Jinsi Ya Kufanya Na Kukamilisha Majukumu Yako Kwa Wakati


 

 

Rafiki yangu hongera sana kwa siku hii nyingine ya kipekee sana. Karibu sana kwenye makala ya siku hii ili uweze kujifunza kitu kipya na kuchukua hatua. Na leo tunaenda kuona ni kwa jinsi gani ambavyo unaweza kufanya kazi na kuzikamilisha kwa wakati. yafuatayo ni mambo muhimu ya kuzingatia.

1. UNAPASWA KUHAKIKISHA KWAMBA UNALIJUA JUKUMU LENYERWE

Kwenye zama za siku hizi ni rahisi sana kwa mtu kuingia kwenye mitandao ya kijamii na kujikuta kwamba yuko bize anafanya kitu wakati hakuna chochote cha maana kinchofanyika. Hivyo, ni jukumu lako kubwa kuhakikisha kuwa unalijua jukumu lako ambalo unapaswa kulifanya na kuhakikisha kwamba unajua umuhimu wa hilo jukumu kwako. Mara zote majukumu yale ya muhimu ndiyo yanapaswa kufanyiwa kazi kwanza kabla ya majukumu mengine kiasi kwamba kama muda utaisha basi haya majukumu ambayo si ya muhimu yanaweza kusalia na yasilete tatizo lolote.

 

2. WEKA NGUVU ZAKO ZOTE KWENYE HILO JUKUMU MOJA

Sasa ukishalifahamu ni jukumu gani ambalo unaenda kufanya, kinachofuata ni wewe kuhakikisha kwamba unaweka nguvu zako zote kwenye hilo jukumu lililo mbele yako. Hakuna kugawa nguvu zako kwenye majukumu mengine mengine. Jukumu lillo mezani linapaswa kufanywa kwanza kabla ya jukumu jingine.

Akili, muda wako, na nguvu zako zote zinapaswa kuelekezwa kwenye jukumu moja lililo mezani kwako.

 

3. USIRUHUSU WAGENI  AU SIMU ZIZIZO ZA LAZIMA WAKATI WA KAZI

Jiwekee utaratibu kuwa wakati unafanya kazi hakupaswi kuwepo na watu ambao wanakuja kwako kuongea na wewe wanavyojisikia na kuondoka. Hii itakufanya wewe usahau kazi yako kwanza na kuanza kuongea na mgeni wako, huku ukipoteza umakini ule uliokuwa nao kwenye kazi. hivyo, ni muhimu sana kuhakikisha kwamba wageni wanapokuja kunakuwa na namna ya kufanya wageni wasiweze kufika kwako moja kwa moja unapokuwa na kazi. inabidi wageni wasubiri mpaka utakapokuwa umemamaliza kazi au la inabidi wageni wawe na miadi ya kuonana na wewe kwanza ili hiyo ikusaidie wewe kuweza kupangilia ratiba yako kwa usahihi.

 

Kitu kama hiki unapaswa kukifanya kwa simu yako pia. Hakikisha kwamba hakuna mtu ambaye anakusumbua kwenye simu wakati unaendelea na kazi. na ili kuwezesha hili hapa unaweza kuweka simu yako kwenye flight mode au total silence(siku hizi simu nyingi zina uwezo huu hapa). au la unaweza kuacha simu yako mbali kidogo na eneo ambapo unafanyia kazi. kiufupi ni kwamba hakikisha unapofika muda wa wewe kufanya kazi hakuna kitu chochote ambacho kinakuwa mbele yako kukusumbua.

 

4. USIRUHUSU MAWAZO YAKO KUHAMAHAMA

Sasa kama umeweza kudhitibiti hivyo vitu vyote, kikwazo kukubwa ambacho wewe utabaki nacho na ambacho kinaweza kukutafuna ni ni wewe mwenyewe. Mawazo yako yanaweza kuwa yanahama kutoka eno moja kwenda eneo jingine. Sasa kitu muhimu unachohitaji hapa ni kuhakikisha kwamba mawazo yako yote yapo kwenye kazi ambayo unaifanya kwa wakati husika bila ya kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine

 

Rafiki yangu hizo ndizo njia zenye uwezo wa kukufanya wewe ukamilishe majukumu yako kwa wakati na kwa ubora pia. Ukiwa na visumbufu vingi wakati wa kazi ni rahisi sana kwako kufanya kazi ambayo si bora au la utajikuta kwamba unamaliza siku yako ukiwa umechoka sana ila kiuhalisia ukiulizwa ni kazi gani kubwa ambayo umeweza kuifanya basi kazi hiyo haitaonekana.

 

Umekuwa nami rafiki yako Godius Rweyongeza

 

 

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X