Fursa Tano Ambazo Vijana Wa Siku Hizi Wanachezea (SEHEMU YA PILI)


 

Leo tutaendelea na sehemu ya pili. Kama hukusoma sehemu ya kwanza; BONYEZA HAPA kwanza.

2. Fursa ya kujifunza
Acha nikurudishe nyuma tena, mpaka miaka ya akina Benjamin Franklin. Miaka hiyo walikuwa wanafanya apprenticeship kwa miaka 7-9. Huo ni muda ambao mtoto au kijana alikuwa ananolewa chini ya mtaalamu bila malipo. Kama kijana alifuatilia vizuri masomo yake basi ilikuwa inategemewa kuwa baada ya muda huo kijana atakuwa amenolewa na kunoleka. Na baada ya miaka hiyo 7,8 au 9 alikuwa anaweza kufanya kitu alichokuwa anaandaliwa kukifanya. Akina Darwin, wote walipitia kwenye kipindi hiki cha kujifunza kwa vitendo.

Na hiki ndicho kimekuja kuzalisha ile dhana ya saa elfu kumi kwenye ulimwengu wa hamasa.
Unaifahamu dhana ya saa elfu 10? Dhana hii imepewa unaarufu sana na mwandishi Malcon Gladwell. Kwenye kitabu chake cha Outliers, mwandishi kaainisha kuwa inachukua saa elfu kumi kwa mtu kuwa mbobevu kwenye jambo fulani.

Yaani, kuwa hizi ni saa elfu kumi mbapo mtu anaweka akili yake, nguvu zake na kila rasilimali aliyonayo katika kufanyia kazi kipaji, ujuzi au kitu fulani. Na baada ya huo muda kama kweli mtu huyo atakuwa amejitoa na kujifunza kwa kina basi atakuwa ameweza kufanikiwa kufikia utaalam au ubobevu.
Mwandishi anatolea mfano wa Bendi maarufu ya The Beatles. Hii ilikuwa bendi maarufu sana miaka ya 60 huko Marekani. Ilifanya maonyesho kwa weredi mkubwa na iliuza albamu nyingi kwa enzi zake. Mpaka leo hii inaaminiwa kuwa ni bendi bora kuwahi kutokea. Kama huamini kamuulize Google.

Sijui kwa hapa Tanzania bendi maarufu miaka hiyo ilikuwa ipi. Ngoja kwanza nimpigie baba yangu, bila shaka ataniambia. Si unajua mimi kijana wa kisasa najua tu mambo ya akina Diamond, Alikiba na Harmonize? Hahaha

Achana na hayo tuendelee bwana, Japo dhana ya saa elfu kumi imekuja siku za hivi karibuni, ila ilikuwepo tokea enzi hizo. Ndiyo maana enzi za akina Benjamin Franklin vijana walisota hiyo miaka 7-9. Kipindi ambacho sasa hivi kinaaminika kuwa kinaendana na hizo saa elfu kumi.

Hata Benjamin Franklin alisota miaka 9 chini ya kaka yake akijifunza uchapaji wa vitabu tu. Ila walikuwa wanazingua kweli, au wewe unasemaje. Eti jamaa miaka 9 alikuwa anajifunza kuchapa vitabu tu! Loo!

Ila kwa miaka hiyo ilikuwa lazima. Maana upatikanaji wa taarifa ulikuwa adimu sana. Siku hizi vijana tuna raha zetu asikwambie mtu. Kitu chochote kile unachotaka, unaingia Google tu na kukipata ndani ya sekunde chache. Halafu ninavyokujua wewe ukimaliza hapa utaenda kumtafuta Benjamin Franklin Google ili uone ninayosema ni sahihi au namsingizia. Kama nakuona vile.

Wanasema kwamba taarifa zinazopatikana sasa hivi ni nyingi sana kiasi kwamba hata mfalme wa karne ya 15 hakuwa na uwezo wa kuzipata. Kabisa.

Sisi tunayo hazina kubwa. Tuna mitandao ya kufundisha kwa video Kama YouTube.
Tuna mitandao ya kufundisha kwa njia ya sauti tu.
Tuna vitabu, ambavyo aidha vinapatikana kwa bei rahisi sana au bure kabisa. Wakati babu zetu hawakuwa na uwezo wa kupata hivi vitu vyote, kitu kilichowafanya waendelee kubaki nyuma. Ila sisi tunavyo vyote tena kiganjani.

