Haya Ni Maajabu Yaliyojificha Kwenye Kutoa


 

Rafiki yangu kuna nguvu kubwa sana katika kutoa. Hii ni tabia ambayo unapaswa kujifunza na kuifanyia kazi kila siku. Nadhani utakuwa umewahi kusikia kuwa matajiri wana hadi mashirika ambayo yanahusika na utoaji. Kwa mfano, Bill Gates ana shirika la GATES AND MELINDA FOUNDATION. Elon Musk ana shirika la MUSK FOUNDATION na mabilionea wengine pia wana mashirika ya aina hiyo au wamejiunga moja kwa moja na shirika la Bill Gates.

 

Sasa hili suala la kutoa linaweza kuwa linakuchanganya kidogo. wewe unaweza kuwa unaona kwamba hauna kitu cha kutoa. Au pengine unasubiri mpaka pale utakapokuwa milionea au bilionea ili utoea. Ila ukweli ni kwamba hakuna binadamu ambaye ni masikini kiasi cha kukosa kitu cha kutoa. Hivyo, katika ngazi yoyote ile ulipo, una uwezo wa KUTOA.

Na hapa ninapozungumzia kutoa simaanishi kwamba, utoe fedha peke yake. Fedha ni kipengele kimojawapo cha kutoa kwa watu. ila kuna vitu vingine ambavyo unaweza kutoa ikiwa ni pamoja na muda wako, nguvu zako, furaha yako, kuwasaidia watu kutengeneza maisha bora na utajiri, kuwaburudisha watu kwa kipaji chako n.k

 

Rafiki yangu, kwa kuangalia kitu kama hicho ni wazi kuwa wewe hapo huwezi kukosa kabisa kitu cha kutoa. Kwa hiyo kwenye malengo yako ambayo unaweka kuanzia leo hii hakikisha kwamba unaweka malengo ya kutoa na kuwasaidia watu. hata ukiweza kumsaidia mtu ambaye alikuwa na mawazo na haelewi anaenda kufanya nini na maisha yake bado utakuwa umetoa na huo ni msaada mkubwa.

 

Dunia ina maajabu yake kwenye kufanya kazi, siku zote inahakikisha kuwa unapotoa na wewe inakutengenezea mazingira ya kupata zaidi. Na sio lazima upate kile ambacho wewe umetoa. Unatoa kile ulichonacho ila dunia inakurudishia kitu kitu kingine ambacho wewe  hukuwa nacho na tena kwa wingi zaidi. Yaani, ni kama dunia inakuwa inakutunzia zile zawadi zako unazotoa kwa watu na baadae inazibadilisha na kuzirudisha kwako kwa njia ambayo wewe hapo awali hukutegemea.

 

Kwa hiyo kuanzia leo hii, hakikisha kuwa kwenye malengo yako unakuwa na malengo ya KUTOA. Kwa watu au jamii ambayo imekuzunguka.

Nakukumbusha tena, ninapozungumzia kutoa hapa sio lazima utoe fedha. Inaweza kuwa ni muda wako, nguvu zako, akili yako, kicheko chako, kuwafanya watu wafurahi, kuwafanya watu watengeneze fedha, vitabu, kuwafundisha watu unachojua ila wao hawajui n.k. kuna njia nyingi sana za kutoa. Wewe huwezi kukosa walau kitu kimoja cha kutoa kwa jamii au watu ambao wamekuzunguka.

Vitu muhimu unavyopaswa kuepuka kwenye kutoa.

1. achana na dhana ya kutoa pale unapotaka kupewa

2. usitegemee kupata kitu kutoka kwa yule mtu ambaye umempa. Na wala usianze kumsumbua mtu kwamba unajua mimi nilikusaidia kipindi fulani sasa na wewe unapaswa kunisaidia. Huo sio utoaji bali ni UUZAJI.

3. usimlazimishe mtu kupokea kile kitu unachotoa. Kama mtu hataki wewe achana naye endelea mbele utatoa kwa mwingine ambaye yuko tayari kupokea.

 

Kabla sijamalizia kipengele hiki hapa cha kutoa, basi ningependa nikwambie pia kuwa kutoa kunaendana sana na kupokea. Wewe pia unapaswa kuwa mpokeaji mzuri. Moja ya kitu kinachowafanya watu kuwa masikini ni kwa sababu sio wapokeaji wazuri. Dunia huwa inatoa fursa mbalimbali kwa watu. sasa kama mtu sio mpokeaji mzuri ndio unakuta fursa zinapita.

Hivyo jifunze kupokea pale kitu kinapotolewa kwako.

 

Baada ya kupokea shukuru. Tena sio tu ushukuru baada ya kupokea. Shukuru hata kabla ya kupokea. Kwenye Biblia utakutana na Yesu ambaye katika maombi yake alikuwa anaanza na shukrani hata kama kitu alikuwa bado hajakipokea. Utakuna na na maneno kama BABA NAKUSHUKURU….

Kwa hiyo na wewe jenga utaratibu wa kushukuru kwa kile ulichonacho sasa hivi. Shukuru kwa hali ambayo unayo sasa hivi. Shukuru kwa vitu ambavyo umepata kipindi cha nyuma, sasa hivi na vijavyo.

Kushukuru ni kama kunakuwa kunafanya zawadi zizidi kumiminika kwako zaidi.

 

Rafiki yangu, bila shaka hiki ulichojifunza hapa unaenda kukifanyia kazi bila kuchelewa.  nakushukurusana kwa kuweza kusoma andiko hili hapa mpaka mwisho. Nikutakie kila la kheri.

SOMA ZAIDI; Hiki ni kitu kimoja ninachokijua kuhusu wewe

Umekuwa nami,

GODIUIS RWEYONGEZA

0755848391

MOROGORO-TZ

 

, ,

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X