataa Ile hela kwa kusema kwamba amekatazwa kupokea fedha na wazazi wake. Sikumlazimisha kwa sababu asili pia huwa hailazimishi. Ilikupa wewe kitu ukakikataa, jua wazi kuwa Kuna MTU mwingine ambaye anaenda kunufaika na kile ambacho wewe mwenyewe umekataa.

Baada ya kugundua kuwa Hilo, nimeandaa sala yangu binafsi linapokuja suala la fedha, kutoa na kupokea. Na wewe unaweza kuitumia pia. Inasema hivi. Ewe nguvu ya asili, Kama kuna fursa au fedha zinakuja kaa watu na hawapo tayari kuzipokea, tafadhali Sana naomba uziletw kwangu. Nipo tayari kuzitumia na kuzitumia kwa usahihi maishani mwangu.

Napenda kusisitiza kitu kimoja kikubwa: najua wengi wanaamimi kuwa ni kheri zaidi kutoa kuliko kupokea. Ila ukweli ni kwamba, kwa kanuni za asili zilivyo, ukitoa milango ya wewe kupewa inafunguka pia. Hivyo siyo kheri kutoa tu! Bali ni kheri zaidi kutoa na ni kheri zaidi kupokea. Kama nilivyosema tangu mwanzo, hivi vitu ni Kama mzani, hakuna upande ambao unapaswa kuzidiwa.

Haupaswi kuwa mpokeaji tu kila mara. Na haupaswi kuwa mtoaji bila kupokea.

Ili mzani uende sawa unapaswa kutoa na unapaswa kupokea. Kwa hiyo, ni kheri zaidi kutoa na ni kheri zaidi kupokea pia.

Ila sasa ukitoa, usianze kulazimisha kupewa. Kamwe usifanye hivyo. Na usitegemee kupokea kutoka kwa mtu hiyohiyo ambaye wewe umempa.

Asili huwa haisahau, ni Kama vile inakutunzia mema yako na baadaye yale mema yako yanakurudia kwa njia nyingine ambayo ni bora zaidi.

Na wala ukitoa usijigambe.

Mwembe unatoa maembe lakini haujigambi kuwa umetoa maembe.
Ng’ombe anatoa maziwa ila haujigambi wala kutamba kuaa katoa maziwa.

Na wewe ukitoa usije kuanza kusema ooh, unajua, fulani asingekuwa na maisha aliyonayo bila ya mimi. Ooh unajua mimi ndiye nimemsaidia mtu fulani kupata kitu fulani.

Kibaya zaidi, usije ukaanza kulazimisha mtu akupe, eti kwa sababu wewe umempa au uliwahi kumpa kitu fulani siku za nyuma.

AMRI YA TISA: SHUKURU

Jenga utaratibu wa kushukuru. Kuwa mtu mwenye shukrani Mara zote!

Kuna watu wanashangaza kweli.
Mtu anaweza kuwa na shida ya fedha, akatokea mtu akamtumia kiasi kidogo kulinganisha na kile alichokuwa anataka, unakuta huyu aliyetumiwa anaanza kulalamika, ooh fedha yenyewe kanitumia kidogo!

Ndugu yangu, SHUKURU. Kushukuru ni kuomba tena Kama ulivyo methali ya wahenga wetu.

Mtu akikupa kitu SHUKURU.
Ukiamka asubuhi SHUKURU,
Ukimaliza siku yako SHUKURU.
SHUKURU kwa ajili ya wazazi wako, ndugu zako, watoto wako, mwenza wako, nguvu zako, mali na chochote unachomiliki.

Una vitu vingi vya kushukuru kuliko kulalamika.

Kwenye Biblia Yesu alikuwa mfano mzuri kwenye hili. Kila alipotaka kufanya Jambo alishukuru kwanza.

Ndio maana kwenye Biblia utakutana na maneno kama baba nakushukuru kwa ajili ya…Mara nyingi.

Alipotaka kuponya mtu alishukuru.
Alipotaka kulisha watu alishukuru
Na hata alipokuwa anakufa alishukuru.

Wewe pia Jenga utaratibu wa kushukuru.

Ila ngoja kwanza,
Napenda kushukuru sana kwa kusoma andiko langu la leo. Ubarikiwe sana, endelea kufuatilia mafunzo mengine zaidi hapahapa.

Kila siku naweka Makala mpya mbili bila kukosa.

Unaweza pia kupata mafunzo zaidi kwa njia ya email hapa.

Asante.

AMRI YA KUMI: KITU CHOCHOTE KISIPOTUMIKA KITAPOTEA

Hii ni amri nyingine pia ambayo unapaswa kuifahamu. Kiungo cha mwili, kipaji au uwezo wako usipoutumia, jua kuwa uwezo huu unaenda kufifia na itafikia hatua ambapo utapotea. kipaji chako usipokitumia kitapotea. Na hata ukijenga nyumba bila ya kukaa, itaharibika.

yaani kuna vitu viwili. ni au utumie uwezo wako ili uendelee kuongezeka zaidi na zaidi au usiutumie ili upotee.

kuna watu huw wanadhani kwamba wakitumia kitu labda kipaji chao kitakwisha. hakuna kitu kama hicho. kadiri unavyotumia uwezo wako, ndivyo unavyoongezeka na kuzidia na wewe unazidi kuwa imara zaidi.

kadii unavyoandika ndivyo unazidi kubobea zaidi

kadiri unayotibundivyo unazidi kuwa daktari mbobevu.

kadiri unavyoimba, ndivyo unazidi kupanua wigo wako na kuwa mwimbaji mzuri zaidi.

kadiri unavyochora ndivyo unazidi kuwa mchoraji mzuri zaidi.

ukifuatilia watu wote waliobobea, kazi zao za kwanza hazikuwa kazi bora kabisa. hata Ben Carson ambaye ni daktari maarufu kwenye suala zima la upasuaji, hakubobea siku ya kwanza. ila kadiri alivyokuwa akiendelea kutumia uwezo wake, ndivyo alivyokuwa anazidi kuimarika na kuwa bora zaidi.

na wewe kama una kipaji. kitumie. nakuhakikishia kuwa utazidi kuimarika na kuwa bora zaidi ya ulivyokuwa mwanzoni.

hizo hapo ndizo amri za maisha. zifuate kwa manufaa yako, zivunje kwa hasara yako.

kila la kheri.

Ni mimi rafiki yako wa ukweli Godius Rweyongeza kutoka SONGAMBELE

Tuwasiliane kwa 0755848391

kwa mafunzo mengine zaidi kutoka kwangu. usisite kujiunga na jumuiya ya watu wangu wa nguvu wanaopokea mafunzo kwa njia ya barua pepe hapa chini. kila la kheri.




2 responses to “AMRI KUMI ZA MAISHA”

  1. Asante kwa kuandaa somo zuri.
    Ni ujumbe wa maana sana na wa kumfanikisha mtu katika kila jambo ikiwa ataamua kubadilika na kuwa na nidhamu ya maisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X