Leo hii ukiamua kujifunza kilimo cha kitunguu ni rahisi sana ukilinganisha na babu yako miaka 60. Halafu wewe hii fursa unaichukulia poa.

Sisi hivi vitu tunavichukulia poa kwa maana tunaona vipo tu, ila kama nilivyokwambia jana, kama babu yako angekuwa anafufuka leo hii. Angeweza kukuchapa viboko maana unachezea fursa ya kujifunza.

Leo hii kuna watu wanasema kuwa ile dhana ya saa elfu kumi unaweza kuipunguza kutokana na wingi wa maarifa. Unaweza kujifunza kwa kina kitu fulani tena kwa gharama nzuri na kupunguza hizo saa.
Kitakachokufanya upunguze hizo saa ni

Moja, kujifunza kutoka kwenye makosa ya watu wengine. Wewe huhitaji kurudia makosa ambayo yamefanywa na wengine badala yake unajifunza  na kuyaepuka hayo.
Pili, kujifunza Kutoka kwa mambo ambayo watu wengine wamefanya vizuri ili uyafanye vizuri zaidi. Ni ujinga kurudia makosa ambayo yamefanywa na watu karne ya 19 wakati wameshayaandika na unaweza kuyasoma.

Labda unajiuliza nijifunze nini?
Nimeshasema, ila nasisitiza tena.
Soma vitabu,
Jifunze kupitia mtandaoni (huko Kuna blogu na tovuti zenye mambo mengi ya kukufaa).
Hudhuria semina.

Kwa leo napenda kuhitimisha na nukuu kutoka Alvin Toffler. Kwenye kitabu chake cha The Future Shock anasema, mjinga wa karne ya 21 siyo yule ambaye hajui kusoma, bali anayejua kusoma ila hasomi.

Kijana kama unajua kusoma ila husomi basi wewe ni….(mimi naishia hapo, usije ukanipiga mawe bure)
    

Nimeandika kitabu kinachoitwa MAISHA NI FURSA;  ZITUMIE ZIKUBEBE. Kitabu hiki ninaenda kukizindua rasmi tarehe 1.10.2021.

Ila habari njema ni kuwa leo hii unaweza kuweka oda ya kupata kitabu hiki. Na kwa atayaweka oda;
Kwanza atapata kitabu kwa bei ya punguzo.
Pili, nitampa vitabu vingine vya ziada kama zawadi; tena hivyo vitabu vingine vya zawadi nitavituma leo hii baada ya mtu huyo kuweka oda.

Kuweka oda utalipia, elfu kumi tu (10,000/-) tu. Ila kwa kuwa utalipia elfu kumi leo hii, utpewa  vitabu vingine vitatu wakati ukiendelea kukisubiri kitabu cha maisha ni fursa, ZITUMIE ZIKUBEBE.
Vitabu utatavyopewa kwa sasa ni
1. KUTOKA SIFURI MPAKA KILELENI
2. SEKTA 11 ZA KUTENGENEZA MAMILIONI YA FEDHA TANZANIA
3. MAAJABU YA KUWEKA AKIBA.

Rusha elfu kumi leo kwa namba 0755848391. Upate vitabu hivyo vitatu, na kitabu cha MAISHA NI FURSA, ZITUMIE ZIKUBEBE kitatumwa kwako tarehe 1.10.2021 bila wewe kuhitajika kuongeza senti ya ziada.

Namba ya malipo ni

MPESA 0755848391
Airtel money: 0684 408 755
Kote jina ni GODIUS RWEYONGEZA.

NAKUKUMBUSHA TU: Ukituma elfu kumi leo. Taarifa zako zitatunzwa vizuri, na tarehe 1.10.2021 utatumiwa kitabu cha MAISHA NI FURSA; ZITUMIE ZIKUBEBE bila kuongeza senti ya ziada, wala bila kutukumbusha tukutumie.

Karibu.

Vitabu vyote ni soft copy.

Ni mimi
GODIUS RWEYONGEZA
+255755848391
MOROGORO-TZ


One response to “Fursa Tano Ambazo Vijana Wa Siku Hizi Wanachezea (SEHEMU YA PILI)”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X