Maswali Matatu (03) ya Kukusaidia Kuwa Tajiri


Utajiri hauwezi kuja kwa siku moja labda ikitokea ukashinda kwenye bahati na sibu au ukapata mali za kurithi.

Watu waliofanikiwa huwa hawajengi uchumi binafsi kwa siku moja bali ni mpango wa mda mrefu wa kukuza na kudumisha mali zao.
Haijalishi kipato chako ni kidogo au kikubwa ni muhimu kujua na kutambua njia unayotaka kuchukua ili kuweza kufikia mafanikio yako.
Katika makala hii tutaona maswali matatu ambayo utalazimika kuyajibu ili kujua upo katika hali gani.
Namna  utavyojibu maswali haya kutaeleza kitu gani unakosa, wapi unataka kwenda na msaada gani unahitaji  ili kjiinua.
Swali # 1. Je, una mtazamo gani kuhusu pesa?
Mtazamo wako wa pesa ni jinsi unavyofikiri kuhusu pesa. Mtazamo wako ni muhimu kwa sababu ndio hukuleta katika mawazo yako kuhusu pesa. Matendo na tabia zote hutokana na mawazo na mtazamo.
Nataka uwe na mtazamo chanya kuhusu pesa na uende katika njia chanya na uondokane na vitu vinavyokushikiria na kukurudisha nyuma.
Kama unafikiri hauna bahati kwa sababu umeanza kujifunza kuhusu pesa ukiwa umechelewa, au hukwenda chuo au hukupata kazi unayoitaka huu hapa ni muda wa kuondokana na mtazamo huo hasi.
Haijalishi unafanya kazi ya chini sana au au kazi nzuri ambayo inalipa msahara mzuri sana, mtazamo wako wa pesa ndio ufunguo wa wewe kuwa na mali ya kudumu. Uwezo wa wewe kuwa tajiri hautegemei aina ya kipato unachoingiza, hata kama utaingiza pesa kiasi gani itakuja kuisha kama hujui mambo muhimu. Mfano ni muhimu kujua kwamba haupaswi kuwa na matumizi makubwa zaidi ya kipato chako.
Utakuwa umesikia watu waliokuwa maarufu wakicheza mpira au wasanii waliokuwa wakiingiza mamilioni ya pesa kwa mwaka, lakini baada ya kustaafu wakaishia kuwa maskini ingawa walikuwa wanatengeneza kiasi kikubwa sana. Ukweli ni kwamba kila mtu anaweza kuishia kuwa maskini bila kujali pesa kiasi gani anaingiza. Vilevile kila mtu anaweza kuwa tajiri kama atakuwa na mtazamo chanya wa pesa, atafanya uwekezaji wa kutosha na kuweka akiba.
Swali # 2. Je nina malengo sahihi ya kipesa?
Hili ni swali la pili la kujiuliza kwa maneno mengine tunaweza kusema;
Je unavijua vipaumbele vyako na umeviwekea mpango mzuri wa kifedha? Na je umevipa thamani?
Kuvipa vitu thamani ni kuamini kwa undani kwa baadhi ya vitu kama vile kuwa huru, kuwa na uhusiano mzuri, kuwa na afya njema, na kuwapa watoto wako msingi mzuri wa kipesa.
Njia mojawapo ya kuangalia kama kipato chako kinaendana na vitu unavyovipa thamani ni kuangalia kwenye bajeti yako kama unayo.
Mfumo wako wa kutumia hela katika bajeti utakwambia vitu gani unavipa thamani.
Ili kuwa na uhakika unataka kuifanyia nini pesa yako unapaswa kujua lengo la msingi ni lipi,?
Mtazamo wa mtu wa maisha ya baadae ni tofauti. Kuna mwingine ana mpango wa kustaafu mapema, mwingine kununua nyumba nzuri na mwingine kuhamia sehemu nyingine mjini au kijijini n.k.
Ukishajua ni vitu gani unavipa thamani  kwa mfano elimu ya watoto wako. Sasa unaweza kuweka lengo kuu. Jiwekee mpango, unataka uweke kiasi gani na kwa muda gani?
Swali # 3. Je, nina mpango mzuri na ninaufuata?
Hili pia ni swali zuri la kijiuliza kama una mpango mzuri wa kifedha na unaufuata. Kama mapato yako ni sawa na matumizi yako hii ni ishara tosha kwamba unapaswa kuwa na na mpango mzuri na bajeti.  Mpango wako na bajeti vitakusaidia kujua vipaumbele ni vipi. Utakuwa dira yako ya kukutoa sehemu moja kwenda nyingine. Weka mipango midogomidogo ambayo yote italenga kukamilisha mipango mikubwa mikubwa.
Endelea kusoma makala za kuelimisha na kuhamasisha kutoka kwenye blogu hii.

Ni mimi rafiki na ndugu yako 
Godius Rweyongeza
Tuwasiliane 
godiusrweyongeza1@gmail.com
0755848391
Asante.
Unaweza kuupenda ukurasa wangu ya facebbook kupitia

fb.me/songambeleblog


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X