Kwa kawaida mtu ukitaka kufanya jambo fulani la maana basi kila mmoja huwa anakuja na kauli zake na mtazamo wake.
Wako baadhi ambao hutoa kauli fulani ambazo hulenga kukukatisha tamaa ili usiendelee
Baadhi ya kauli hizo ni kama ifuatavyo.
1. Unapoteza mda.
Hawa husema hivi wakijua wewe hutaweza kufikia ndoto yako ambayo imo akilini mwako.
Ni muhimu kufahamu kwamba wewe ndiye uliye na maono na wewe ndiye mwenye uwezo wa kuona uendako. Hakuna mtu mwenye uwezo wa kuona kule ambako wewe unapaona. Usiwasikilize hao wewe songa mbele.
Hakikisha malengo yako umeyapanga vizuri. Weka mpango wako na jinsi utakavyoukamilisha hatua kwa hatua
Anza sasa usisubiri mpaka pale utakapokuwa umejiandaa vizuri. Nakuhakikishia siku ambayo utakuja kusema nimejiandaa vizuri haipo. Kila siku utakuwa unaona bado kuna kitu fulani hujakamilisha na kuendlea kusema najiaandaa. Anza sasa. Kama hauko tayari sasa hutakuja kuwa tayari.
2. Hilo huliwezi, fulani alifanya akashindwa.
Mtu wa aina hii anayekwambia kauli kama hiyo ni mwoga wa kufikria na mwoga wa changamoto.
Cha msingi ni kwamba kushindwa kwa fulani hakuwezi kukufanya na wewe kushindwa, yawezekana alishindwa kukabiliana na changamoto na kuzitatua.
Kumbe kushindwa kwake kuwe chanzo cha wewe kufanikiwa. Fuatlia ujue ni nini yeye kilimfanya ashindwe, anza mara moja na uwe tayari kukabiliana na changamoto. Kadri utakavyoweza kutatua changamoto zaidi ndivyo utakavyokuwa katika hali nzuri ya kufikia mafanikio.
Ni muhimu sana kufahamu kwamba sio kila mtu anaweza kukushauri katika kile unachofanya. Mtafute mtu ambaye amewahi kufanya jambo fulani ambalo na wewe unataka kufanya ili aweze kukupa mwongozo juu ya jambo fulani. Nakuhakikishia huwezi kupoteza mda. Waache wao wapoteze mda kwa kukujadiri wewe. Songa mbele.
3.Haya mambo waachie wazungu.
Hii ni kauli nyingine ambayo watu hupenda kuitumia ilil kukatisha tamaa. Mfano, nilipomwambia rafiki yangu kwamba nimeanzisha blogu alinijibu hivi “ haya mambo ya kutengeneza na kuendesha blogu waachie wazungu?”
Je, wewe kuna mtu amewahi kukwambia hivi?
Kiujumla mtu huyu naona anatawaliwa na utumwa akilini mwake, hali ambayo inamfanya yeye ajione hawezi kufanya jambo la maana isipokuwa wazungu tu.
Ebu jiulize swali hili “ wazungu wana nini ambacho mimi sina kiasi kwamba baadhi ya mambo niwaachie wao ?”
Ni aibu kubwa sana kukuta mtu anatoa kauli kama hiyo. Hakuna jambo ambalo haliwezekani ukiamua. Kwa hiyo amua sasa akilini mwako kwamba nataka kufanya jambo fulani. Jiwekee utaratibu wa kujisemea na kujikumbusha na kufikria kile ambacho kipo kwenye mpango wako kila siku.
Kwa uhakika kelele za kukatisha tamaa zipo kila kona, usiogope.amua sasa, anza sasa, wakati ni sasa, songambele
Ni rafiki na ndugu yako
Godius Rweyongeza
Tuwasiliane.
godiusrweyongeza1@gmail.com
0755848391
Endelea kusoma makala za kuelimisha na kuhamasisha kutoka kwenye blogu hii.